Na Prisca Ulomi, WWUM, Arusha
Dkt. Zainabu Chaula, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Arusha. Ujenzi huo unafanywa kwa ubia baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na PAPU kwa gharama ya shilingi bilioni 33.58 mpaka kukamilika kwake.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Chaula ameridhika na maendeleo ya ujenzi huo na kutoa wito kwa wananchi kuzidi kuiamini Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuendelea kufanya vizuri, kwani kwa kupitia ujenzi huo nchi itanufaika kwa mikutano na vikao vya kimataifa hivyo kuingiza fedha za kigeni na kutoa ajira za moja kwa moja kwa wananchi ikiwa ni pamoja na matumizi ya vifaa na malighafi zinazotumika katika ujenzi huo zinapatikana nchini.
“Nichukue fursa hii kuwapongeza wataalamu wanaosimamia na kufuatilia ujenzi wa ofisi za PAPU, Arusha. Jengo hili litakapokamilika ndoto ya Serikali ya kujenga ofisi za makao makuu ya PAPU itakuwa imekamilika na jengo hili ni kitega uchumi ambapo sisi kama nchi tutanufaika kwa uwepo wa jengo hili nchini”, alisema Dkt. Chaula.
Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2022. Jengo hilo linamilikiwa na Serikali kupitia TCRA kwa asilimia 40 na PAPU asilimia 60 ambazo ni michango ya nchi 45 wanachama wa PAPU ambapo Tanzania ni nchi mwanachama na inachangia dola za marekani 33,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 75 kwa mwaka.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo utaleta mandhari mpya ndani ya jiji la Arusha na kutupa fahari kama nchi kuweza kutunza na kuifadhi taasisi za kimataifa nchini.
“Sisi kama Sekta ya Mawasiliano tutahakikisha jengo hili linakamilika kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi na kwa kiwango cha kimataifa ili kuonesha uwezo wa nchi kujenga majengo yenye hadhi ya kimataifa”, alisema Dkt. Yonazi.
Akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, Msimamizi wa ujenzi huo, Mhandisi Hanington Kagiraki amesema kuwa mpaka sasa ujenzi upo katika hatua ya msingi ambapo ni sawa na asilimia nne ya ujenzi na matarajio ni ujenzi kufika kwenye hatua ya kukamilishwa kwa ghorofa ya chini ifikapo mwezi disemba mwaka huu.
Aidha, aliongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo umezingatia vigezo vyote vya kujenga majengo marefu ikiwa ni pamoja na kuzingatia hali ya udongo na tetemeko la ardhi kwa kuwa Arusha ipo kwenye ukanda wa bonde la ufa.
Katibu Mkuu wa PAPU, Younouss Djubrine akiwa katika ziara hiyo, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuhakikisha kuwa ujenzi wa jengo hilo unaendelea vizuri chini ya uongozi imara wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano).
Katika ziara hiyo, Dkt. Chaula aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome, wawakilishi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Jiji la Arusha pamoja na wawakilishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
No comments:
Post a Comment