RAIS wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko kutokana na madai ya ubadhirifu wa takribani sh bilioni 3.6, kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 iliyotolewa leo kwa Rais na CAG, Charles Edward Kichere Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma.
Rais Mh. Suluhu Hassan amesema katika shirika la bandari kuna ubadhirifu wa karibu shilingi bilioni nne za Kitanzania, hivyo ameagiza kusimamishwa kazi Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Mhandisi Kakoko ili apishe uchuguzi zaidi.
''Nimeona ubadhirifu mkubwa uliofaywa katika shirika la bandari, ninaomba TAKUKURU hii ni kazi maalum jishughulishe pale, ninajua Waziri Mkuu aliunda kamati na wakafanya uchunguzi kidogo pale na mambo yaliyotoka, hatua chache zilichukuliwa,"
''lakini imani yangu ni kwamba kama kuna ubadhirifu ndani ya shirika, na kwa ripoti ile ulionikabidhi jana jioni kuna ubadhirifu kama wa sh bilioni 3.6 karibu bilioni nne lakini wakati Waziri Mkuu alipofanya uchunguzi waliosimamishwa ni wa chini.Naomba mara moja kutoa agizo la kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa bandari , halafu uchunguzi uendelee," alisema Rais Samia.
CAG, Kichere Kichere amekabidhi ripoti 21 kwa Rais Samia, zikigusa maeneo mbalimbali baadhi ni kama vile ripoti ya ukaguzi wa serikali kuu, Mashirika ya Umma, Mamlaka za serikali ya mitaa, miradi ya maendeleo na TEHAMA.
Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa CAG kupitia fedha zote zilizotoka kuanzia mwezi Januari mpaka mwezi Machi zilizokwenda kwenye utekelezaji wa miradhi ya maendeleo zionekane.
No comments:
Post a Comment