KAMATI YA MIUNDOMBINU IMEZITAKA TAASISI ZILIPE KODI KWA TBA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 17 March 2021

KAMATI YA MIUNDOMBINU IMEZITAKA TAASISI ZILIPE KODI KWA TBA

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kazi zinazoendelea za ujenzi wa baarabara za juu (Flyover) mpya katika makutano ya magari ya Chang’ombe, mkoani Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mbunifu Majengo Elius Mwakalinga, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakati alipokagua mtambo mpya wa kukagua ubora wa barabara (Road Scanner System), mkoani Dar es Salaam.


Mtaalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Ladislaus Bigambo, akifafanua jambo kwa wajumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu (hawapo pichani),walipokuwa wakikagua mtambo mpya wa kukagua ubora wa barabara zote hapa nchini (Road Scanner System), mkoani Dar es Salaam.

Meneja wa Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota Mbunifu Majengo Bernard Kayemba, akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, mkoani Dar es Salaam. Ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 93.


Muonekano wa sasa wa majengo ya makazi ya Magomeni Kota ambayo yapo katika hatua za mwisho za ujenzi wake na kutarajiwa zaidi ya kaya 644 kuhamia hapo ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imezitaka Taasisi na Wakala za Serikali zinazodaiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kulipa madeni yao kwa wakati ili kuiwezesha Wakala huo kufikia malengo yake kwa wakati.

 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso amesema hayo wakati wa ukaguzi wa mradi wa nyumba za makazi za Magomeni Kota ambao ujenzi wake uko katika hatua za mwisho na kusisitiza umuhimu wa TBA kuwezeshwa ili ijiendeshe yenyewe na kuzalisha faida.

 

Mwenyekiti huyo ameipongeza TBA kwa ujenzi wa nyumba bora na kuwataka wakamilishe majengo hayo kwa wakati.

 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi wenye sifa na walioshiriki katika ujenzi huo kuajiriwa.

 

"Wizara hakikisheni wafanyakazi wenye sifa na bidii wanaajiriwa ili kuwapa motisha ya kufanya kazi kwa moyo", amesisitiza Mheshimiwa Kakoso.

 

Akizungumza katika ukaguzi huo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameahidi kuisaidia TBA kuhakikisha ujenzi wa majengo yake yanakuwa ya ubora na yanayoendana na thamani ya fedha.

 

Zaidi ya shilingi bilioni 50 zimetumika katika ujenzi wa majengo ya Magomeni Kota ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 93 na zaidi ya kaya 644 zitaishi katika majengo hayo hivi karibuni.

 

Naye, Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Mbunifu Majengo Elius Mwakalinga, amesema Wizara imejipanga kuiwezesha TBA kuwa na wataalam na vifaa vya kisasa ili kufanyakazi kwa tija na kuipa hadhi Wakala huo kwa upande wa majengo nchini.

 

Mwakalinga ameeleza kuwa watumishi wa TBA wanaokaimu nafasi zao watathibitishwa ili kuwapa nguvu ya kutekeleza majukumu yao kwa kujiamini.

 

Katika hatua nyingine Kamati hiyo imekagua mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili kati ya Gerezani hadi Mbagala (km 20.3), barabara za juu (Flyover) mbili na vituo vya mabasi unaosimamiwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na kuelezea kuridhishwa na mradi huo.

 

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amewaeleza wajumbe hao kuwa mradi unaenda vizuri na mpaka sasa umefikia asilimia 78 kwa upande wa ujenzi wa majengo.

 

Ameongeza kuwa mradi huo umetoa ajira ya wafanyakazi 1,121 ambapo watanzania ni 1,039 sawa na asilimia 93. 

 

Mradi huo unaotarajiwa kupunguza adha ya usafiri na msongamano kwa wakazi wa Dar es Salaam na kuleta tija katika shughuli za kijamii na kiuchumi unatarajiwa kukamilika baadae mwakani.

 

Aidha, wajumbe wamezungumzia umuhimu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuilinda miundombinu hiyo inayojengwa kwa gharama kubwa.

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iko katika ukaguzi wa miradi ya ujenzi inayoendelea kutekelezwa mkoani Dar es Salaam.


 


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.


No comments:

Post a Comment