Na Abdi
Shamnah, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka akinamama kupeana
elimu juu ya umuhimu wa kuchunguzwa saratani ya shingo ya kizazi pamoja na
kuwataka watoto wa kike kuhudhuria vituo
vya afya kupata chanjo ya maradhi hayo.
Amesema hatua hiyo itawezesha
kugundulika mapema viashiria vya kuwepo maradhi hayo na hivyo kuweza kupata
tiba sahihi na kwa wakati muafaka.
Dk. Shein amesema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa uchunguzi wa Saratani ya
shingo ya kizazi, iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil,
Kikwajuni mjini hapa.
Mradi huo wa miaka minne unatekelezwa
kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya
Afya pamoja na Kamisheni ya Afya na uzazi wa mpango, kutoka Jimbo la Jiangsu nchini
China.
Hafla hiyo imewashirikisha
viongozi mbali mbali wa Serikali, madaktari; wauguzi na wataalamu kutoka sekta
ya afya, wawakilishi wa Kamisheni ya Afya na mpango wa uzazi kutoka Jiangsu pamoja
na wadau wengine wa sekta ya Afya nchini.
Dk. Shein alisema kuna
umuhimu mkubwa kwa akinamama kuhimizana na kupeana elimu, ili kila mmoja aone
umuhimu na faida ya kwenda kuchunguzwa maradhi hayo, sambamba na kuwahimiza
watoto wa kike walio na umri kati ya miaka tisa hadi 14 kupata chanjo kama
inavyoelekezwa na wataalamu.
Alisema katika kufanikisha
jambo hilo, ni muhimu kwa akinababa kuiunga mkono jinsia hiyo ili kuepukana na
athari mbali mbali zinazoweza kujitokeza, ikiwemo uchelewaji wa kupata
matibabu.
“Nyenzo zipo na wataalamu
wapo, hivyo vyema tuzingatie usemi usemao tusifuge ndwele na waganga tele,
hakuna sababu ya kuona haya, wajitokeze katika uchunguzi, tukiona aibu tutaharibu nafasi ya kuchunguzwa’, alisema.
Alieleza kuwa Serikali kwa
kushirikiana na wadhamini wa mpango huo watawahudumia na kuwapatia matibabu sahihi
na kwa wakati muafaka wale wote watakaobainika kuwa na matatizo, hatua hiyo
ikiwa ni kuzingatia sera ya Serikali ya kutowa matibabau bure kwa wananchi bila
ya ubaguzi.
Aidha, alisema mpango huo
unakwenda sambamba na azma ya serikali ya kuhakikisha huduma za afya
zinaendelea na ustawi wa afya ya wanawake unaimarika, kama ilivyohimizwa katika
Ilani ya CCM ya 2015- 2020.
“Tumedhamiria kuongeza kasi
katika kuhakikisha huduma muhimu za afya zinatolewa hapa hapa nchini, ili
kuwapunguzia usumbufu wananchi pamoja na kupunguza gharama za matibabu za
kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi”, alisema.
Dk. Shein aliitaka jamii
kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya ili kufanikisha mpango huo,
akibainisha kuwa una umuhimu wa pekee na utawezesha kujua taarifa halisi za
ukubwa wa maradhi hayo hapa Zanzibar.
“Lakini pia utatuwezesha
kujua mwenenndo na aina ya virusi vya HPV hapa Zanzibar kwani ndivyo
vinavyosababisha kupatikana saratani hiyo kwa asilimia 90’, alisema.
Dk. Shein alieleza kufarijika
na kampeni iliyofanywa na Serikali ya
kuwapatia chanjo dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi watoto wa
kike wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi 14, ambapo uzinduzi wake ulifanyika
April, mwaka huu.
Alisema kampeni hiyo
iliyowashirikisha washirika wa maendeleo kutoka Mashirika ya WHO,UNICEF na mengineyo
Duniani imetowa mwanga katika kunusuru maisha ya wanawake wengi hapa nchini.
“Kwa mantiki hiyo naendelea
kusisitiza bado suala la kinga linahitaji kupewa umuhimu mkubwa mno katika
kukabiliana na maradhi haya, tusisubiri hadi yajitokokeze na kuanza kutuathiri
na ndipo tuanze kuchukua hatua’, alisistiza.
Akigusia ukubwa wa tatizo
hilo, Dk. Shein alisema ugonjwa huo thakili umekuwa ukipoteza roho za watu
wengi hapa nchini na kubainisha kuwa taasisi ya Saratani ya hospitali ya Ocean
Road imeripoti kuwa jumla ya wanawake 35,000 hupata saratani ya shingo ya
kizazi kila mwaka, huku asilimia 20 pekee ndio hufika katika taasisi hiyo kwa
matibabu.
