Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 12 December 2018

Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU)



NA MWANDISHI WETU

WALIOKUWA vigogo watano wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka minne kila mmoja, baada ya kutiwa hatiani kwa makosa mawili likiwemo la kukisababishia chama hicho hasara ya zaidi sh. milioni 109.

Hata hivyo, vigogo hao ambao walitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya ya Tabora, mbele ya Hakimu Mkazi, Tengwa Chiganga na kupewa adhabu hiyo, watatumikia kifungo cha miaka miwili gerezani kutokana na adhabu za kifungo zinakwenda sambamba.

Waliotiwa hatiani na kupewa adhabu hiyo ni  mwenyekiti wa chama hicho, Mkandala Mkandala, Kaimu Meneja Mkuu John Kusanja, Mhasibu Mkuu Prosper Mbacho, Francis Mpeta na Makamu Mwenyekiti Msafiri Ngassa ambao walipelekwa katika gereza la Uyui kuanza kutumikia adhabu ya kifungo jela.

Wakati vigogo hao wakitiwa hatiani na kupewa adhabu hiyo, mahakama hiyo iliwaachia huru washitakiwa wawili katika kesi hiyo Hamza Kapela na mfanyabiashara Faraz Abbas ama Faraz Yaseen Abbasi, kutokana na upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao pasi na kuacha shaka yoyote.

Washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka manne ambayo ni kula njama ya kutenda kosa, kughushi, matumizi mabaya ya madaraka kwa kununua gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 bila kupata kibali kutoka kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini na kukisababishia chama hicho hasara ya sh. 109,010,000 kutokana na kununua gari  hilo.

Akisoma hukumu hiyo mapema wiki hii, Hakimu Chiganga alisema wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo upande wa jamhuri ulileta mashahidi 16 na vielelezo 16.
Alisema upande  wa jamhuri umeweza kudhibitisha mashitaka mawili bila ya kuacha shaka yoyote dhidi ya washitakiwa  Mkandala, Kusanja,  Mbacho,  Mpeta na Ngassa.

Hakimu Chiganga aliyataja makosa hayo kuwa ni  matumizi mabaya ya ofisi kwa kununua gari chakavu lenye thamani kubwa kuliko lililopitishwa na WETCU na kukisababishia chama hicho hasara.

Alisema kutokana na hilo, mahakama inawatia hatiani washitakiwa hao watano. Hata hivyo, alisema upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa Faraz na Kapela hivyo wanaachiwa huru.

Akitoa adhabu, Hakimu Chiganga alisema shitaka la kwanza la matumizi mabaya ya ofisi kila mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela na la pili la kukisababishia chama hicho hasara  kila mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela, adhabu ambazo zitakwenda sambamba.

Baada ya kutolewa kwa adhabu hiyo, upande wa jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wa serikali waandamizi, Shadrack Kimaro, Juma Masanja na Wakili wa Serikali, Tumaini Ocharo walisema hawajaridhika na adhabu hiyo, hivyo waliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufani.

Washitakiwa hao katika kesi hiyo, walikuwa wakiwakilishwa na mawakili Hassan Kilingo na Kanani Chombala. Vigogo hao wa WETCU walikamatwa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuamuru ambapo iligundulika walinunua gari chakavu kwa bei ya gari jipya na kinyume na uamuzi wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao uliamuru kununuliwa gari kwa thamani y ash. milioni 40 na mrajisi wa vyama vya ushirika aliridhia.

Inadaiwa washitakiwa hao walinunua gari hilo kwa mfanyabiashara Faraz ambapo nyaraka za gari zinaonesha ni la mwaka 2008, lakini wao walighushi kadi na kuonesha la mwaka 2014 na likauzwa kwa sh. 269,010,000.

Machi 16, 2017, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimuagiza  Kamanda wa Polisi, Mkoa wa  Tabora kuwakamata viongozi wanne wa Chama Kikuu cha Ushirika wa  Tumbaku (WETCU) na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa tuhumaza ubadhirifu wa fedha za chama hicho utakapokamilika.

Pia, Waziri Mkuu alivunja Bodi ya WETCU na  Bodi ya Tumbaku Tanzania  – TTB kwa sababu ya kushindwa  kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Waziri Mkuu alitoa  maagizo hayo  katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora, ambapo alisema  Rais Dk. John Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa TTB, Vita Kawawa  na Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo  Wilfred Mushi.

Viongozi wa WETCU ambao Waziri Mkuu aliagiza wakamatwe ni Mwenyekiti Mkandala, Makamu Mwenyekiti. Msafiri Kassim, Mkaguzi wa Ndani na Mhasibu  Mkuu. Pia aliwasimamisha kazi watumishi wa kitengo cha uhasibu wa chama hicho hadi uchunguzi utakapokamilika.

“Kuanzia sasa watumishi wote wa kitengo cha uhasibu pamoja menejimenti nimewasimamisha kazi pamoja na Mrajisi wa mkoa wa Tabora Deogratius Rugangila. Kamanda hakikisha ofisi hazifunguliwi kuanzia sasa hadi hapo timu ya ukaguzi  itakapokamilisha kazi yake,” amesisitiza.

Waziri Mkuu alisema kwa muda mrefu wakulima wameteseka na zao hilo kukosa tija kwa sababu ya usimamizi mbovu wa viongozi wa ushirika na Bodi ya Tumbaku Tanzania jambo ambalo Serikali haiwezi kulivumilia.

“Hatuwezi kuwa na ushirika ambao hauwasaidii wanachama. WETCU walipokea sh. bilioni 15 ambazo walizikatia risiti na hazijaonekana. Pia waliwalipa wazabuni sh, bilioni 10 ambazo hawajazikatia risiti,”.

“Wakati wanachama ambao ni wakulima wakiendelea kutesema WETCU walinunua gari la sh. milioni 269 kinyume na na maelekezo ya Mkutano Mkuu wa wadau ambao ulipitisha zitumike shilingi milioni 40 tu,” alisema.

Waziri Mkuu alisema  chama hicho kimesababisha kupungua kwa uzalishaji kwa kiasi kikubwa kutokana nakuwa na menejimemti mbovu jambo ambalo limechangia wakulima wa tumbaku kukosa tija.

Amesema WETCU kimekithiri kwa matumizi mabaya ya fedha ambapo alitolea mfano suala la ukarabati wa ofisi tatu ikiwemo ya makao makuu ambayo ilipangwa ikarabatiwe kwa sh. milioni 33 wakatumia sh. milioni 170 na ofisi za Tabora na Urambo zilipangiwa sh. milioni tano kila moja na hazikukarabatiwa.

No comments:

Post a Comment