VIONGOZI DINI WAMLILIA MUNGU DHIDI YA CORONA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 23 April 2020

VIONGOZI DINI WAMLILIA MUNGU DHIDI YA CORONA

Baadhi ya Viongozi wa  dini wakati wa maombi ya kitafa dhidi ya Janga la Corona  yaliofanyika katika Viwanja Vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki katika maombi ya kitaifa dhidi ya janga la Corona yaliyofanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kushoto ni Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuber.

Na WAMJW Dar Es Salaam
VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya Dini wameendesha maombi maalum ya kuiombea nchi dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona. Maombi hayo yamefanyika katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Akizungumza kabla kuanza rasmi kwa maombi hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema hadi tarehe 21/04/2020, Watanzania 284 walithibitika kuambukizwa Corona, 256 wanaendelea vizuri, saba wako chini ya uangalizi, 11 wamepona na kurejea makwao na  watu 10 wamefariki Dunia.
Amesema kuwa Serikali inatambua jitihada kubwa inayofanywa na viongozi wa dini katika kuhamasisha waumini wao kuzingatia masharti na tahadhari dhidi ya Corona.
"Tuendelee kufanya kazi kama Serikali tunaendelea kutathmini kila hatua inayochukuliwa dhidi ya maambukizi ya Corona, tumeona watu wamevaa barako kwa wingi  wengine wametunia hadi vitambaa vya mkononi ili mradi kuzuia maambukizi” alisema
Waziri Mkuu ameongeza kuwa ni lazima kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya kwani yatasaidia kuondokana na maambukizi nchini na kupunguza uwezekano wa kuwa na maambukizi mapya. Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi nchini kudhibiti mizunguko isiyo lazima kwa watoto wao ili kukabiliana na maambukizi mapya.
 “Tulipofunga shule na vyuo, tulijua kuwa watoto hawana uwezo wa kuzingatia maelekezo hayo, hivyo wazazi Washiriki kudhibiti watoto  tunaamini mwenyezi Mungu anayo nafasi" alisema.
Aidha amezitaka kamati za ulinzi na usalama za mikoa kuzingatia masharti ya kinga dhidi ya ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kupandisha bei ya bidhaa ikiwemo Sukari hasa kipindi hiki kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
"Kuna baadhi baadhi ya wafanyabiashara wanaouza kilo ya sukari kwa shilingi 4,500/= ipo sukari ya kutosha, yeyote atakayekutwa akiuza kwa bei hiyo hatua kali zichukuliwe dhidi yao"
Wakiongoza maombi hayo ya kitaifa baadhi ya viongozi wa dini wamemshukuru Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuruhusu kuabudu na kuliombea taifa dhidi ya janga la Corona nchini.
Kwa upande wake Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari Zubeir alimwomba yarabi kuondosha mtihani huo wa Coronaamabao umeitikisa dunia kwasasa na kuomba waumini kuendelea kuomba kwajili ya kuondokana na janga hilo.
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Jude Thadeus Rwaichi amesema kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mlinzi wa Maisha ya mwandamu hivyo ni budi kumuomba yeye ili atupitishe salama na kuondokana na janga hili la Corona.
Pia Viongozi wengine waliongoza maombi walitoka katika  Jumuiya ya Kikristo Tanzania, Jumuiya ya Mabohora, Kanisa la Pentekoste, Kanisa la Wasabato, Mwakilishi wa Mufti wa Zanzibar na wafuasi wa madhebu ya Budha Tanzania.
Maombi haya dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu inayoambukizwa na virusi vya Corona ni mwendelezo wa maombi ya kitaifa yaliyoitishwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia tarehe 17 hadi 19 Aprili, 2020 kote nchini.
Mapema tarehe 9 Aprili, 2020 Viongozi wa Dini na baadhi ya Viongozi wa Serikali walikutana jijini na Dar es Salaam na kuazimia kufanyika kwa maombi maalum ya kitaifa yanayoshirikisha waumini wa madhebu yoye nchini ili kuiombea nchi dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

No comments:

Post a Comment