MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo amewataka wanahabari mkoani humo kuhakikisha wanajikinga kwa namna yoyote ile ikiwemo kufuata maelekezo ya wataalamu kwa kuvaa barakoa pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni kwani kazi zao zinahusisha kukutana na watu katika kutafuta habari mbalimbali zinazohusiana na Corona na nyinginezo katika kijamii.
Amesema kuwa mara kadhaa amekuwa akiwashuhudia wakitumia kipaza sauti kimoja wakati wa kuwahoji watu na hutumia kipaza sauti hicho kuripoti habari kwenye vyombo vyao, hivyo amewataka kuwa makini zaidi na kuongeza kuwa kutokana na uwezo mdogo wa waandishi hao kujikimu kuwa na vifaa vya kujikinga, ametoa wito kwa mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali kuona umuhimu wa kuwawezesha wanahabari ili wafanye kazi zao kwa usalama.
“Muwe makini sana, vinginevyo maambukizi yatawapata sana, kwasababu ugonjwa huu hauchagui, hauna Mwanahabari, hauna Mkuu wa Mkoa, hauna DC(Mkuu wa Wilaya), hauna Waziri, hauna mtu yeyote yule, isipokuwa unapenya kwa mtu ambaye hajachukua tahadhari, na tahadhari mojawapo ni kuvaa barakoa, Wanahabari vaeni Barakoa kila mahali, mjilinde, nafahamu wanahabari wa Rukwa uwezo ni mdogo hivyo nitoe wito kwa amashirika ya ndani na nje ya nchi, tutaanzia na ofisi yangu hapa ya mkoa, Katibu Tawala utafute hata boksi mbili, tatu tuwape wanahabari ili wajilinde,”Alisema.
Aidha, Mh. Wangabo amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha kuwa Taasisi zote ndani ya Mkoa zinakuwa na Vipima joto (Thermal Scanner) na kuongeza kuwa Mkoa umesambaza vifaa vya kujikinga (Personal Protective Equipment – PPE) 139 katika halmashauri nne za mkoa pamoja na kusambaza vipeperushi 12,200 vya kutolea elimu kwa jamii juu ya ugonjwa wa Corona.
Mh. Wangabo ameyasema hayo katika semina fupi iliyowakutanisha waandishi wa Habari katika Mkoa wa Rukwa na wataalamu wa afya ngazi ya mkoa pamoja na wadau wa mradi wa Lishe Endelevu unaosimamiwa na Shirika la Save the Children ambapo katika semina hiyo waandishi walipata kuelewa aina tofauti za barakoa na utendaji kazi wake, Elimu ya Lishe ya mtoto katika kipindi hiki ambacho ugonjwa wa Corona umekuwa tishio pamoja na njia za kufuata wanapotafuta habari kuanzia ngazi ya halmashauri, Wilaya na mkoa.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Lishe wa mkoa Teddy Swallo alitoa ufafanuzi juu ya namna ya kuendeleza lishe yam toto kutoka kwa mama endapo mmoja kati yao atakuwa ameambukizwa ugonjwa wa Corona na kusisitiza kuwa mtoto hatakiwi kuachishwa kunyonya kwasababu ya maambukizi na kusisitiza kuwa mama na walezi wa mtoto wanawe kabla na baada ya kumshika mtoto na wavae barakoa wakati wa kumhudumia mtoto.
“Kuna maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusiana na unyonyeshaji na ugonjwa Covid – 19, swali, virusi vya Corona vinapatikana kwenye maziwa ya mama? jibu ni kwamba hadi sasa tafiti zinaonyesha kuwa virusi vya corona havipatikani kwenye maziwa ya mama, swali, mtoto aliyepata Covid-19 ataendelea kunyonyeshwa? Jibu ni ndio ataendelea kunyonyeshwa ili aweze kupata king ana virutubishi muhimu kutoka kwenye maziwa ya mama yake na muhimu mtoto anayeumwa anyonye mara nyingi zaidi ya kawaida,” Alisisitiza.
Halikadahalika, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Emanuel Mtika wakati akijibu swali kuhusu dawa inayosemekana inatibu Corona ya kuchanganya malimao na tangawizi alisema kuwa, mchanganyiko huo utamsaidia mtumiaji kusafisha na kuimarisha kinywa chake lakini sio kujitibu ugonjwa wa Corona na kusisitiza wale wanaojisikia dalili za mafua makali waharakishe kufika katika vituo vya kutolea huduma na sio kubaki nyumbani wakitegemea ugonjwa huo utapona wenyewe.
Katika kuhakikisha elimu ya ugonjwa wa Corona inawafikia wananchi Mh. Wangabo ameshafanya vikao na viongozi wa makundi mbalimbali ya jamii, kuwaelimisha na kutoa maelekezo kwa viongozi wa kata za mwamabo wa Ziwa Tanganyika zenye bandari bubu 57, na kuunda timu za wataalamu kutoka katika sekta mbalimbali 11 kuanzia ngazi ya mkoa hadi halmashauri pamoja na kusimamia uandaaji wa mpango wa dharura wa kukabiliana na Corona uitwao Regional Covid -19 Contingency Plan ulioanza utekelezaji wake mwezi Machi mwaka huu.
No comments:
Post a Comment