WATANZANIA WAISHIO NJE WATAKIWA KUSHAWISHI WAWEKEZAJI - MAJALIWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday, 3 September 2018

WATANZANIA WAISHIO NJE WATAKIWA KUSHAWISHI WAWEKEZAJI - MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watanzania waishio nchini China Kwenye ubalozi wa Tanzania uliopo Beijing, Septemba 2, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Baadhi ya Watanzania wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao Kwenye ubalozi wa Tanzania uliopo Beijing nchini China, Septemba 2, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na mke wa Balozi wa Tanzania nchini China na Waziri wa Madini, Angela Kairuki wakati alipowasili kwenye ubalozi wa Tanzania uliopo Beijing China kuzungumza na Watanzania, Septemba 2, 2018. Katikati ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akisalimiana na Watanzania waishio nchini China baada ya kuzungumza nao kwenye ubalozi wa Tanzania uliopo Beijing Septemba 2, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewatakaWatanzania waishio nje ya nchi  wahakikishe wanashiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi yao  kwa kushawishi wawekezaji wenye mitaji mikubwa waje kuwekeza nchini na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.



Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Magufuli inaamini kuwa Tanzania itapata maendeleo makubwa ya kiuchumi endapo wananchi wake watatekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya “Hapa Kazi tu”.



Aliyasema hayo Septemba 02 ,2018 wakatiakizungumza na Watanzania waishio nchini China kwenye ofisi za Ubalozi wa Tanzani uliopo jijini Beijing.



Alisema nchi zote zilizoendelea  zilihakikisha kuwa wananchi wake wanaelewa na kutekeleza matamko yanayowahamasisha kufanya kazi, hivyo alitumia fursa hiyo kuwahamasisha Watanzania popote walipo kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu.’



Waziri Mkuu alisema China ambayo imefanikiwa kuwa moja kati ya nchi zenye nguvu  kubwa ya kiuchumi duniani, imefika hapo kutokana na mchango mkubwa uliotolewa na wananchi wake, ambao waliamua kuunga  mkono juhudi za Serikali yao kwa kufanya kazi kwa bidii na weledi wakiwa ndani au nje ya nchi.



Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka Watanzania waishio nje ya nchi wajiepushe na vitendo vya uhalifu hasa biashara ya dawa za kulevya  ambayo inachafua jina na heshima ya nchi yao kimataifa.



“Tanzania ni nchi nzuri na inaheshimika duniani, nawasihi wote mnaoishi nje muachane kabisa na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa sababu inalitia doa Taifa na adhabu yake katika baadhi ya nchi ni kifo,” alisisitiza Waziri Mkuu.



Awali, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga alisema mwelekeo  wa Diplomasia ya Tanzania Kimataifa hivi sasa ni kiuchumi (economic diplomacy), hivyo Watanzania waishio nje wanapaswa kuwa wabunifu, makini katika kutafuta fursa zenye manufaa kwa nchi yao.



Alisema Diplomasia ya Uchimi si kupeleka Tanzania wawekezaji tu bali wawekezaji katika viwanda ambavyo kila vinapojengwa vinachangia kuinua uchumi wa Taifa.



Kwa upande wake,Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki aliwaasa vijana kuitumia teknolojia ya mawasiliano na mitando ya jamii kutafuta habari na taarifa muhimu hasa nafasi za masomo ili kujiendeleza kielimu.

No comments:

Post a Comment