Waumini wakishiriki katika hafla hiyo. |
Na Lusungu Helela, Geita
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amesali katika Kanisa la Wasabato la Geita Kati mkoani Geita ambako ameendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha Afya.
Lengo la kuendesha harambee hiyo ni kwa ajili ya kuchangisha pesa zitakazotumika katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kanisa la Wasabato kinachotarajiwa kujengwa katika kata ya Bombambili eneo la Magogo kitakachosaidia kuihudumia jamii.
Katika harambee hiyo Naibu Waziri Mhe. Kanyasu aliambatana na wadau wake ambapo kwa pamoja waliweza kukabidhi Sh15 milioni zikiwa ni fedha taslimu kama mchango wao. Katika harambee hiyo, ahadi mbali mbali zimeweza kutolewa ikiwemo matofali, saruji pamoja na malori ya mchanga na mawe.
Sambamba na hilo, Mhe. Kanyasu ameupongeza uongozi wa kanisa hilo kwa kuwa na mpango huo wa kuisaidia serikali katika kutoa huduma kwa jamii ambayo kimsingi ni kazi ya Serikali,
''Suala la kujenga vituo vya afya ni jukumu la serikali lakini ninyi mmeamua kuisaidia serikali nawapongezeni sana na msisite kunishirikisha kwa lolote,"
Aidha, Mhe. Kanyasu amewataka waumini wa Kanisa hilo kuendelea kujitolea kukamilisha hatua za ujenzi wa kituo hicho cha Afya. Kwa upande wake Mchungaji na Mwenyekiti wa South Nyanza Conference, Sadoki Butoke amesema kituo hicho cha Afya mara baada ya kukamilikwa kwake kitatumika kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na sio kwa ajili ya kupata kitu.
Ameongeza kuwa kituo hicho kitawasaidia kitasaidia kuijenga jamii kiroho na kimwili na ili kukamilika kwake jumla ya sh 150 milioni zinahitajika.
No comments:
Post a Comment