NMB YAKABIDHI MSAADA WA VIFAA VYA SHULE WILAYA YA UBUNGO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 24 March 2020

NMB YAKABIDHI MSAADA WA VIFAA VYA SHULE WILAYA YA UBUNGO

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori (kulia mwenye suti) pamoja na Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam- Badru Idd (wa pili kushoto) wakikata utepe kuzinduwa madawati, viti na meza 150 katika Shule ya Sekondari Kibamba, vilivyotolewa na Benki ya NMB kuzisaidia Shule tatu za Manispaa ya Ubungo ambazo ni Kibamba na Kinzudi Sekondari na Shule ya Msingi Makuburi Jeshini kutatua changamoto za madawati leo katika Manispaa ya Ubungo.


Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Dar es Salaam - Badru Idd (kushoto) akimkabidhi msaada wa madawati, viti na meza 150 Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori (kulia) katika Shule ya Sekondari Kibamba. Vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 15 vimetolewa na NMB kuzisaidia Shule tatu za Manispaa ya Ubungo ambazo ni Kibamba, Kinzudi Sekondari pamoja na Shule ya Msingi Makuburi Jeshini zote za jijini Dar es Salaam.


BENKI ya NMB, imekabidhi msaada wa viti, meza na madawati vyote vikiwa na thamani ya Sh. Milioni 15 kwa ajili ya Shule za Sekondari Kibamba na Kinzudi na Shule ya Msingi Makuburi Jeshini, zilizoko wilayani Ubungo jijini Dar  es Salaam.

Hafla ya kukabidhi msaada huo ilifanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kibamba, ambako Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd alimkabidhi msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori (aliyekuwa mgeni rasmi).

Alisema Kibamba Sekondari yenye wanafunzi 1,365, ilikuwa na changamoto ya uhaba wa viti na meza na kwamba msaada wa NMB unaenda kupunguza kwa kiasi kikubwa adha ya wanafunzi kusoma katika mazingira yasiyo rafiki.

Naye Ofisa Elimu (Sekondari) Wilaya ya Ubungo, Hilda Shalanda, alisema kinachofanywa na benki ya NMB katika wilaya yake kwenye sekta ya elimu, ni kitu cha kupongezwa na kinachopaswa kuungwa mkono na wadau wengine kwa kuzifikia shule mbalimbali zenye uhitaji.

Aliongeza kuwa, kwa niaba ya Halmashauri ya Ubungo, wanaishukuru NMB kwa kuwa kimbilio la mahitaji ya kielimu wilayani mwake, huku akiwataka walimu na wanafunzi wa shule zilizopokea vifaa hivyo, kuvitumia kwa ustaarabu na kuvitunza.

Akizungumzia mgawanyo wa misaada hiyo, Badru alisema Shule ya Sekondari Kibamba na Kinzudi kwa pamoja zimepewa viti 100 na meza 100 (sawa na viti 50 na meza 50 kwa kila moja), huku Shule ya Msingi Makuburi Jeshini, ikipewa madawati 100.

Alibainisha kuwa, benki yake imekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ambayo imetumika kwa karibu miaka 10 sasa, ikitoa usaidizi wa utatuzi wa changamoto katika sekta za elimu, afya na majanga.

“Ni utamaduni tulioufanya kwa karibu miaka 10 sasa, lengo likiwa ni kurejesha kwa jamii sehemu ya faida yetu ya kila mwaka, lakini pia utaratibu huu unalenga kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta hizo na kuleta matokeo chanya,” alisema Badru.

Aliwataka wanafunzi wa shule za Kibamba, Kinzudi na Makuburi Jeshini, kutunza vifaa hivyo, ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kusaidia wanafunzi wa shule hizo watakaotumia kuepukana na adha za kusoma wakiwa sakafuni.

Akitoa neno la shukrani baada ya kupokea vifaa hivyo, DC Makori aliishukuru NMB kwa namna inavyoshikamana sekta za elimu na afya wilayani mwake na kwamba kwa niaba ya Serikali, wanatambua na kuthamini mchango wa benki hiyo.

“Kwa hakika NMB ni wadau muhimu wa sekta ya elimu na afya wilayani Ubungo, mmetusaidia mara kadhaa na tunawaomba msituchoke, tena muendelee kufanya hivyo kila tutakapowakimbilia, ili kusaidia pale Serikali inapoishia katika shule, zahanati na vituo vya afya,” alisema Makori.

Aliwataka wadau zaidi wa elimu kujitosa kusaidia utatuzi wa changamoto za sekta hiyo wilayani mwake kama inavyofanya NMB, na kubainisha kuwa wilaya yake kwa sasa ina uhaba wa vyumba vya madarasa 100, pamoja na madawati 7,000 ili kutosheleza idadi ya wanafunzi waliopo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Sekondari ya Kibamba, Natujwa Mrinde, kwa niaba ya wakuu wa shule zilizosaidiwa, aliishukuru NMB na kuiahidi kuvitunza vifaa hivyo, alivyokiri vimekuja kwa wakati muafaka, akiamini vitachangia kukuza ufaulu katika shule hizo.


#NMBKaribuYako

No comments:

Post a Comment