Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba akipata
maelezo ya kitaalamu kutoka kwa Dkt. Linus Munishi mtafiti kutoka Taasisi ya
Nelson Mandela. Taasisi hiyo imetenga eneo maalumu la majaribio ya kuua mimea
vamizi bila kuathiri mazingira, utafiti unao onekana kufanikiwa.
SERIKALI imeazimia kurudisha ikolojia ya hifadhi ya
Ngorongoro katika mazingira yake ya asili na kusisitiza kuwa shughuli zote za
kuharibu na kuchafua ikolojia hiyo
vitadhibitiwa kwa nguvu na uwezo wote.
Akizungumza na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January
Makamba amesema kuwa lengo la ziara yake ni kufuatilia utekelezaji wa maagizo
aliyoyatoa kwa Mamlaka hiyo mwezi Machi 2017.
Katika ziara yake mapema mwaka jana pamoja na mambo
mengine Waziri Makamba aliagiza Mamlaka hiyo kuchukua hatua za haraka na
kuwaelekeza wamiliki wa hoteli na loji hususan zilizoko katika kingo za kreta
katika bonde la Ngorongoro kutafuta vyanzo mbadala vya maji na kuondokana na
kutegemea chanzo cha chemichemi za Lerai.
Aidha, Waziri Makamba aliagiza kuchukuliwa kwa hatua za
haraka ili kudhibiti mimea inayohatarisha uoto wa asili katika Mamlaka ya
Ngorongoro kwa kuunda jopo la wataalamu kutoka Tume ya Sayansi na
Tecknolojia, Baraza la Taifa la Hifadhi
na Usimamizi wa Mazingira, Hifadhi za Taifa za Tanzania, Wizara ya Kilimo na
Mifugo na Mamlaka ya Ngorongoro ili kufanya utafiti wa kina na wakisayansi wa
kubaini mbinu mpya ya kupambana na mimea hiyo vamizi inayotawala mimea
inayotumiwa na wanyama kama malisho.
Akitoa
taarifa ya utekelezaji wa maagizo hayo Kaimu Mhifadhi wa Ngorongoro Dkt. Maurus
Msuha amesema kuwa Mamlaka ya Ngorongoro iliwaandikia barua wamiliki wote wa
hoteli na loji na kufanya tafiti kupitia
kwa wataalamu elekezi wawili tofauti ambao kwa pamoja walishauri kuandaliwa kwa
mkakati wa usimamizi na matumizi ya maji ndani ya Mamlaka ya Ngorongoro utakaokuwa
suluhisho la matatizo la maji bila kuathiri mifumo ya ikolojia katika Hifadhi.
Aidha,
katika kukabiliana na changamoto ya mimea vamizi ndani ya hifadhi, Bw. Msuha
amesema kuwa Mamlaka imeanda ramani ya kuainisha aina, kiasi na maeneo ilipo
mimea vamizi ndani ya hifadhi ili kuweza kuweka mikakati na mbinu sahihi za kukabiliana
nayo ikiwa ni pamoja na kuendelea na kazi ya kutumia njia rafiki ya kimazingira
ya kungo’a, kufyeka na kuchoma njia iliyoonyesha mafanikio makubwa hususan
katika kudhibiti mmea tishio (Darura
stramonium) ndani ya kreta na maeneo mengine.
Bw.
Msuha amefafanua kuwa Ofisi yake inashirikiana na wataalamu wa Taasisi ya Sayansi
na Teknoljia ya Nelson Mandela ya Mkoani Arusha na wameanziasha utafiti
utakaodumu kwa kipindi cha miaka miwili, utafiti wa kuua magugu katika hifadhi
kwa kutumia mifumo ya ki-biolojia. Matokeo ya awali yanaonyesha mafanikio kwa
asilimia 70 katika kupambana na mimea vamizi.
Mara
baada ya kupokea taarifa hiyo, Waziri Makamba amesema kuwa suala la mimea
vamizi ni janga la kitaifa ambalo kwa sasa linawekewa mikakati ya kitaifa ili
kuweza kukabiliana nalo. “Mimea hii vamizi imetapakaa maeneo mengi nchi hivyo
jitihada za pamoja zinahitajika, Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais tumeitisha
Mkutano Mkubwa Arusha tarehe 04/09/2018 utaojumuisha wataalamu na wadau kutoka
taasisi mbalimbali ili kwa pamoja tuzungumze chanzo cha tatizo hili, ukubwa
wake, madhara na hatua za kuchukua” Makamba alisisitiza.
Pia,
Waziri Makamba ametoa muda wa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Ngorongoro kuanza
kutekeleza kwa vitendo Mpango wa usimamizi na matumizi ya maji ndani ya Mamlaka
na kutoa rai kwa wamiliki wa Hoteli na loji hususan zilizoko katika kingo za
kreta katika bonde la Ngorongoro kuanza kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ya
kutibu maji taka ili yaweze kutumika tena na kuwataka kufahamu kwa matumizi ya
maji kutoka ndani ya kreta hitimisho lake linakaribia.
Waziri
Makamba yuko Mkoani Arusha kupitia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa mwaka
jana pamoja na kuzungumza na wadau waliowekeza katika hoteli na kambi za
uwindaji.
No comments:
Post a Comment