SERIKALI KUWEKEZA SEKTA YA ANGA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 22 May 2020

SERIKALI KUWEKEZA SEKTA YA ANGA

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela (kushoto) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, alipokuwa akifafanua jambo, wakati wa uzinduzi wa safari ya kwanza ya Ndege ya Shirika la Ethiopia ya kubeba mizigo ya minofu ya samaki kutokea jijini Mwanza kuelekea nchini Ubelgiji jana.

Muonekano wa ndege aina ya Boeing Dreamliner 787-8 ya Shirika la Ndege la Ethiopia ikiwa katika kiwanja cha Ndege cha Mwanza, mara baada ya kuwasili kwa safari yake ya kwanza ya kubeba mizigo ya samaki kutokea mkoani hapo kuelekea nchini Ubelgiji.

SERIKALI imewahakikishia wafanyabiashara wa samaki jijini Mwanza kuwa itaendelea kuimarisha miundombinu na kuboresha sera ya sekta ya anga ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, aliposhuhudia safari ya kwanza ya Ndege ya Shirika la Ethiopia katika safari yake ya kwanza ya kubeba minofu ya samaki kutokea kiwanja cha Ndege cha Mwanza ambapo aliwataka wafanyabiashara hao kuzalisha bidhaa zaidi ili kuuza mzigo mkubwa zaidi nje.

“Niwahakikishie wafanyabiashara kuwa kwa sasa jengo la kutunzia mizigo lipo na lina viwango vizuri, usafiri wa kusafirisha mizigo upo na soko lipo hivyo kazi kwenu kuchangamkia fursa hii” amesema Naibu Waziri Mhandisi Nditiye.

Naibu Waziri Nditiye, ameongeza kuwa tayari kuna maombi ya mashirika mengine ya ndege kutaka kusafirisha mizigo kupitia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA), Dar es Salaam na Mwanza, hivyo Wizara inaendelea kupitia maombi hayo ili kuruhusu ndege nyingi zaidi kusafirisha bidhaa mbalimbali nje ya nchi.

Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, ametanabaisha kuwa usafirishaji wa minofu ya samaki umeongeza ajira na kipato kwa wananchi wa Mwanza kwani viwanda zaidi ya kumi na tano vinazalisha minofu na kusafirisha ndani na nje ya nchi.

“Kuna ajira zimeongezeka kuanzia kwenye uvuvi wa samaki,  uzalishaji wa vifungashio mpaka kwenye viwanda vinavyosindika na kupakia samaki, hivyo niwaombe wenye viwanda kuhakikisha wanazingatia viwango na masharti ili soko liweze kuongezeka ndani na nchi” amesema Naibu Waziri Mhandisi Manyanya.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amewataka wafanyabishara mjini Mwanza kuwa na jukwaa la pamoja kujadili namna bora ya kuboresha bidhaa zinazolishwa na kuahidi kuwa Serikali ya mkoa iko tayari kutatua changamoto zozote watakazoziwasilisha baada ya zoezi la usafirishaji wa moja kwa moja kuanza. 

Aidha, Mfanyabiashara wa samaki Edwino Oking’o amesema kuwepo kwa shirika zaidi ya moja kusafirisha mzigo wa minofu wa samaki kutachangia bidhaa hizo kuwafikia wateja kwa wakati huku mzigo ukiwa na ubora kwani kumepunguza mzunguko ambapo awali minofu hiyo ilikuwa ikisafirishwa kupitia Nairobi.

“Kabla ya safari za mashirika haya mawili la Rwanda na Ethiopia tulilazimika kuutunza mzigo mpaka ndege zipatikane au kusafirisha kupitia Nairobi, lakini sasa hivi kuna ahueni kwani mashirika haya mawili yanafanya safari zake mara mbili kwa wiki kila shirika hivyo mlaji atapata bidhaa kwa wakati na ubora,” amesema Oking’o.

Shirika la ndege la Ethiopia ambalo limeanza rasmi kusafirisha mizigo ya minofu ya samaki limesafirisha zaidi ya tani 19 na limekuwa shirika la pili kuanzisha safari za mzigo kutokea Mwanza kuelekea nchini Ubelgiji, ambapo awali mizigo hiyo ilikuwa ikisafirishwa na shirika la ndege la Rwanda pekee.  

Imetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.

No comments:

Post a Comment