Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Hawa Mchafu akisikiliza kwa makini maelezo
kutoka Mhandisi wa TTCL mkoa wa Ruvuma Abrahamu Msangi kuhusu mtambo wa
mawasiliano ya mnara huo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati hiyo (hawapo
pichani) ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye kijiji cha Mbatamila
kilichopo wilayani Tunduru kwenye mkoani huo.
KAMATI ya Bunge ya Miundombinu imelipongeza Shirika la
Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa kujenga mazingira rafiki ya uwepo wa choo na
kibanda cha mlinzi kwenye minara ya simu iliyojengwa na Shirika hilo maeneo
mbali mbali nchini kote.
Hayo yameelezwa na
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Hawa Mchafu wakati wa
ziara ya Kamati hiyo ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano kwenye kijiji cha
Mbatamila kilichopo kwenye kata ya Nampungu wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Mhe. Mchafu amesema kuwa
tumeshuhudia kuwa Shirika letu la kizalendo la TTCL pekee ndilo ambalo
limejenga miundombinu rafiki ya choo na kibanda kwenye minara yao yote
waliyojenga kwenye maeneo mbali mbali nchi nzima kwa ajili ya mlinzi anayelinda
minara ya mawasiliano tofauti na kampuni nyingine za mawasiliano ambapo zote
kwa pamoja zimepatiwa ruzuku na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
(UCSAF) ya kujenga minara hiyo kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara.
“Hongereni mmepata
mawasiliano ya mnara wa TTCL ambapo wamejenga miundombinu rafiki ya choo na
kibanda cha mlinzi cha kupumzikia hivyo mnara utalindwa muda wote, kutakuwa
hamna maambukizi ya magonjwa kwa kukosa choo”, amesema Mhe. Mchafu. Ameipongeza
TTCL kwa kuwa wamejenga mnara ambao unatoa mawasiliano muda wote kwa kuwa kuna
nishati ya jenereta kubwa ya kisasa.
Naye Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameipongeza TTCL kwa kujenga
minara ya mawasiliano yenye mazingira rafiki kwenye minara yao yote iliyopo
maeneo mbali mbali nchi nzima.
Nditiye ameongeza kuwa
Tunduru ni Wilaya pekee ambapo TTCL ina jumla ya minara 14 na kupitia UCSAF
itaongeza minara mingine mitatu kwenye vijiji ambavyo vina mawasiliano hafifu
kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanawasiliana.
Ameongeza kuwa Serikali inajenga meli na reli ya kisasa hivyo wahakikishe kuwa
muda wote wananchi wanawasiliana wakiwa safarini.
Pia, ameiagiza Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhakikisha kuwa kampuni za simu
zinatoa huduma ya mawasiliano kwa wananchi ya kupiga simu, vifurushi na ujumbe
kuendana na gharama ya vocha iliyowekwa ambapo ni tofauti na TTCL ambao hawana
ujaja ujanja wa kuwaibia wananchi.
Akithibitisha kuhusu
upatikanaji wa mawasiliano mbele ya Kamati hiyo, mwananchi wa kijiji cha
Mabatamila kilichopo kwenye kata ya Nampungu iliyopo wilayani Tunduru mkoani
Ruvuma Bwana Kassim Zuberi amesema kuwa wanaipongeza TTCL kwa kutoa mawasiliano
kwa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na kampuni nyingine za mawasiliano.
“Tunaiomba TTCL watufungulie huduma za 4G ili tuweze kupata mawasiliano ya
intaneti”, amesema Zuberi.
Mwendeshaji wa UCSAF
Mhandisi Albert Richard amesema kuwa UCSAF imetoa shilingi milioni 460 kwa TTCL
ili iweze kujenga mnara huo ambapo wananchi wanapata mawasiliano. Pia,
ameongeza kuwa tayari UCSAF kupitia ruzuku inayotoa tayari minara 14 imejengwa
kwenye Wilaya hiyo na kwenye zabuni ijayo itaongeza minara mitatu ili wananchi
waweze kuwasiliana muda wote.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma Mhe. Christina Mndeme akizungumza na wajumbe wa Kamati hiyo walipofika
ofisini kwake wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano mkoani
humo, Mhe. Mndeme ameishukuru Serikali kwa kujenga minara 14 kwenye Wilaya ya
Tunduru.
Amesema kuwa mawasiliano
ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa kuwa wanapokea watalii wengi ambao
wanachangia pato la taifa. “Niwaombe watoa huduma watoe huduma ya intaneti kwa
kuwa ni kikwazo kwa wawekezaji mkoani kwetu ambapo wanataka wapate mawasiliano
wakati wote,”amesema Mndeme. Ameongeza kuwa mawasiliano yatasaidia miamala ya
kifedha ambapo inakuwa rahisi kwa wananchi kuwasiliana.
Pia, amefafanua kuwa
watoa huduma za mawasiliano wanaojenga minara waangalie jiografia ya mkoa wa
Ruvuma kwa kuwa una milima, misitu ni mingi sana, hifadhi, mabonde, ziwa Nyasa
na iko mpakani mwa nchi ambapo maeneo hayo yanakuwa na changamoto za
mawasiliano na baadhi ya maeneo ya Chiwindi na Chimati wananchi hawapati
mawasiliano. Amesema kuwa mawasiliano yanahitajika wakati wote hasa maeneo ya
mipakani kwa kuwa mawasiliano ni muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa
wananchi na taifa kwa ujumla
Mjumbe wa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu Mhandisi Ramo Makani na Mbunge wa jimbo la Tunduru
Kaskazini akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mbatimila
(wanaomsikiliza) kilichopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wakati wa ziara ya
Wajumbe wa Kamati hiyo (hawapo pichani) ya kukagua upatikanaji wa mawasiliano
kwenye mkoa huo.
No comments:
Post a Comment