Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia wakati wa ufunguzi wa maonesho ya kwanza ya viwanda Kibaha. |
Na Khalfan Said
MAKAMU wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameuagiza uongozi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kuendelea kuwafuatilia waajiri ambao bado hawajajisajili ili waweze kufanya hivyo.
Makamu wa Rais alitoa wito huo leo Oktoba 29,
2018 alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye maonesho ya viwanda Mkoa wa Pwani
kwenye viwanja vya CCM-Sabasaba, Picha ya Ndege Mkoani humo.
Alisema viwanda vimeongezeka nchini na kwamba
huduma za WCF zitahitajika sana kwa wakati huu na hivyo kuutaka uongozi wa
Mfuko, kuhakikisha unaendelea na ufuatiliaji kwa waajiri wa zamani na wapya ambao bado hawajajisajili na kuwasilisha michango kwenye Mfuko watekeleze takwa hilo la kisheria ili
mfanyakazi anapoumia aweze kupata haki yake ya fidia.
“Waajiri wao muwabane wajisajili na mfuko na
waweze kuwasilisha michango ili Mfuko uendelee kuwa na uwezo wa kulipa fidia,
pale watoto wetu (wafanyakazi) wanapokatika vidole au kuumia waweze kupata
haki zao.” Alisisitiza.
Katika
hatua ya kuimarisha Hifadhi ya Jamii, Tanzania, Serikali ilianzisha Mfuko wa
Fidia Kwa Wafanyakazi kwa mujibu wa kifungu namba 5 cha sheria ya Fidia kwa
Wafanyakazi, kipengele cha 263 kilichofanyiwa marejeo mwaka
2015 ili kuhakikisha kila mfanyakazi Tanzania Bara kutoka sekta ya umma na
binafsi anapata fursa ya kuwekewa bima na mwajiri wake ili anapopata majeraha
au magonjwa awapo kazini basi aweze kufidiwa kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, WCF imekuwa miongoni
mwa taasisi zilizotunukiwa vyeti vya shukrani kwa kuwezesha maonesho hayo kufanyika.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi unashiriki
maonesho hayo ya kwanza ya viwanda kufanyika Mkoani Pwani ambapo waajiri,
wafanyakazi na wananchi wamekuwa wakipita kwenye banda la Mfuko huo kupata
elimu kuhusu shughuli za Mfuko.
Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akimkabidhi cheti cha shukrani Mkurugezni Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba kutokana na Mfuko huo kuwa miongoni mwa taasisi zilizowezesha kufanyika kwa maonesho ya kwanza ya viwanda Kibaha kwenye viwanja vya Sabasaba-Picha ya Ndege Mkoani Pwani, Oktoba 29, 2018.
Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba, alipotembelea banda la Mfuko huo.
Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akipeana mkono na Mkurugenzi wa Huduma za
Fedha na Uwekezaji, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw.Bezil Ewala, alipotembelea banda la Mfuko huo. Wapili kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Mshomba.
Wananchi wakipatiwa maelezo na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa WCF, Bw. Sebera Fulgence walipofika kwenye banda la Mfuko huo.
Mgeni rasmi katika picha ya pamoja na wawezeshaji wa maonesho hayo.
Kikundi cha ngoma cha JKT
No comments:
Post a Comment