MSEMAJI MKUU WA SERIKALI DK ABBASI AIPONGEZA PSSSF - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday 15 June 2019

MSEMAJI MKUU WA SERIKALI DK ABBASI AIPONGEZA PSSSF

Msemaji Mkuu wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dk. Hassan Abassi, (kushoto), akipeana mikono na Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF), Bi. Eunice Chiume baada ya mazungumzo yao ofisini kwa Dk. Abassi jijini Dar es Salaam Juni 15, 2019. Bi. Chiume ambaye alikuwa katika ziara ya kuvitembelea vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii jijini Dar es Salaam, amehitimisha ziara hiyo kwa kufanya mazungumzo na Dk. Abassi.

Na Khalfan Said

MSEMAJI Mkuu wa serikali, Dk. Hassan Abbasi ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuanza vizuri kutekeleza majukumu yake katika kipindi kifupi tangu kuunganishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo Juni 15, 2019 ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati alipotembelewa na Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF), Bi. Eunice Chiume, aliyefuatana na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko huo Bw. Abdul Njaidi.
Kwa takriban wiki nzima, Meneja huyo amekuwa kwenye ziara ya kuvitembelea vyombo vya habari vikiwemo vile vya mitandao ya kijamii ili kuendeleza mahusiano mema ikiwa ni pamoja na kueleza malengo ya Mfuko huo ambao ni mpya baada ya serikali kuunganisha Mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF kwa lengo la kuboresha utoaji huduma.

“Tunaposikia kuwa watu wameanza kupata mafao yao tena kwa wakati kwakweli ni jambo la faraja kwa serikali kwahiyo mpeleke salamu zangu kwa watendaji wote, akiwemo mtendaji mkuu wa Mfuko, tunaona na tunafarijika kwamba yale malengo ya serikali kuu kuunganisha hii mifuko ili kutoa huduma bora yametimia.” Alisema.
Dk. Abbasi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Malezeo, pia amempongeza Meneja huyo kwa uamuzi wa kuvitembelea vyombo vya habari kwa lengo la kuelimisha umma na kueleza shughuli za Mfuko kwani hii itasaidia wanachama kujua kinachoendelea kwenye Mfuko wao.

“Huu ni Mfuko mpya bilashaka kunakuwa na maswali mengi toka kwa wanachama hivyo elimu inahitajika ili kuondoa maswali hayo." Amefafanua Dk. Abassi
Aidha Dk. Abassi alitoa wito kwa wastaafu na wale wastaafu watarajiwa kutambua kuwa msingi wa pensheni ni kumuhudumia mfanyakazi anapokosa nguvu ya kufanya kazi ama uzeeni au kutokana na kupata madhara mengine ambayo yatakufanya ukose nguvu ya kufanya kazi.
“Niwakumbushe watanzia kuwa tuweke pesa benki zile tunazohitaji kutumia leo au kesho lakini mafao ni kwa ajili ya kukusaidia maisha ya baadaye, si vema umetumikia nchi, jamii halafu baadaye ukaishi maisha ya mashaka.” Alisema.
Awali Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Bi. Eunice Chiume alimweleza Dk. Abassi kuwa amepata fursa ya kutembelea vyombo vya habari ili kujenga na kuendeleza mahusiano ikiwa ni pamoja na kuutambulisha Mfuko huo mpya yakiwemo malengo yake.
Alisema Mfuko ulianza kutekelez amajukumu yake Agosti 1, 2018 na ndani ya miezi 6 tangu Mfuko uanze kutekeleza majukumu hayo umeweza kulipa malimbikizo ya pensheni ya mkupuo na ile ya kila mwezi kiasi cha shiljngi bilioni 880, lakini pia inaendelea na zoezi la kuhakiki taarifa za wanachama (wastaafu)  ambapo kati ya wastaafu 120,000, elfu 10 bado hawajahakikiwa.
“Kwa hiyo tumeeleza kuwa Mfuko umefungua ofisi nchi nzima bara na visiwani na kwa kila mstaafu ambaye bado hajahakiki taarifa zake afike kwenye ofisi ya PSSSF iliyo karibu naye ili atekeleze wajibu huo wa kisheria.” Alifafanua Bi. Chiume. 

 Msemaji Mkuu wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dk. Hassan Abassi, (kulia), akizungumza na Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF), Bi. Eunice Chiume, wakati Bi, Chiume alipomtembeleka Dk. Abassi ofisini kwake jijini Dar es Salaam Juni 15, 2019.

 Dkt. Abassi (kulia), akimsikiliza mgeni wake. Bi. Eunice Chiume ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

 Bi. Chiume akiziungumza.


 Dk. Abassi (kulia), akijadiliana jambo na Bi. Eunice Chiume, (katikati), na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi, mara baada ya mazungumzo yao.


 Msemaji Mkuu wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dk. Hassan Abassi, (kushoto), akipeana mikono na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa PSSSF bw. Abdul Njaidi.

Dk. Abassi akiwa na wageni wake, Bi. Eunice Chiume (katikati) na Bw. Abdul Njaidi kutoka PSSSF.

No comments:

Post a Comment