Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akiwasili
kisiwani Pemba kukagua changamoto za mawasiliano. Wa kwanza kulia ni Mbunge wa
Viti Maalumu Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maida Hamad Abdallah na wa kwanza kushoto
ni Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Baucha.
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kushoto) akiwa
kwenye boti eneo la Makangale – Mnarani akikagua upatikanaji wa mawasiliano
wakati wa ziara yake Pemba. Wa kwanza kushoto ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Maida Hamad Abdallah na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mtendaji
wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga.
NAIBU Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amefanya ziara ya kukagua
upatikanaji wa mawasiliano ya simu za mkononi kwa wananchi waishio kwenye Mkoa
wa Kaskazini kisiwani Pemba na kubaini kuwa yapo baadhi ya maeneo yana usikivu
mdogo wa mawasiliano na mengine hakuna kabisa mawasiliano ya simu za mkononi.
Nditiye aliambatana na
Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maida Hamad Abdallah ambaye
ndiye chimbuko la ziara hiyo kwa kuuliza maswali Bungeni wakati wa vikao vya
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu changamoto ya mawasiliano
kisiwani Pemba.
“Zipo changamoto mbali
mbali ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, wananchi wanapata tabu za kuwasiliana
hasa nyakati za usiku hasa wakipata msiba au mgonjwa, tuliwasilisha changamoto
hizi Bungeni ili ziweze kutekelezwa,” amesema Maida.
Nditiye amebaini uwepo
wa usikivu mdogo wa mawasiliano na ukosefu wa mawasiliano wakati wa ziara yake kwenye Shehia ya
Kiungoni – Wingwi, Dodeani, Kiuyu Mbuyuni, Sizini – Chwaka, Tumbe, Kipande
Konge na Makangale – Mnarani zilizopo kwenye Wilaya ya Micheweni pamoja na
kwenye Shehia nyingine za Weni – Tungamaa – Machwengwe, Mtambwe, Mkanjuni na
Kivumoni zilizopo kwenye Wilaya ya Wete.
“Kuna maeneo ambayo
minara ipo ila mawasiliano hayana nguvu na sehemu nyingine hakuna mawasiliano
kabisa kutokana na jiografia ya Pemba, nimekuja na wataalamu wa kutoka Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), nimewaelekeza hili walifanyie kazi, raha yangu ni
kuona wananchi wote wana wasiliana,” amesema Nditiye.
Amefafanua kuwa
masuala ya mawasiliano ni masuala ya muungano ambapo Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imeanzisha UCSAF ili kupeleka mawasiliano nchi nzima,
Tanzania Bara na Visiwani kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara.
“Nimeshuhudia hapa
nilipo hamna mawasiliano na simu yangu ni kopo tu, sipati mtandao wowote”,
amesema Nditiye. Ameongeza kuwa wamejipanga kuhakikisha kuwa popote ambapo
hamna mawasiliano wanafikisha mawasiliano kwa wananchi, kwa kuwa akiwa njiani
ziarani humo ameshuhudia ukosefu wa mawasiliano.
Katika ziara hiyo,
Nditiye aliambatana na Mtendaji Mkuu wa UCSAF Mhandisi Peter Ulanga ambapo
amemwelekeza kuchukua maeneo yote ambayo hayana usikivu wa kutosha na yale
ambayo hayana mawasiliano kabisa ili waanze kuyafanyia kazi mapema mwezi
Januari mwakani.
“Tunachukua changamoto
hizi ili tuweze kuongeza usikivu wa mawasiliano” amesema Mhandisi Ulanga. Ulanga
ameongeza kuwa UCSAF itahakikisha mwananchi akiwa ndani au nje ya nyumba yake
kwenye eneo lote la kisiwa cha Pemba mwananchi anapata mawasiliano mazuri.
Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba, Omari Khamisi Othmani amemwambia Nditiye kuwa, “tuna imani
ujio wako utatuondolea changamoto ya mawasiliano katika mkoa wa Kaskazini na
kisiwa cha pemba kwa ujumla kwa kuwa umeona hali halisi,”
Sheha wa Shehia ya
Kipange, Ramadhan Omari Ahmed akizungumza kwa niaba ya masheha wenzake amesema
kuwa anamshukuru Nditiye na msafara wake pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu wa
Mkoa wa Kaskazini Pemba, Maida Hamad Abdallah kwa kupata ujio huu ili kufika
maeneo hayo ambapo amesema kuwa, “hamna mawasiliano popote ya TIGO, Vodacom au
Zante, pale tunapohitaji mawasiliano tunakwenda sehemu kama vile kupanda juu ya
mlima au uende kwenye uwanja wa mpira au kwa kutembea umbali wa kilomita 1.5
hadi 3.1 kutafuta mawasiliano,”.
“Ni faraja kubwa sana kwa kutembelewa na kuja
kusikiliza maoni ya wananchi kwa kuwa mawasiliano hayako vizuri, tukitaka
kupiga simu tukiwa ndani inatukwaza, hatupati mawasiliano, lengo tupate mawasiliano
na wametuahidi tatizo la mawasiliano sio tu kwa Kiungoni ila litaisha Pemba
yote”, amesema Shehia wa Kiungoni, Omary Khamisi Othmani.
“Kilio hiki kimetukwaza
muda mrefu, naamini alichokuarifu Maida kitafanyiwa kazi, tumefarijika sana
kuona viongozi mnashuka hadi chini kusikiliza wananchi, naamini wataalamu wako
wataifanyia kazi changamoto ya mawasiliano ili wananchi waweze kuwasiliana,”
amesisitiza Mkuu wa Wilaya ya Micheweni, Salama Mbarouk Khatib.
Katika hatua nyingine,
Nditiye amekagua vituo viwili vya TEHAMA kati ya kumi vilivyojengwa na UCSAF
kwenye kisiwa cha Unguja na Pemba ili
wanafunzi waweze kujifunza TEHAMA na wananchi watumie TEHAMA ambapo ametoa wito
kwamba wananchi waruhusiwe kutumia bure kituo cha TEHAMA kwa muda kabla ya
kuanza kuwatoza gharama za uendeshaji wa vituo hivyo ili wafaidi matunda ya
Serikali yao.
Nditiye ameongeza kuwa
mawasiliano ni ulinzi na usalama na mawasiliano ni uchumi ambapo mwananchi
akiwa na simu, inamuwezesha kuuza na kununua kiurahisi bidhaa zake, hivyo kwa
kutumia TEHAMA tunajiunga na dunia kupitia mawasiliano.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment