Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila akikagua fedha zilizo okolewa na TAKUKURU Mkoa wa Songwe ambao wameokoa Zaidi ya million 225 fedha za mapato ya ndani na za vyama vya Ushirika. |
Sehemu ya fedha kati ya zaidi ya milioni 225 zilizo okolewa na TAKUKURU Mkoani Songwe zikiwa zimewasilishwa kwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe. |
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Songwe imeokoa jumla ya shilingi milioni 225.25 fedha mbichi za mapato ya ndani pamoja na fedha za Vyama vya Ushirika.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Songwe Damas Suta amekabidhi fedha zilizookolewa kwa Katibu Tawala Mkoa wa Songwe jana na kuongeza kuwa fedha mbichi ni zile ambazo zilikusanywa na watendaji kisha hawa kuziwasilisha na za Vyama vya Ushirika ni madeni ya muda mrefu.
Suta amesema shilingi milioni 150.8 zimetoka kwa watendaji walio kusanya mapato ya ndani kutoka katika halmashauri tano za Mkoa wa Songwe kisha fedha hizo hazikuwekwa katika akaunti za halmashauri kama inavyotakiwa huku shilingi milioni 74.4 na mizani 17 zikiwa ni mali za Vyama vya ushirika ambapo yalikua madeni ya muda mrefu yasiyolipika.
Amesema licha ya kuwa ni jukumu la TAKUKURU Kufuatilia matumizi ya mali za umma endapo yapo sahihi, mnamo February 2020 Mkuu wa Mkoa wa Songwe aliwaagiza kufuatilia mapato ya halmashauri zote za Mkoani hapa yanayokusanywa kwa mashine za POS lakini pia Novemba 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaagiza kurudisha madeni na mali za vyama vya ushirika zilizopo katika mikono ya watu binafsi.
Suta ameongeza kwa kuwakumbusha viongozi wa halmashauri wenye dhamana ya kusimamia mapato wahakikishe wanatekeleza jukumu hilo bila kusuasua wala uoga huku akitoa wito kwa wakusanya mapato ya serikali kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kwa kufata taratibu na sheria zilizo wekwa.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila ameipongeza TAKUKURU kwa kazi ya uokoaji wa fedha hizo na kuongeza kuwa upotevu wa fedha za makusanyo ya ndani ya halmasahuri sio changamoto ya Mkoa wa Songwe pekee isipokuwa Songwe imeamua kufanya kazi kwa uwazi Zaidi.
Kafulila amesema, “ingewezekana haya ya kuokoa fedha yakafanyika bila ya wananchi kujua ila sisi Songwe tumeamua wananchi wa Songwe lazima wafahamu masuala ya fedha za Umma na kama kuna kasoro zimetatuliwa vipi na kimsingi hizi ni zama za kumuonyesha Mwananchi kila penye kasoro pame tatuliwaje na sisi Songwe tutafanya kazi kwa uwazi katika hatua zote”.
Ameongeza kuwa tathimini ya Kasoro za kwenye mfumo wa mashine za kukusanyia mapato (POS) itafanyika kwakuwa baadhi zilionyesha kuna watu wanadaiwa fedha nyingi kuliko uhalisia ila baada ya tathmini endapo kuna watakaobainika kuwa bado wanadaiwa fedha TAKUKURU iendelee kuwachukulia hatua.
No comments:
Post a Comment