BILIONI 83 ZALIPWA KWA WAKULIMA 82,835 WA KOROSHO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 10 December 2018

BILIONI 83 ZALIPWA KWA WAKULIMA 82,835 WA KOROSHO

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wabanguaji wadogo wa korosho kutoka katika mikoa mitano ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Morogoro uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Mtwara leo tarehe 9 Disemba 2018. 

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe Joseph Kakunda (Mb) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wabanguaji wadogo wa korosho kutoka katika mikoa mitano ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Morogoro uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Mtwara leo tarehe 9 Disemba 2018.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo- Mtwara

HADI kufikia jana tarehe 9 Disemba 2018 serikali imefanikiwa kuwalipa jumla ya wakulima 82,835 katika Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Jumla ya fedha iliyolipwa kwa wakulima hao ambao tayari wamefanyiwa uhakiki ni Bilioni 83 ambapo katika mkoa wa Mtwara wakulima 50,835 wamelipwa mkoa wa Lindi wakulima 22,131 na Mkoa wa Ruvuma ni wakulima 9,445.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 9 Disemba 2018 wakati akizungumza kwenye mkutano wa wabanguaji wadogo wa korosho kutoka katika mikoa mitano ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Morogoro uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mjini Mtwara.

Aidha, Mhe Hasunga alisema kuwa jumla ya vyama 328 vimefanyiwa uhakiki kati ya vyama 504 vilivyopo katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma ambapo jumla ya vyama 319 vimekwishalipwa.

Vilevile amewatoa hofu wananchi wanaopotoshwa kuwa bado wakulima hawajalipwa kiasi chochote cha fedha huku akisisitiza kuwa wakulima wanalipwa kupitia njia ya benki hivyo wanapaswa kuwa na utamaduni wa kwenda benki.

Mhe Hasunga alisisitiza kuwa serikali imedhamiria kuwanufaisha wakulima wa korosho ambapo tayari amewaelekeza watendaji wa Bodi ya Korosho Tanzania kuwasajili wakulima wote wa korosho ili watambulike.

Waziri Hasunga alisema kuwa kikao hicho kina lengo la Kujadiliana na kukubaliana utaratibu uliopangwa na serikali katika ubanguaji wa korosho mwaka 2018/2019 kwa kuelekeza ubanguaji kufanyika nchini ili kuwanufaisha wananchi katika ajira hiyo.

“Tumeiona changamoto ya mitaji kwa wabanguaji wadogo nchini sambamba na wabanguaji wakubwa hivyo ili serikali iwarahisishie upatikanaji wa mitaji tumeamua kuwapa kazi ninyi wenyewe,” Alisisitiza.

Aliongeza kuwa swala la uhakiki limejikita zaidi kubaini udanganyifu unaofanywa na baadhi ya wahujumu wa biashara ya korosho “Kuna watu walikuwa wametoa akaunti za benki lakini zinatofautiana na majina ya watu waliwasilisha korosho zao kwenye maghala ya kuhifadhia korosho” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa.

“Tulipoona soko la korosho linayumba huku lengo la serikali likiwa ni kutaka kuonana wakulima wananufaika tuliamua kuingilia kati na kuanza kununua korosho zote na kwa kwenda mbele Zaidi tumeamua kubangua korosho zote hapa hapa nchini.”

No comments:

Post a Comment