Aidha, alisema takwimu za
maradhi hayo katika Kilinik ya Hospitali ya Mnazimmoja inaonyesha kuwa asilimia
80 ya wanawake wenye aina hiyo ya saratani, hufika hospitali kwa ajili ya
matibabu, wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa huo.
Katika hatua nyengine, Dk.
Shein alikemea vikali tabia ya baadhi ya watendaji katika sekta ya Afya ya
kufanya kazi bila kuzingatia maadili ya kazi zao.
Alisema utekelezaji wa mradi
huo, utaweza kufanikiwa vyema, endapo tu watendaji watatekeleza vizuri dhamira
za kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kiazazi kwa kuzingatia uwezo wa
kiuchumi wa nchi pamoja na mila na desturi za wananchi wa Zanzibar.
Aliwakumbusha madktari,
wauguzi na watendaji wote wa sekta hiyo kuzingatia suala la maadili ya kazi
katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Wizara lazima iwe makini katika
kuhifadhi na kulinda taarifa na siri za wagonjwa ili wananchi wazidi kuzipokea
vizuri juhudi zetu za kutoa kinga ya maradhi mbali mbali, siri ya mgonjwa ni
kati ya mgonjwa mwenyewe na Daktari’, alifafanua.
Akinasibisha kauli yake na
matukio yaliojiri duniani katika siku za hivi karibuni, Dk. Shein alisema,
dharau, sahau, kubabaika na kutozingatia maadili ya kazi kwa daktari au
muuguzi, sio tu kuwa kunaharibu sifa za mtu huyo, bali kwa kiasi kikubwa
kunaathiri sifa za taasisi na baadhi ya nyakati, nchi nzima.
Aidha, Dk. Shein aliwataka Viongozi wa Wizara hiyo
pamoja na Vituo vya Afya kote nchini kuzingatia upya suala zima la matumizi ya simu za mkononi na
nyenzo nyengine za mawasiliano ya kiasa yanayofanyika katika Wodi za Hospitali
pamoja na maeneo yote muhimu yanayohifadhi na kulinda siri na taarifa za
wagonjwa.
“Ipo haja ya kuangalai upya
ni maeneo gani tuyaruhusu, ili wafanyakzi na wagonjwa waingie na simu na nyenzo
nyengine zinazotumika kutoa taarifa, suala la maadili ni pana mno , hivyo
viongozi wa afya mnapaswa mlizingatie katika mpango huu”,alisema.
Vile vile, aliutaka uongozi
wa Wizara hiyo kubuni mipango kabambe itakayowezesha kuendeleza mpango huo
baada ya kipindi cha ufadhili (miaka minne) kumalizika, ili mafanikio
yatakayopatikana yawe endelevu.
Mapema, Balozi mdogo wa
China, Xie Xiaowu alisema China itaendeleza ushirikiano wa muda mrefu uliopo
kati yake na Zanzibar katika sekta ya afya, ambapo kwa nyakati tofauti imekuwa
ikitowa msukumo katika nyanja mbali mbali, ikiwemo afya ya jamii, ujenzi wa miundo
mbinu, uaptikanaji wa vifaa pamoja na wataalamu.
Nae, Waziri wa Afya Zanzibar,
Hamad Rashid Mohamed alisema ujio wa mradi huo utafanikisha azma ya Serikali ya
kuwa an wanawake imara na wenye afya njema.
Alisema wanawake wanakabiliwa
na changamoto mbali mbali za maradhi, ikiwemo saratani ya shingo ya kizazi,
hivyo akawataka akinamama kutumia vyema fursa hiyo, ambapo watachunguzwa na
kupatiwa tiba bila ya malipo yoyote.
Aidha, Naibu Rais kutoka
Naijing Drum Tower Hospital, alisema mradi wa uchunguzi wa shingo ya kizazi, ni
eneo jipya la ushirikiano katika sekta ya afya, kati ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar na Jimbo la Jiangsu nchini China. Alisema katika kukabiliana an
saratani ya shingo ya kizazi, suala la elimu ya kina linalopaswa kupewa umuhimu
pamoja na kufanyika uchunguzi kabla ya tiba.
Nae, Katibu Mkuu wa Wizara
Afya, Asha Abadalla alipongeza uongozi wa kamisheni ya Afya na uzazi wa mpango
kutoka jimbo la Jiangsu nchini China , kwa utayariwao katika utekelezaji wa mpango
huo.
Uchunguzi wa saratani ya
shingo ya Kizazi hufanyika kwa wnaawake wenye umri wa kunzia miaka 21 hadi 65,
ambapo wastani wa wanawake 35,000 wanatarajiwa kuchunguzwa katika kipindi hicho
na kupatiwa matibabu na Serikali.
No comments:
Post a Comment