Wazazi wahimizwa kushirikiana na walimu kumjengea mtoto maadili...! - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday 7 May 2024

Wazazi wahimizwa kushirikiana na walimu kumjengea mtoto maadili...!

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadhimisho Juma la Elimu, Bw. Greyson Mgoi wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa elimu katika Kata ya Mgusu Halmashauri ya Mji wa Geita, ikiwa ni sehemu ya ziara za wadau wa elimu katika kuadhimisha Juma la Elimu kwa Mwaka 2024.

Ofisa Uchunguzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, Bi. Abigail Majige akizungumza na wazazi na wanafunzi katika mikutano ya majadiliano, ikiwa ni sehemu ya ziara za wadau wa elimu katika kuadhimisha Juma la Elimu kwa Mwaka 2024.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadhimisho Juma la Elimu, Bw. Greyson Mgoi  ambaye pia ni Meneja Mawasiliano wa Shirika la Uwezo Tanzania akizungumza na wanafunzi, ikiwa ni sehemu ya ziara za wadau wa elimu katika kuadhimisha Juma la Elimu kwa Mwaka 2024.

Kaimu Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala (mbele) akiteta jambo na wanafunzi kwenye Maadhimisho ya Juma la Elimu, nchini kwa mwaka 2024.

WAZAZI wamehimizwa kujenga ushirikiano mzuri kati yao na walimu ili kuweza kuwasaidia watoto wajifunze na kuwajenga katika maadili mema.  

Rai hiyo imetolewa Mei 7, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadhimisho Juma la Elimu, Bw. Greyson Mgoi wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa elimu katika Kata ya Mgusu Halmashauri ya Mji wa Geita ikiwa ni sehemu ya ziara za wadau wa elimu katika kuadhimisha Juma la Elimu kwa Mwaka 2024. 

Bw. Mgoi amesema ili mtoto aweze kupata elimu bora na kumjenga vyema katika masuala ya stadi za maisha na maadili kuna kila haja ya wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto anuai zinazowakabili watoto. 

Akisisitiza juu ya suala hilo, alisema ni vizuri wazazi wakajenga utaratibu mzuri wa kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya watoto wao akiwa shuleni kwa kuwasiliana na walimu mara kwa mara na pia kuhudhuria vikao vyote vya shule ili kuweza kupata nafasi ya kujadili na kupanga mipango muhimu ya shule. 

Pamoja na mambo mengine, Bw. Mgoi amewataka wazazi kuacha kuwachukia walimu pale wanapotoa adhabu ndogondogo kwa watoto shuleni kwa kuwajenga kinidhamu, kwa kuwa mbali ya jukumu la walimu kutoa elimu kwa watoto wana jukumu pia la kuwalea vyema. 

Aidha, amewaomba wazazi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika suala la uchangiaji wa chakula cha watoto shuleni, ili kuwawezesha watoto kupata elimu yao pasipo na changamoto ya njaa. Sambamba na hilo, Mgoi ambaye pia ni Meneja Mawasiliano wa Shirika la Uwezo Tanzania amewaasa wanafunzi kuzingatia elimu kwa kuwa ndio msingi wa maisha yao ya badae. 

Naye, Ofisa Uchunguzi kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, Bi. Abigail Majige akizungumza na wazazi na wanafunzi katika mkutano huo alisema wazazi wanapaswa kuwa mfano bora wa kuwajenga watoto katika maadili mema. 

Majige alisema, kama mzazi akiwa mlevi mtoto naye atajengeka akijua maisha ndivyo yanatakiwa kuwa, vivyo hivyo na kama mzazi atakuwa na tabia nyingine mbaya, watoto nao watajengeka kwa namna hiyo hiyo. Hivyo kuwahimiza wazazi kuhakikisha wanadumisha maadili mema katika familia na jamii zao kwa mifano ili kuwasaidia watoto kujengeka katika maadili. 

Maadhimisho ya Juma la Elimu kwa Mwaka 2024 yamezinduliwa rasmi Mei 6 katika Halmashauri ya Mji wa Geita, mkoani Geita na Naibu Katibu Mkuu Elimu Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk. Charles Msonde ambapo kilele cha maadhimisho hayo ni Ijumaa ya Mei 10 Mwaka 2024.

No comments:

Post a Comment