NYUMBA SITA ZAUNGUA KWA WAKATI MMOJA HANDENI. - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 21 September 2026

NYUMBA SITA ZAUNGUA KWA WAKATI MMOJA HANDENI.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (MCC), Rajabu Abdulrahaman Abdallah (kulia), akimkabidhi Shilingi Milioni 5, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Samwel Nyamwese ikiwa ni ni msaada wake kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Kitongoji cha Kwedifonyela, Mtaa wa Kwedigunda, Mkata wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, ambao nyumba zao zimeteketea kwa moto. 

Na Denis Chambi Tanga.


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri Taifa (MCC) Rajabu Abdallah amechangia kiasi cha Shilingi Milion tano ikiwa ni faraja kwa wananchi waliounguliwa na nyumba zao katika mtaa wa Kwedigunda Kijiji cha Mkata Mashariki Wilayani Handeni.


Tukio hilo linalodaiwa kutokea  saa 9 za  usiku limeibua maswali baada ya nyumba  zote sita kuungua kwa wakati mmoja licha ya kuwa zipo katika maeneo tofauti tofauti hali ambayo imemfanya Mwenyekiti huyo kuagiza ufanyike uchunguzi wa haraka na sheria  zifuate mkondo wake kwa yeyote atakayekutwa na hatia.


Akizungumza katika Mkutano wa hadhara wa Chama hicho uliofanyika kwenye ofisi za Kijiji cha Mkata Mashariki na kuchangia kiasi hicho cha fedha amewasiisitiza wananchi kulinda na kutunza amani na kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na viashiria vyovyote vinavyoweza kuchafua amani katika jamii na Taifa kwa ujumla .


"Jambo la kujiuliza nyumba hizi zote zimeungua kwa wakati mmoja zingekuwa zimeongozana tusingekuwa na maswali yeyote lakini zipo maeneo tofauti tofauti bila shaka kuna watu walidhamiria kufanya jambo hili la uasi, nimeielekeza Serikali ufanyike uchunguzi wa kina na tupate matokeo ya haraka wale wote waliohusika watiwe kwenye mikono ya sheria wachukuliwe hatua kali, sisi hatujawahi kuishia hivyo tumezoea kuishia kwa amani Watanzania wenzangu tusichezee amani ya nchi yetu" amesisitiza Rajabu.

 

Licha ya tukio hilo ambalo limeacha kaya nne bila Makazi mmoja wa Ndugu wa karibu wa waliopata changamoto hiyo ameeleza kuwa hakukuwa na madhara yoyote yaliyotokea kwa binadamu isipokuwa vyombo na mali zote zilizokuwa ndani ya nyumba hizo ziliteketea.


Mbali na Mwenyekiti Rajabu Abdallah kuchangia Milion tano na kuagiza ufanyike tathmini ya hasara iliyopatikana viongozi mbalimbali walioshiriki Mkutano huo wa Chama waliguswa na kutoa  michango yao akiwemo Mbunge wa Jimbo la Handeni vijijini  Charles Sungura aliyetoa  Milioni mbili na nusu, Mbunge wa viti maalum mkoa Mwanaisha Ulenge pamoja na  Mbunge wa Jimbo la Bumbuli  Ramadhani Singano wakichangia Milioni moja kila mmoja.


Akipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Mwenyekiti Rajabu Abdallah, mkuu wa wilaya ya Handeni Salum Nyamwese ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo amempongeza na kumshukuru Mwenyekiti pamoja na wote waliotoa michango yao kiwafariji  wananchi waliopatwa na changamoto hiyo ambayo ameahidi uchunguzi wake kufanyika kwa haraka iwezekanavyo.


Mbali na fedha zilizotolewa kwa  waathirika wa tukio hilo la moto Mjumbe huyo wa Halmashauri kuu Taifa ametoa kiasi cha Shilingi Milion 10 kwa wakina mama wanaofanya shughuli za ujasiriamali pamoja na Milion 10,500,000 kwa  kikundi cha vijana kwaajili ya kununua Pikipiki tatu zitakazotumika kwenye usafirishaji maarufu kama bodaboda ili ziweze kuwaingizia kipato

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (MCC), Rajabu Abdulrahaman Abdallah, akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio ilipoungua moja ya nyumba hizo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (MCC), Rajabu Abdulrahaman Abdallah, akisalimiana na mmoja wa wakati waliounguliwa nyumba zao.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (MCC), Rajabu Abdulrahaman Abdallah, akitoa pole kwa waliounguliwa nyumba zao.
Mkazi wa eneo hilo Ally Mganga, akizungumzia tukio hilo.
Ramadhani Hamadi Mhanga wa tukio hilo akizungumzia tukio hilo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (MCC), Rajabu Abdulrahaman Abdallah, akiwa na Mhanga wa tukio hilo Ramadhani Hamadi.


 

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Mwanaisha Ulenge, akiahidi kutoa Shilingi Milioni 1, kwa ajili ya kuwashika mkono wahanga wa kuunguliwa nyumba zao.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (MCC), Rajabu Abdulrahaman Abdallah (wa pili kushoto), akiwaa na viongozi mbaalimbali wakati wakienda kutoa pole kwa wananchi waliounguliwa nyumba zao.

No comments:

Post a Comment