NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imezindua
akaunti maalum ya kidijitali iitwayo 'NMB Niwekee,' inayolenga kuleta ukombozi
wa maisha ya baadaye ya watu walio nje ya mfumo rasmi wa ajira, ambayo
inajumuisha faida kedekede ikiwemo Bima ya Maisha yenye fidia hadi ya Sh.
Milioni 50.
NMB Niwekee ambayo ni
fursa na wepesi wa kuniwekea kifuta jasho cha baadaye, ni akaunti maalum kwa
wajasiriamali wadogo na WA kati, watoa huduma wa Sekta ya Usafirishaji kwa
Pikipiki 'bodaboda,' mama na baba lishe, pamoja na hata waajiriwa wanaopenda kujiongezea
vyanzo vya akiba ya uzee iliyo nje ya mifumo rasmi.
Uzinduzi wa NMB
Jiwekee uliowakutanisha pamoja 'Chama la Watunza Pesa,' umefanyika jijini Dar
es Salaam Jumatatu Mei 13, ikizinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Deogratius Ndejembi, mwenyeji wa hafla
akiwa Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi.
Akizingumza katika
uzinduzi huo uliofanyika kwa mfumo wa kipindi cha runinga kilichoongozwa na
Mtangazaji Millard Ayo, Waziri Ndejembi alisema ya kwamba, NMB Jiwekee
inayoambatana na faida lukuki kwa wajasiriamali na kada zingine, ni mwendelezo
wa juhudi za wazi za taasisi hiyo kuunga mkono jitihada za Serikali kuyawezesha
makundi maalum ya kijamii.
"NMB Jiwekee ni
huduma chanya na rafiki kwa watu walio katika mifumo ya ajira isiyo rasmi na
wale wenye ajira rasmi wanaotaka kuongeza vyanzo vya akiba kwa ajili ya maisha
yao ya baadaye, ambayo Serikali tunaamini kwamba imekuja kwa wakati sahihi.
"Serikali kila
uchao inapambana kuimarisha mahusiano na taasisi za fedha (mabenki) katika
kusaidia kutanua WiGo wa Watanzania waliounganishwa kwenye Huduma Jumuishi za
Kifedha, na kwa jambo hili taasisi zingine zinapaswa kufuata nyayo za NMB kwa
kuanzisha huduma Bora na rahisi, nafuu na salama kama hizi.
"NMB ijikite
katika kutoa elimu kwa Watanzania juu ya umuhimu wa huduma hii mpya, lakini pia
taasisi zingine ambazo najua zitafuata nyayo hizi za vinara wa huduma za fedha
nchini, nazo zitoe elimu ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia mifumo ya
kitaasisi katika utunzaji wa akiba.
"Serikali haiwezi
'ku-cover' kila kitu ndio maana tunasisitiza nguvu za wadau hususani taasisi za
fedha katika kuwaunganisha Watanzania na Huduma Jumuishi za Fedha.
"Zaidi
niwapongeze NMB kwa kuwapa uhuru watumiaji wa NMB Jiwekee wa kuchagua asilimia
za kujitunzia kutokana na matumizi ya fedha zilizo kwenye akaunti zao,"
alisema Waziri Ndejembi.
Akizungumzia jitihada
za Serikali katika kupunguza umaskini kwa wananchi, Waziri Ndejembi alisema
kipaumbele cha awali kilikuwa ni kurasmisha makundi na sekta zisizo rasmi, ili
kuwawezesha wahusika kutambulika, kukopesheka na kuwa sehemu wa wachangiaji wa
Pato la Taifa.
"Mfano wa juhudi
hizo ni ile Programu ya Kujenga Kesho Iliyo Bora kwa Vijana na Wanawake (BBT),
ambako tuna BBT Kilimo, BBT Ufugaji na Uvuvi, zote hizo ni jitihada za
kupunguza umaskini kwa Watanzania, pamoja na ule Mpango wa 'Four Four Two'
unaojumuisha asilimia nne ya fedha za mikopo kwa akina mama, asilimia nne kwa
vijana na asilimia mbili kwa wenye ulemavu," alisema Waziri Ndejembi.
Kwa upande wake,
Filbert Mponzi, akijibu maswali ya Millard Ayo aliyetangazwa kuwa Msemaji wa
'Chama la Watunza Pesa,' alisema NMB Jiwekee ni zao la tafakuri za kina
zilizofanywa na benki hiyo katika kufanya mapinduzi ya ukombozi wa maisha ya
watu wasio na ajira rasmi.
"NMB Jiwekee ni
zao la maswali juu ya watu walio nje ya mfumo rasmi wa ajira na wale ambao
hawajaajiriwa kabisa, juu ya utunzaji akiba zao kwa maisha ya baadaye, tunajua
ipo mifumo rasmi ya akiba kwa waajiriwa kama Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF).
"Tukajiridhisha
kuwa NSSF ni kwa waajiriwa, inakuwaje kwa watu wasio na ajira ama wale ambao
hawana ajira rasmi, ndipo likaja wazo lililozaa NMB Jiwekee ambayo ni kwa kila
mmoja miongoni mwa wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo, bodaboda, mama na baba
lishe na makundi mengine kwenye Sekta zisizo rasmi.
"Uwekaji akiba
hutokana na pato la mfunguaji wa NMB Jiwekee linalopitia katika benki yetu, ama
waweza kuweka kwa kupitia miamala ya simu za mkononi kutunza pesa kidijitali na
kunufaika na faida nyingi zilizomo, ikiwemo akiba ya baadaye, riba ya asilimia
tano ya akiba kwa mwaka na bima ya maisha.
"Bima hii itakuwa
na fidia mara mbili ya akiba yako uliyojiwekea katika NMB Jiwekee, ama hadi
shilingi Milioni 50 ya fidia upatapo ulemavu wa kudumu utakaokufanya ushindwe
kuendelea kujiwekea akiba. Kianzio kwa njia ya akaunti kinaanzia asilimia moja
hadi 100 ya pesa zako zinazopitia NMB," alibainisha Mponzi mbele ya
waalikwa waliohudhuria uzinduzi huo.
No comments:
Post a Comment