WAZIRI MKUU AAGIZA MRADI WA MAJI CHATO UKAMILIKE KWA WAKATI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 27 November 2018

WAZIRI MKUU AAGIZA MRADI WA MAJI CHATO UKAMILIKE KWA WAKATI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi waliojitokeza kumlaki wakati alipowasili kwenye Kiwanja cha Ndege cha Chato kuanza ziara ya Kazi mkoani Geita, Novemba 27, 2018.  Wapili kushoto ni Waziri wa Nishati na Mbunge wa Chato, Dk. Medard Kalemani, kushoto ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais TAMISEMI,  George Mwita Waitara na Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita,  Mhandisi Robert Gabriel wakati alipowasili kwenye Kiwanja  cha Ndege cha Chato kuanza ziara ya kazi mkoani Geita, Novemba 27, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaameweka jiwe la msingi mradi wa maji wa Imalabupina/Ichwankima wilayani Chato ambao una thamani ya sh. bilioni 8.28 na amewaagiza viongozi wa wilaya hiyo wahakikishe unakamilika kwa wakati.

Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dk. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao ya makazi.
Ameyasema hayo Novemba 27, 2018 alipozungumza na wananchi kwenye kijiji cha Nyamirembe baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi huo wa maji wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Geita.

Amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha wananchi wote nchini wakiwemo na wa wilaya ya Chato mkoani Geita wanapata huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao, hivyo amewataka waendelee kuwa na imaji na Serikali yao.

“Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo mbalimbali nchini vikiwemo na vijiji vya wilaya ya Chato ili kuwawezesha wananchi kupata maji.”

Waziri Mkuu ameagiza mradi huo ukamilike kwa wakati kwa kuwa Serikali inahitaji kuona wananchi wakinufaika na huduma hiyo. Mradi huo ulianza kujengwa Mei, 2017 na ulitakiwa ukamilike Mei, 2018 ila kutokana na changamoto mbalimbali unatarajiwa kukamilika Februari 2019.

Awali, Mkuu wa wilaya ya Chato Mhandisi, Mtemi Simeon alisema mradi huo unatarajiwa kuhudumia watu takribani 59,609 katika vijiji 11 vilivyopo kwenye kata nne za Nyamirembe, Ichwankima, Kachwamba na Kasenga.

“Vijiji vitakavyonufaika na mradi huu ni Nyamirembe, Kalebezo, Nyambiti, Busalala, Imalabupina, Ichwankima, Kachwamba, Ipandikilo, Idoselo, Igagula na Mwangaza. Tayari vituo 240 vya kuchotea maji vimeshakamilika na matenki nane kati ya tisa yamekamilika pamoja na mabirika 10 ya kunyweshea mifugo.”

No comments:

Post a Comment