Afisa Programu Utetezi na Ushiwishi kutoka TGNP Mtandao, Deogratius Temba akizungumza. |
Na Mwandishi Wetu
VIONGOZI wa serikali
za Mitaa na Jeshi la Polisi wameshauriwa kushirikiana na wananchi
kuhakikisha vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hasa Ukeketaji vinakomeshwa Jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa
Mjadala wa Bunge la Jamii uliohusiha Viongozi wa Mitaa yote ya Kata ya Kitunda
Manispaa ya Ilala, jijini Dar es salaam, waalimu wa shule za msingi na
sekondari, Jeshi la Polisi na wadau wa mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia,
Afisa Programu Utetezi na Ushiwishi kutoka TGNP Mtandao, Deogratius Temba,
alisema vita dhidi ya Ukeketaji wa wasichana ndani ya Manispaa ya Ilala
itafanikiwa endapo wadau wote watashirikiana.
Wakati wa mjadala huo
ambao ni sehemu ya mradi wa Kupambana na mila potofu zinazosababisha kuendelea
kwa vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto unaofadhiliwa na Foundation for
Civil Society (FCS), wadau kwa pamoja walikubaliana kuuanda kamati za
kutokomeza Ukatili wa Kijinsia ngazi za mitaa kama sehemu ya utekelezaji wa
Mpango kazi wa Taifa wa Miaka Mitano wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na
watoto (NPA) unaotekelezwa kuanzia 2016/17-2021/22.
“Leo tumekubaliana
hapa kuunda kamati za Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia, Taarifa zipo kwetu sisi
wananchi, unapomuona jirani yako anapanga sherehe za kumkeketa
msichana wa shule, toa taarifa kwa kamati au kwa mtendaji wa kata ili hatua
zichukuliwe….”alisema Temba.
Mtendaji wa Kata ya
Kitunda Hamza Juma alisema kwamba, vita dhidi ya Ukatili wa Kijinsia
inawezekana endapo watendaji wa Mitaa, wenyeviti na maafisa
maendeleo ya Jamii Kata watawajibika ipasavyo na kuhakikisha taarifa za Ukatili
zinawafikia polisi kwa wakati ili hatua zichukuliwe.
“ Kuna kazi nzuri
inafanywa na jeshi la Polisi, lakini tunahitaji kuwapa ushurikiano wa kutosha
ili hata wale wanaokeketa wasichana wa shule tutoe taarifa zao mapema na hatua
zitachukuliwe” alisema Juma.
Kwa mujibu wa jamii
zinazofanya ukeketaji, mwaka huu 2018 ni mwaka wa Ukeketaji ambapo kwa Dar es
salaam, kata za Kivule, Kitunda, Kipunguni, mzinga, Msongola, Pugu na Chanika
zinatajwa kuwa na idadi kubwa ya watoto walio hatarini kukeketwa ifikapo
Novemba.
No comments:
Post a Comment