SERIKALI YATOA MIKOPO KIASI CHA SHILINGI MILIONI 600 KWA WANANCHI WA IFAKARA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Wednesday, 28 January 2026

SERIKALI YATOA MIKOPO KIASI CHA SHILINGI MILIONI 600 KWA WANANCHI WA IFAKARA




SERIKALI imeendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia Makundi mbalimbali wakiwemo wajasiriamali/wafanyabiashara ndogondogo ili kukuza mitaji na biashara zao.

Katika kutekeleza azma hiyo ya Serikali Halmashauri ya Mji Ifakara Januari 27,2026 imetoa mikopo ya asilimia 10 yenye thamani ya Shilingi milioni 600 ikiwa ni Mikopo ya Asilimia 10 inayotokana na Mapato ya ndani kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Stendi ya mabasi kibaoni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa maendeleo pamoja na wanufaika wa mikopo hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felista Mdemu, ameipongeza Halmashauri kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba.

Mdemu amevitaka vikundi vilivyonufaika kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa, kuzingatia masharti ya mikataba, pamoja na kurejesha mikopo kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi wengine kunufaika.

Kati ya kiasi hicho cha Shilingi milioni 600, jumla ya Shilingi 404,787,300 tayari imekwishatolewa kwa vikundi 41, vikiwemo vikundi 20 vya wanawake, 17 vya vijana na 4 vya watu wenye ulemavu ambapo fedha hizo tayari zimeingizwa kwenye akaunti za vikundi husika. Aidha, kiasi cha Shilingi 195,212,700 kitatolewa kwa vikundi 17 vilivyosalia mara baada ya kukamilisha maboresho yaliyoelekezwa.

Katika mgawanyo wa mikopo kwa wanawake, jumla ya vikundi 7 vya wajane vyenye wanufaika 60 vimepatiwa mikopo yenye thamani ya Shilingi 42,975,000, sambamba na vikundi viwili vya wanawake wanaoishi na VVU vyenye wanufaika 31 vilivyopatiwa Shilingi 18,269,000.

Kwa mujibu wa aina za shughuli, mikopo hiyo imegawanywa kwa Vikundi vya usafirishaji ambapo vikundi 18 vyenye thamani ya Shilingi 239,400,000,Vikundi vya kilimo ni vikundi 13 vyenye thamani ya Shilingi 82,693,650 Vikundi vya ufugaji jumla ni vikundi 10 vyenye thamani ya Shilingi 82,693,650.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bi.Pilly Kitwana amewasihi wananchi wa Halmashauri ya Mji Ifakara kuendelea kuunda Vikundi kwani pesa bado zipo ambazo zitasaidia kuwainua pia ameahidi kuendelea kufanya tathimini na ufuatiliaji kwa vikundi vilivyonufaika ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta tija na kuchangia maendeleo ya kiuchumi kwa wanufaika na jamii kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment