MOISE KATUMBI AZUIWA KUINGIA DRC KUGOMBEA URAIS - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 3 August 2018

MOISE KATUMBI AZUIWA KUINGIA DRC KUGOMBEA URAIS

Moise Katumbi

MOISE Katumbi, kiongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, amezuiwa kurudi nchini kugombea urais katika uchaguzi mkuu Desemba mwaka huu. Serikali ya Congo imemzuia Gavana huyo zamani wa jimbo la Katanga anayeishi uhamishoni Afrika kusini kurudi nyumbani.

Katumbi aliomba ruhusa kuingia nchini leo asubuhi kuwahi kuwasilisha makaratasi yake ya uteuzi wa chama kuwa mgombea urais kwa tume ya uchaguzi nchini. Maafisa wa polisi huko Lubumbashi wameweka vizuizi katika bara bara kuu na usalama umeimarishwa ndani na katika maeneo yalio karibu na uwanja wa ndege.

Kuna mipango ya kuzifunga njia za ndege kutua kuizuia ndege ya Katumbi isitue DRC. Waziri wa habari Lambert Mende anasema gavana huyo wa zamani kutoka jimbo lenye utajiri mkubwa wa madini atakamatwa iwapo atajaribu kuingia nchini kwa ndege ya usafiri wa abiria.

Katumbi aliondoka nchini Congo mnamo 2016 baada ya kukosana na rais Joseph Kabila. Baadaye alishtakiwa kwa udanganyifu wa mali na alihukumiwa miaka mitatu gerezani pasi yeye kuwepo mahakamani.

Kiongozi mwingine wa upinzani - Jean-Pierre Bemba - alirudi DRC siku ya Jumatano baada ya kutokuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja. Aliwasilisha makaratasi yake ya kugombea urais hapo jana Alhamisi.

" Ninaweza kuthibitisha kuwa nilikuwa na kadi ya kupiga kura, na nimewasilisha nyaraka zote," shirika la habari AFP linamnukuu Bemba akizungumza nje ya makao makuu ya tume ya uchaguzi.
-BBC

No comments:

Post a Comment