Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), Dk Agnes Kijazi. |
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa juu ya hali ya ongezekeo la joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Kwa kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia. Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine.
Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele kati ya mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. Nyakati za usiku pia kunaonekana kuwa na hali ya joto kutokana na kuwepo na kiwango kikubwa cha unyevunyevu angani kinachofika asilimia themanini na zaidi kwa baadhi ya maeneo. Unyevunyevu huo hutunza hali ya joto litokanalo mionzi ya jua na hivyo kuleta hali ya fukuto.
Kwa sasa msimu wa mvua za Vuli umeisha katika maeneo mengi hususan yale yaliyoko ukanda wa Pwani, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Simiyu, Shinyanga hivyo kuwa na joto kali. Pamoja na maeneo hayo mkoa wa Tabora nao unatarajiwa kuendelea kupata vipindi vya joto
kali.
Katika wiki ya kwanza hadi ya tatu ya mwezi Januari 2020 viwango vya juu vya joto kwa baadhi ya maeneo yaliyopo ukanda wa pwani yanatarajiwa kuwa na kiwango cha juu cha joto cha nyuzijoto 32 hadi 34 hususan kwa maeneo ya Dar es Salaam, Tanga, Unguja na Pemba Vipindi hivi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kuongezeka katika mwezi Februari 2020 wakati jua litakuwa la utosi hapa nchini.
Baada ya kipindi hicho hali ya joto inatarajiwa kuanza kupungua hasa kuelekea mwezi Machi ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka katika maeneo yanayopata mvua za msimu na kuanza kwa msimu wa mvua za masika.
Hata hivyo, taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa katika utabiri wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, hivyo tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki kila inapobidi.
Imetolewa na: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
No comments:
Post a Comment