'NILIITWA MCHAWI BAADA YA MUME WANGU KUUGUA MARADHI YA AKILI' - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 8 January 2020

'NILIITWA MCHAWI BAADA YA MUME WANGU KUUGUA MARADHI YA AKILI'

Esther Wanjiru Kiama.

KWA muda wa miaka kumi na minne ndoa ya Esther Wanjiru Kiama ilikabiliwa na pandashuka sio haba, kwa namna zote, sio mtihani ambao mwanamke yoyote anaweza kufikira kuupitia na zaidi kuuhimili.

Lakini kwa muda wote na kadri ya walivyoweza, yeye na mumewe walijizatiti kuushinikiza msingi wa ndoa yao. Hivi karibuni Esther anatimiza miaka 60. Ni mkewe David Kiama Kuru, Mama ya watoto wanne, bibi au nyanya wa wajukuu sita na hii leo, ni mtoa nasaha kuhusu masuala ya kijamii.

Licha ya kwamba ameyafikia hayo yote, ndoa yake ilikabiliwa na majaribio, wakati mumewe alipoamua kwena kutafuta riziki mbali na familia yake. Alielekea magharibi mwa Kenya kutoka mkoa wa kati, ambako alifanya kazi huko kwa takriban mwaka mmoja.

Ni baada ya kipindi hicho ndipo Esther alipopokea simu ya ghafla akitakiwa kufika mjini Bungoma mara mmoja. Ufafanuzi aliopewa ni kwamba mumewe amepatwa na 'ugonjwa wa kiakili'. Kuanzia hapo, esther anasema maisha ya jamii yake yalibadilika sana.

Kwanza kabisa, kwasababu mume wake alikuwa ndio mtafuta riziki katika familia na tegemeo kuu la wote. Esther anasema kuwa alishtuka sana kumuona mumewe akiwa amechanganyikiwa na haelewi mambo yalivyokuwa yanaendelea ni kana kwamba alikuwa katika ulimwengu wake.

Anahoji kuwa awali ilikuwa vigumu kuelewa ni ugonjwa upi aliokuwa anaugua mumewe, kwani alikuwa na ishara za 'kujisemesha mwenyewe, huku akirusha mikono hapa na kule , na vilevile kuonekana kana kwamba alikuwa anazungumza na watu waliokuwa mbali licha ya kuwa hakuna mtu karibu'.

Kuanzia hapo, Esther anasema baadhi ya marafiki wake, jamaa na hata majirani walianza kumsema na kumsimanga kwamba yeye ndiye chanzo cha maradhi anayougua mumewe wake. Wengi walimbandika majina kama 'mrogi, mchawi na mwanamke ambaye ametafuta dawa ilikumuangamiza mume wake'.

"Waliniita majina mengi...kuwa mimi ndio nimemroga mumewangu " asimulia Esther.
Lakini Licha ya haya yote aliamua kujipa nguvu na kufunika aibu ya Mumewe , lakini haikuwa rahisi kwani jamaa wa kutoka upande wa mumewe siku mmoja walimchukua kwa nguvu kutoka mikononi mwake Esther na wanawe na kumsafirisha hadi kwao mashambani huku wakisema kuwa hawakuamini kuwa Esther alikuwa na nia njema na mumewe .

Kwa miaka mitatu yeye na wanawe walitafuta njia ya kumuona Kiama lakini familia ya mumewe ikawa haitaki kabisa na kumzibia njia zote za wao kumuona. Kilikuwa kipindi kizito mno kwa Esther , japo hakukata tamaa. Baada ya miaka mitatu Esther alitafuta njia ya kumtoa kwa nguvu mumewe kutoka mikononi mwa jamii yake, alipanga njama na watoto wake ambayo ilifaulu.

"Nilipomuona mume wangu sikuamini macho yangu... afya yake ilikuwa imedhoofika sana kana kwamba hakukuwa na mtu wa kumuhudumia ipasavyo " anasema Esther.

Anasema kuwa 'kucha za miguu na za mikono zilikuwa chafu na ngumu kupindukia ilichukia siku kadhaa kuzisafisha', vile vile ndevu zake pamoja na nywele zilikuwa zimemea kupita kiasi na kumuacha kuwa na sura ya kutisha.

"Ni vigumu sana kumtizama mtu unayempenda akihangaika na ugonjwa usiouelewa vyema , ila nilijizatiti tu" aliongezea Esther.

Baada ya kumrejesha nyumbani, safari ilianza hapo ya kumtunza na kuhakikisha kuwa mume wake anapata matibabu ya hospitalini.

Mwanasaikolojia anayehusika na maswala ya ndoa na jamii kutoka Kenya, Daktari Maggie Gitu anasema kuwa sio sawa kwa jamii kuwaita wagonjwa wenye matatizo ya akili kuwaita majina kama 'wendawazimu au kichaa'.

"Sisi hatupendi kusema kuwa mtu ni wazimu, ila kama wanasaikolojia hutizama ishara anazoonyesha mngonjwa, na kutathmini ni ugonjwa upi wa kiakili anaougua mgonjwa "anafafanua Dkt Maggie.

Kwa mfano ugonjwa kama huu ambao ulimuathiri mumewe Esther Kiama, Gitu anautaja kuwa huenda ulitokana na kwamba alikuwa anapitia kipindi kigumu wakati ule , na akili yake ikawa ilishindwa kuihimili hali.

Daktari Gitu anasema kuwa magonjwa mengi ya kiakili hutokea pale kemikali kwenye ubongo wa mgonjwa inaposhuka sana na ubongo kushindwa kuhimili kazi yake ya kawaida.

Magonjwa mengi ya kiakili daktari anasema husababishwa na hali za mtu za kindani, sana sana husukumwa na hisia za upweke, hisia za hofu au kuhisi kana kwamba hupendeki au hakuna anayekuthamini.

Vile vile magonjwa kama haya anafafanua hutokea pale mtu anapohisi kana kwamba amefeli kulifikia jambo fulani katika maisha yake na kuishia kupoteza uwezo wake wa kufikiria. Njia inayotumiwa sana mbali na kutoa ushauri wa ndani kwa wagonjwa wa kiakili, ni matibabu ya kutumia dawa tofauti ambazo wagonjwa humeza katika kipindi fulani kama njia ya kuihimili hali.

Tangu mwaka wa 2017, mumewe Esther Kiama alianza kuonyesha dalili za kupona kufuatia maibabu aliyokuwa anapokea licha ya kuwa bado anatumia dawa hizo hii leo.

Esther Kiama anasema kilichompatia motisha na subira katika kipindi chote hicho ni ahadi zake za ndoa kwa mumewe alizosimama nazo wakati wa 'shida na furaha' na anasema kamwe 'hakuna kitakacho nitenganisha na mumewangu ila kifo.'
-BBC

No comments:

Post a Comment