Baadhi ya jengo la zamani la kihistoria la ambalo ni kivuto cha utalii ambapo Taasisi za Uhifadhi nchini zitakuwa na jukumu la kukarabati pamoja na kuyasimamia ili kuchagiza utalii. |
SERIKALI imeanza mkakati maalum wa kuinua Utalii wa kiutamaduni na wa kihistoria kwa kuvigawa vituo 16 vya Malikale kwa Taasisi za uhifadhi nchini. Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kupitia upya sera ya Malikale ya namna ya kuyahifadhi maeneo hayo kufuatia majengo mengi ya kale na ya kihistoria kuwa katika hali mbaya ya uchakavu.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu alipotembelea mji wa kihistoria wa Mikindani katika Manispaa ya Mikindani,mkoani Mtwara ambao kwa sasa eneo lake linasimamiwa na kuendeshwa na Taasisi ya Makumbusho ya Taifa.
Amesema lengo la uamuzi huo ni kuziwezesha Taasisi zitakazokuwa na jukumu la usimamizi ziyakarabati na kuyasimamia maeneo hayo ya kihistoria ili yaweze kuchangia katika pato la Taifa kupitia sekta ya utalii nchini.
Mhe. Kanyasu amesema vituo hivyo 16 vitawekwa chini ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Makumbusho ya Taifa (NMT) pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Ameeleza kuwa Taasisi hizo zitakuwa na jukumu la kusimamia, kukarabati, kuendeleza, kuendesha pamoja kutangaza vituo hivyo vyenye utajiri mkubwa wa kihistoria na kiutamaduni.
Aidha, kwa mujibu wa tathmini ya ukaguzi iliyofanyika mwaka jana jumla ya majengo 85 ya kihistoria yalikuwa yapo hatarini kudondoka na kupotea kabisa yasipokarabatiwa. Kufuatia hali hiyo Mhe. Kanyasu amesema Taasisi hizo zitasaidia kuyakarabati majengo hayo ili yaweze kurudi katika hali yake ya mwanzo na kuwa kichocheo cha Utalii.
Akizungumzia mkakati wa kutangaza vivutio hivyo vya Malikale amesema vitakuwa vikitangazwa kwa mfumo wa vifurushi (packages) ili kuwawezesha watalii wanapokwenda Mtwara waweze kutembelea vivutio vingi vilivyopo katika mkoa huo kwa vile ni ngumu kwa mtalii kwenda Mtwara kwa ajili ya kutembelea mji wa Mikindani pekee.
‘’Tunataka vivutio vya utalii vya Kusini na maeneo mengine ya nchini yawekwe kwenye vifurushi ili mtalii akipanga kwa mfano kutembelea mkoa wa Mtwara atembelee Pori la Akiba la Lukwika Lumesule akitoka hapo atembelee majengo ya kale, ajionee vikundi vya ngoma za asili kisha aende akapumzike kwenye fukwe zetu nzuri’’ Amesema.
Awali akizungumza kuhusu majengo ya Kale, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya CCM wa mkoa wa Mtwara, Lukasi Elwesi amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa mikoa ya Kusini imejaliwa kuwa na majengo ya kale mengipamoja na fukwe ambazo hazijaguswa hivyo, ameiomba Wizara iongeze nguvu katika Kanda hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Malikale, Dkt. Fabian Kigadya amezitaka Halmshauri nchini kulinda na kuendeleza majengo ya kihistoria kwa ajili ya kuvutia watalii hali itakayosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia malikale hizo.
No comments:
Post a Comment