WAKUU WA SHULE ENDELEENI KUDHIBITI MICHANGO HOLELA-MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 14 March 2020

WAKUU WA SHULE ENDELEENI KUDHIBITI MICHANGO HOLELA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Wadau wa Elimu wa Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi, kwenye kikao cha maendeleo ya elimu, kilichofanyika katika ukumbi wa Narung’ombe, Machi 14, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa shule zote nchini wahakikishe wanaendelea kutekeleza agizo la Serikali la kudhibiti michango holela kwenye shule zao.

Amesema lengo la elimu msingi bila ada ni kuleta ujumuishi kwa watoto wote hususani wale wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo wapate fursa ya kusoma.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Machi 14, 2020) wakati akizungumza na wadau wa elimu wilayani Ruangwa kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Narung’ombe.

Amesema sekta ya elimu ndio wakala wa mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia na kijamii katika nchi yoyote, hivyo ni muhimu ikapewa kipaumbele kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Pia, Waziri Mkuu amesema ili sekta hiyo iweze kupata mafanikio tarajiwa ni lazima wazazi na walezi nao washiriki kikamilifu katika kufuatilia mienendo ya watoto wao kwa kuhakikisha wanakwenda shule badala ya kuliacha jukumu kwa walimu pekee.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewapongeza walimu wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa bidii waliyokuwanayo katika utendaji kazi hali iliyowezesha wilaya kuwa na matokeo mazuri katika mitihani mbalimbali ya Kitaifa.

“Kazi mnayofanya inaonekana, nawasihi muendelee hivi hivi na wilaya yetu itaweza kuendelea kupiga hatua kielimu. Pia muwaelimishe wazazi na walezi juu ya umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya vijana wetu.”

Akizungumzia kuhusu, homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona, Waziri Mkuu amewasisitiza wadau hao wa elimu wakiwemo walimu kwenda kuwaelimisha wanafunzi na wananchi namna ya kujikinga na virusi hivyo ikiwa ni pamoja na kutosalimiana kwa kushikana mikono.

Kwa upande wake, Afisa Elimu (Sekondari) wilaya ya Ruangwa Mwalimu Ernest Haule amesema katika mwaka masomo wa 2020 asilimia 86 ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza waliripoti katika shule walizopangiwa.

Akizungumzia kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya elimu wilayani Ruangwa amesema ni pamoja na upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pamoja na utoro kwa wanafunzi.

Naye, Afisa Elimu Mkoa wa Lindi, Vicent Kayombo amewapongeza wadau wa elimu kwa ushirikiano wao uliosababisha wilaya ya Ruangwa kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali ngazi ya Taifa.

Amesema baada ya kuona wadau wa wilaya hiyo wakiongozwa na Halmashauri wameanzisha utaratibu wa kugawa zawadi kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri waliagiza halmashauri zote mkoani Lindi kuiga utaratibu huo wa kuwatambua waliofanya vizuri.

Waziri Mkuu ameungana na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kugawa zawadi kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya Kitaifa ya kidato cha sita, nne na darasa la saba.

No comments:

Post a Comment