WAZIRI HASUNGA AFUTA MIKUTANO YA WADAU WA KILIMO KUJIEPUSHA NA CORONA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 23 March 2020

WAZIRI HASUNGA AFUTA MIKUTANO YA WADAU WA KILIMO KUJIEPUSHA NA CORONA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)

Na Mathias Canal, Dodoma

KUTOKANA na kuwepo kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu ujulikanao kama corona Wizara ya Kilimo imeamua kufuta mikutano yote ya wadau wa mazao ya kilimo iliyopangwa kufanyika kati ya mwezi Machi na Aprili, 2020 hadi hapo baadae maelekezo yatakapotolewa na kuziagiza Bodi za mazao na Taasisi zote zinazohusika na mazao kuendelea na matayarisho ya nyaraka na miongozo mbalimbali itakayotumika katika msimu wa mwaka 2020/2021.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 22 Machi 2020 Ofisini kwake Jijini Dodoma na kuongeza kuwa Serikali haitajihusisha na upangaji wa bei za mazao ya wakulima kuanzia mwaka 2019/2020, badala yake vyama vya ushirika na wakulima wote kwa kushirikiana na wadau mbalimbali vimeagizwa kupanga bei za mazao kwa kuzingatia bei za masoko ndani na nje ya nchi.  

Kutokana na kuwepo kwa ugonjwa wa corona, minada yote itakayoendeshwa kwenye vyama vya ushirika vya korosho, kahawa, tumbaku, mkonge, pamba, n.k lazima mikusanyiko isiwe mikubwa na watu wakae mbali kati ya mita 2 na kuendelea kati ya mtu na mtu ili kupunguza msongamano.

Aidha, taasisi za Wizara ya Kilimo zinazoshughulika na mazao, zinatakiwa zianze matayarisho ya kuanza kununua mazao mbalimbali, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA na taasisi ya Bodi ya Mazao Mchanganyiko zinatakiwa kujipanga kwa ajili ya kuanza ununuzi kwa mwaka 2019/2020.

Vile vile vyama vya ushirika wa mazao mbalimbali kama mahindi, mchele, choroko, dengu, mbaazi, kahawa, tumbaku, pamba, korosho n.k vinatakiwa kuanza maandalizi ya ununuzi wa mazao hayo kwa msimu ujao.  Pia wanunuzi wa mazao kama pamba, kahawa n.k wanatakiwa kulipa tozo za ushirika na Halmashauri kama ilivyokubalika katika vikao vya wadau haraka iwezekanavyo.

Kuhusu Muhtasari wa uchambuzi wa ukaguzi wa Vyama vya Ushirika uliofanyika katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai-Disemba 2019 amesema kuwa katika kipindi cha miezi sita jumla ya vyama 3,160 vimekaguliwa. Kati hivyo vyama vikuu ni 35, vyama vya mazao (AMCOS)  ni 1,882, vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) 1,059 na vinginevyo ni 184.

Katika Daftari ya Mrajis wa vyama vya ushirika linaonesha kuwa kuna vyama vya ushirika 11,149 ambapo Vyama 3,436 vitafuta rasmi tarehe 17 April 2020.

Ameyataja matokeo ya ukaguzi huo uliohusisha vyama 4413, vyama 69 vimepata hati inayoridhisha, Vyama 1545 vimepata hati ya mashaka, Vyama 330 vimepata hati isiyoridhisha huku vyama 1216 vikiwa vimepata hati mbaya.

Waziri Hasunga amesema kuwa Kwa kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi inaamini kuwa ushirika ndiyo chombo pekee cha kumsaidia mwananchi mnyonge ili kuweza kupata bei nzuri za mazao yao, kuwaunganisha wakulima na kuwa na maisha mazuri, ikiwa ni pamoja na kuondoa umsakini wa wanyonge, ametoa maagizo 13

Ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuanza kutoa elimu ya ushirika kwa vyama vyote nchini kwa namna ya kusimamia na kuviongoza vyama hivyo. Mafunzo ya kutunza kumbukumbu za vyama, mali, fedha na kutengeneza hesabu za mwaka pamoja na kufanya ukaguzi maalumu ndani ya mwezi mmoja kwa vyama vikuu 16 vilivyopata hati isiyoridhisha au mbaya.

