Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (Kulia) akikabidhi vitambulisho vya wajasiliamali kwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura. |
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo amewatahadharisha wafanyabiashara watakaogushi taarifa kwa nia ya kupatiwa vitambulisho vilivyotolewa na Rais Dk.John Pombe Magufuli kwaajili ya wajasiliamali wadogowadogo kote nchini walio na mitaji isiyozidi shilingi milioni nne.
Amesema kuwa jukumu lake ni kuvikabidhi kwa wakuu wake wa wilaya ili nao kuvifikisha kwa wakurugenzi na hatimae kuwafikia walengwa wa vitambulisho hivyo na kuongeza kuwa wajasiliamali waondoe shaka juu ya idadi ya vitambulisho hivyo kwani vikiisha vitaagizwa vingine na hakuna atakaekosa.
“20,000/= kwa kila kitambulisho, lakini kwa mtu yeyote yule ambae atakuwa “amefoji” ambae atapewa kitambulisho bila ya kustahili atanyang’anywa kitambulisho hicho na 20,000/= hazitarudi, kwahiyo nitoe angalizo kwa hawa wajasiliamali wadogo wadogo wazingatie hizo taratibu ambazo zimewekwa,” Alisisitiza.
Ameyasema hayo katika hafla fupi ya kukabidhi vitambulisho hivyo 25,000, kwa wakuu wa Wilaya tatu za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi zenye halmashauri nne, hivyo kila halmashauri kupatiwa vitambulisho 6,250.
Wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, katibu Tawala wa Mkoa huo Bernard Makali alitahadharisha kuwa vitambulisho hivyo vina alama maalum ambayo haionekani kwa macho na kuonya kuwa wananchi wasijidanganye wala kuthubutu kugushi popote walipo.
Awali akisoma masharti ya kupatiwa kitambulisho hicho Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoa wa Rukwa Fredrick Kanyiriri alisema kuwa miongoni mwa mashari ya mjasiliamali atakayekabidhiwa kitambulisho hicho ni pamoja na mjasiliamali huyo kujaza fomu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kujipambanua kwamba mauzo yake hayafiki shilingi milioni nne kwa mwaka na kulipa shilingi 20,000/= ambayo itaingia katika akaunti kodi za ndani.
Pia alifafanua “Sharti la pili ni lazima mjasiriamali huyo lazima awe hajasajiliwa TRA kwa maana ya hana namba ya utambulisho (TIN) isipokuwa tu kwa wale waliopata namba ya utambulisho huko mwanzoni kwasababau mchakato huu ulianzia TRA wa kuwatambua wajasiliamali hawa lakini lakini baada ya kukwama Mh. Rais aliamua auchukue na kuuweka katika utaratibu mwingine lakini kuna wenye TIN.”
No comments:
Post a Comment