NAIBU WAZIRI MABULA AWAFUNDA MAKAMISHNA WASAIDIZI WAPYA WA ARDHI WA MIKOA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 24 March 2020

NAIBU WAZIRI MABULA AWAFUNDA MAKAMISHNA WASAIDIZI WAPYA WA ARDHI WA MIKOA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Makamishna Wasaidizi wa Mikoa alipokutana nao jana katika ofisi za Wizara zilizopo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma. Kulia kwa Naibu Waziri ni Kamishna wa Ardhi Natahaniel Nhonge.

Baadhi ya Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa Mikoa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) alipokutana nao jana katika ofisi za Wizara zilizopoMji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.


Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

NAIBU  WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa kushirikiana na wakuu wa wilaya katika kutekeleza majukumu yao ili kufanya kazi kwa ufanisi na kuondoa migogoro ya ardhi.

Dkt,Mabula alitoa kauli hiyo jana alipokutana katika kikao maalum na Makamishna Wasaidizi wa ardhi wa mikoa jijini Dodoma ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa ofisi za ardhi za mikoa ikiwa ni jitihada za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kurahisisha utoaji huduma za ardhi na kupunguza migogoro.

Alisema, ni vizuri Makamishna wasaidizi wa Ardhi wa mikoa walioteuliwa kutumia nafasi zao  kushirikiana na Wakuu wa wilaya na ofisi za Wakuu wa mikoa sambamba na kutoa elimu kuhusiana na masuala ya ardhi ili kuwajengea uelewa na ikiwezekana kuwapatia sheria za ardhi ili kupunguza migogoro ya ardhi.

Aidha, aliwataka watendaji hao wapya wa ardhi wa mikoa ya Tanzania Bara kusisitiza utendaji kazi kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa sekta ya ardhi na kutolea mfano maafisa ardhi wanaweza kushirikiana na wataalamu wa fani nyingine za ardhi katika kuandaa hati.

‘’Siyo afisa ardhi pekee anaweza kushiriki katika uandaaji hati bali wataalamu wengine wa sekta hiyo nao wanaweza kushiriki kazi hiyo maana wote wamesoma chuo kimoja na hilo limefanyika kwa baadhi ya maeneo’’ alisema Naibu Waziri Mabula

Aliwataka Makamishna hao Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa kuhakikisha panakuwepo mawasiliano kutoka Afisa mmoja kwenda kwa mwingine kwenye majalada ya ardhi na kuipongeza ofisi ya ardhi ya Kanda ya Ziwa kwa kutoa mafunzo kwa watunza kumbukumbu wa ardhi katika ofisi za halmashauri za kanda hiyo baada ya kuona watendaji wake kutofanya vizuri.

Akizungumzia utoaji hati za ardhi, Dkt Mabula alitaka kasi ya utoaji hati iongezeke na kubainisha kuwa ni vizuri waendaji hao wapya wa ardhi wa mikoa kuwasiliana na wakurugenzi wa halmashauri ili hati zitolewe kwa pamoja badala ya kila mmiliki kuifuta katika ofisi za Kanda au mkoa.

Vile vile, alisisitiza suala la upimaji maeneo yate ya umma na kupatiwa hati kwa lengo la kuepuka migogoro inayoweza kusababishwa na uvamizi wa maeneo hayo kutokana na kutopimwa.

Aidha, Dkt Mabula aliwataka makamishana hao Wasaidizi wa Ardhi wa Mikoa kuhakikisha wakati wa utendaji wao wanatilia mkazo ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi sambamba na kuingiza viwanja vyote kwenye mfumo wa kielektronik.

Kamishana Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Shinyanga Hezekiel Kitlya aliishukuru Wizara ya Ardhi kwa uamuzi wa kuanzisha ofisi za ardhi za mikoa na kueleza kuwa ofsi hizo zitasaidia sana kutoa huduma za ardhi kwa wananchi sambamba na kupunguza migogoro ya ardhi.

Kwa mujibu wa Kitlya, ili ofisi hizo za ardhi za mikoa ziweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kuna haja kwa wizara kuhakikisha ofisi hizo zinapatiwa vifaa pamoja na wataalamu wa kutosha ili kukidhi mahitaji yote ya sekta ya ardhi.

No comments:

Post a Comment