TMA YATABIRI MVUA YA MSIMU WA ‘VULI’ OKTOBA HADI DISEMBA, 2018 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 6 September 2018

TMA YATABIRI MVUA YA MSIMU WA ‘VULI’ OKTOBA HADI DISEMBA, 2018

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi (katikati) akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa taarifa za utabiri wa hali ya hewa ya msimu wa mvua za vuli kwa miezi mitatu leo Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja uendeshaji wa vituo  Hellen Msemo na Mkurugenzi wa Utabiri TMA, Dk. Hamza Kaberwa (kulia). 
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akitoa utabiri wa hali ya hewa ya msimu wa mvua za vuli kwa miezi mitatu zaani Oktoba, Novemba na Disemba, 2018 kwa wanahabari leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja uendeshaji wa vituo vza TMA, Hellen Msemo.


Na Joachim Mushi, Dar es Salaam


MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), leo imetoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli unaotarajiwa kuanza mapema katikati ya mwezi Septemba na mwanzoni mwa Oktoba, 2018 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua. Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes L. Kijazi amesema mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa uwezekano mkubwa wa mvua za vuli kuwa za wastani katika maeneo mengi ya nchi.

Alisema kuwa mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya pwani ya kaskazini katika kipindi cha msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba, 2018, huku akisisitiza wadau sekta mbalimbali kujipanga katika kutekeleza ushauri na tahadhari zinazotolewa na TMA kuepuka madhara makubwa endapo itatokea.

"Katika msimu wa mvua za Vuli 2018 kunatarajiwa kuwa na mvua za wastani katika maeneo mengi pamoja na uwezekano mkubwa wa kupata mvua za juu ya wastani hususan katika maeneo ya Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja and Pemba. Ongezeko la mvua linatarajiwa pia katika mwezi Novemba, 2018 kutokana na uwezekano wa kutokea vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi," alisema Dk. Kijazi.

Alisema kwa Ukanda wa Pwani ya Kaskazini; Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2018 huku kukiwa na mvua za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi.

Aliongeza kuwa vipindi vya ongezeko la mvua vinatarajiwa kutokea katika miezi ya Oktoba na Novemba huku mvua za vuli zikitarajiwa kuisha wiki ya tatu ya mwezi Disemba, 2018. Kwa Nyanda za juu Kaskazini Mashariki kwenye Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2018 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.

Aidha akitoa ushauri kwa wadau sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Wanyamapori alisema katika kipindi cha msimu wa mvua hizo kutakuwa na hali ya unyevunyevu wa udongo na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajiwa kuimarika katika maeneo mengi ya ukanda wa nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na pwani yakaskazini.

Hata hivyo alibainisha kuwa upo uwezekano wa mazao yasiyohitaji maji mengi kuathiriwa na hali ya unyevunyevu wa kupitiliza na maji kutuama. Alibainisha kuwa magonjwa ya wanyama na upotevu wa samaki kutokana na uharibifu wa miundombinu ya kufugia samaki vinaweza kujitokeza kutokana na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo hayo. 

"...Upungufu wa unyevunyevu unaweza kujitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Hivyo, wakulima katika maeneo hayo wanashauriwa kupanda mazao yanayotumia muda mfupi kukomaa na yanayostahimili ukame. Malisho na upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori vinatarajiwa kuwa vya kuridhisha katika maeneo mengi yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani na wastani.

"...Hata hivyo upungufu wa maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori, ufugaji samaki, kupungua kwa samaki katika maji ya asili kutokana na kupungua kwa chakula cha samaki unaweza kujitokeza katika maeneo machache ya magharibi mwa Ziwa Viktoria. Teknolojia ya uvunaji maji ya mvua iimarishwe ili kukidhi mahitaji ya maji katika kipindi cha ukavu. Pamoja na ushauri huu watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wanashauriwa kupata ushauri zaidi kutoka kwa wataalam wa sekta husika ikiwemo maafisa ugani," alisisitiza Dk. Kijazi katika taarifa yake.

Pamoja na hayo, alizishauri Mamlaka za miji na wananchi kwa ujumla kuchukua taadhari kwa kuhakikisha mifumo na njia za kupitisha maji zinafanyakazi ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu pamoja na upotevu wa maisha na mali kwa kile uwepo wa vipindi vifupi vya mvua kubwa vinatarajiwa katika msimu huo wa mvua.

Hatua hizo zinashauriwa kuchukuliwa pia katika maeneo yanayotegemewa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani kutokana na kuwa na uwezekano wa vipindi vifupi vya mvua kubwa, Kutokana na uhaba wa maji salama unaotarajiwa kwa shughuli za binadamu ikiwemo usafi hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani, milipuko ya magonjwa inaweza kujitokeza.

Aidha, maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani pia yana uwezekano wa kukumbwa na milipuko ya magonjwa, hivyo sekta ya Afya inashauriwa kuchukua hatua stahiki kama kugawa dawa za kutibu maji ya kunywa, kuzuia na kuharibu mazalia ya mbu, kudumisha usafiwa mazingira pamoja na hatua nyingine stahiki ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza," alisema Mkurugenzi huyo.

No comments:

Post a Comment