NMB WAKABIDHI MSAADA WA MABATI 1248, MADAWATI 62 KWA SHULE 8 MKOANI KATAVI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 5 March 2019

NMB WAKABIDHI MSAADA WA MABATI 1248, MADAWATI 62 KWA SHULE 8 MKOANI KATAVI



Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Straton Chilongola akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga (walioshikana mkono) sehemu ya msaada wa mabati 1,248 kwa ajili ya Shule 5 za Sekondari na shule 3 za Msingi zote kutoka halmashauri za Mkoa wa Katavi.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa madawati 62 yaliyotolewa na Benki ya NMB kama msaada kwa ajili ya Shule kutoka halmashauri za Mkoa wa Katavi.

Wanafunzi wakiwa na sehemu ya madawati yaliyotolewa na Benki ya NMB kama msaada.

BENKI ya NMB imetoa msaada wa mabati 1,248 na madawati 62 kwa ajili ya Shule 5 za Sekondari na shule 3 za Msingi zote kutoka halmashauri za Mkoa wa Katavi ikiwa ni kusaidia kutatua changamoto anuai kwenye sekta ya elimu.

Msaada huo uliogharimu kiasi cha shilingi milioni 40 umekabidhiwa na  Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Straton Chilongola huku akisisitiza benki hiyo itaendelea kusaidia jamii katika sekta ya afya, elimu pamoja na majanga ikiwa ni kuchochea maendeleo kwa jamii.

Akipokea msaada huo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga aliishukuru Benki ya NMB  kwa kuchangia maendeleo ikiwemo kuthamini sekta ya elimu kwa msaada huo wenye tija.

Awali akitoa taarifa, Afisa Elimu Taalum Sekondari Manispaa ya Mpanda, Raphael Mkupi amebinisha kuwa wanafunzi katika shule ya Sekondari Rungwa hulazimika kukaa wawiliwawili kwa kiti kimoja kutokana na kuwepo kwa upungufu wa viti zaidi ya 300.

No comments:

Post a Comment