TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA ANGOLA, ETHIOPIA NA COMORO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday, 15 February 2026

TANZANIA KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI NA ANGOLA, ETHIOPIA NA COMORO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride la heshima wakati akiondoka Kiwanja che Ndege cha Kimataifa cha Bole, Addis Ababa, nchini Ethiopia kurejea nchini Tanzania, leo tarehe 15 Februari, 2026. Rais Dkt. Samia alikuwemo nchini humo kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku nne, ambapo pamoja na mambo mengine alishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika tarehe 14 na 15 Februari, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiagana na Viongozi mbalimbali katika Kiwanja che Ndege cha Kimataifa cha Bole, Addis Ababa, nchini Ethiopia kurejea nchini Tanzania, leo tarehe 15 Februari, 2026. Rais Dkt. Samia alikuwemo nchini humo kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku nne, ambapo pamoja na mambo mengine alishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika tarehe 14 na 15 Februari, 2026.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Maendeleo ya Miji na Miundombinu wa Ethiopia Mheshimiwa Chaltu Sani Ibrahim katika Kiwanja che Ndege cha Kimataifa cha Bole, Addis Ababa, mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi nchini Ethiopia ambapo pamoja na mambo mengine alishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika tarehe 14 na 15 Februari, 2026.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuimarisha diplomasia ya kimkakati kupitia mazungumzo ya pande mbili aliyoyafanya na viongozi wa nchi mbalimbali, kando ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), jijini Addis Ababa, Ethiopia. Tarehe 13 Februari, 2026, Rais Dkt. Samia alifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Lourenço, yaliyojikita katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda kati ya Tanzania na Angola. 

Katika mazungumzo yao, Rais Lourenço wa Angola alikubali kufanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania, pamoja na kukubali kuwa Mgeni Rasmi katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba mwaka 2026, hatua inayotarajiwa kufungua sura mpya ya ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili. 

Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano ya kihistoria na ushirikiano wa kimkakati kwa manufaa ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili, hususan katika sekta za nishati, madini, viwanda na miundombinu. Vilevile, tarehe 14 Februari, 2026, Rais Dkt. Samia alikutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia, Mheshimiwa Dkt. Abiy Ahmed Ali, kabla ya ufunguzi rasmi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Afrika, ambapo walijadili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kukuza biashara na uwekezaji, pamoja na ushirikiano katika sekta za usafiri wa anga na usimamizi wa rasilimali za maji. 

Viongozi hao pia walibadilishana uzoefu kuhusu mwelekeo wa uchumi wa nchi zao, ambapo Ethiopia inalenga kukuza uchumi kwa asilimia 10.2, huku Tanzania ikitarajia 2/2 kufikia ukuaji wa asilimia 6.5, kama sehemu ya jitihada za kuimarisha ustawi wa wananchi wa nchi zote mbili. 

Halikadhalika, tarehe 15 Februari, 2026, Rais Dkt. Samia alifanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Comoro, Mheshimiwa Azali Assoumani na kujadili kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kikanda, hususan katika sekta za biashara, utalii, usafirishaji wa baharini na masuala ya usalama. 

Rais Assoumani alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa ushirikiano wa pamoja na mchango wa Tanzania nchini kwake, hususan katika kuimarisha huduma za afya, biashara na masuala ya usalama, akishukuru mchango wa Tanzania katika huduma za kibingwa za matibabu kwa wananchi wa Comoro. 

Kupitia mazungumzo hayo, Rais Assoumani pia alionesha nia ya kufanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania. Rais Dkt. Samia aliridhia ombi hilo. Rais Dkt. Samia ameendelea nafasi ya Tanzania katika jukwaa la Afrika na kimataifa kama sehemu ya kuimarisha diplomasia ya kiuchumi ili kufikia malengo ya Dira 2050. Bakari S. Machumu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu

No comments:

Post a Comment