Ameiagiza Tume ya ushirika katika kipindi cha miezi miwili kupitia vyama  vyote vilivyopata hati mbaya ambavyo ni vyama 1,216 na kuhakisha vinarekebisha mahesabu yao na kujibu hoja za ukaguzi sawasawa kadhalika kuhakikisha kwamba wanafuatilia taarifa ya uchunguzi maalumu ya vyama vyote vinavyotajwa kwenye ripoti kwa kufanya ubadhilifu wa fedha za vyamaVyama hivyo ni pamoja na Chama cha msingi cha IKUZU (AMCOS), Chama cha KIREKA (AMCOS), chama cha Mkombozi (AMCOS), chama cha Minaki (AMCOS) na chama cha KABERA (AMCOS).

Pia ameitaka Tume ya ushirika kukamilisha miongozo na kanuni za namna ya kupata viongozi wenye elimu, sifa na uzoefu wa kutosha ndani ya miezi mitatu ili kuweza kuajiri watu wenye weredi, mafunzo na maadili ya uongozi na kuharakisha zoezi la kubadilisha Sheria ya Ushirika ili Serikali iwe na mkono, na kumuweza CAG kufanya ukaguzi wa nje wa vyama vya ushirika vyote na uwezo wa kusimamia maendeleo ya ushirika nchini.

Waziri Hasunga ameitaka Tume ya Ushirika kuhakikisha kuwa kila mwanachama wa ushirika anakuwa na akaunti ya benki ili kurahisisha mfumo wa malipo ya fedha zao na Kila makusanyo ya mapato ya ushirika au tozo za ushirika sharti zilipwe kupitia akaunti ya benki ya chama husika na malipo yote yatolewe kupitia benki.

Pia, ameitaka Tume kuhakikisha kuwa Vyama inatengeneza hesabu za fedha za mwaka kwa kuzingatia weledi na kanuni za utayarishaji wa hesabu za ushirika za kimataifa na Katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 vyama vya korosho vyote vinapaswa kukaguliwa na CAG kwa kuwa korosho yote ilinunuliwa na taasisi ya serikali.

Kadhalika, Waziri Hasunga ameagiza kuwa Vyama vikuu vyote kuajiri mameneja wa vyama wenye sifa na weledi unayohitajika katika kusimamia mali za ushirika kulingana na ukubwa wa chama kimapato huku akisema kuwa Tume inapaswa kuimarisha kitengo cha ukaguzi wa ndani ili kuvisimamia vyama vya ushirika kikamilifu.

Katika hatua nyingine Waziri Hasunga amewataka Watumishi wa TTume ya Ushirika kuanza kubadilika ili kujenga ushirika imara na wenye matumaini kwa wananchi. Uzembe, rushwa, ubadhirifu na kutofanya kazi sawasawa ni muhimu vikapigwa vita.

Ripoti inaonesha kuwa hali ya vyama vya ushirika inaendelea kuwa mbaya kinyume na matarajio ya Serikali. Mambo yaliyosababisha hali hiyo ni pamoja na Uelewa mdogo wa viongozi wa vyama vya ushirika katika kutengeneza hesabu za ushirikaUbadhirifu wa makusudi wa mali na fedha za ushirika unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika; na Uzembe wa makusudi na kusababisha upotevu wa mazao ya wakulima;

Mambo mengine yaliyosababisha ni pamoja na Udhaifu wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato na madeni; Uelewa mdogo wa wanachama wa vyama wa kuchukua hatua na Uongozi na usimamizi mbovu wa vyama vya ushirika katika ngazi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment