Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
SERIKALI la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), zimeitangaza Tanzania kuwa nchi ya pili, baada ya Madagascar, kunufaika na Mfumo wa Ushirikiano wa Kuimarisha Hali ya Hewa kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari mbaya za uharibifu wa mazingira.
Kupitia Mfumo huo, IMF na WBG watafanya kazi kwa karibu na washirika wengine wa maendeleo, kuratibu juhudi zao za kuunga mkono ajenda ya mageuzi ya sera ya Tanzania ili kukabiliana na vihatarishi na changamoto zinazohusiana na mabadiliko hayo ya tabianchi na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wa Tanzania.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa, Bw. Charalambos Tsangarides, alisema kuwa kupitia mpango huo, IMF itaunga mkono kuanzishwa kwa kanuni za uwekezaji wa umma zinazohimili mabadiliko ya tabianchi na utoaji taarifa, huku Benki ya Dunia itajikita katika kusaidia kutekeleza miradi katika sekta zitakazoimarisha uwezo wa Tanzania kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile nishati, maji, hifadhi ya jamii na kilimo.
Taasisi hizo mbili pia zitasaidia uboreshaji na utekelezaji wa sera ya Tanzania ya usimamizi wa hatari za maafa, ikiwa ni pamoja na kufadhili mfumo wa kukabiliana na hatari hizo na uimarishaji wa mtandao wa usalama wa kijamii ili kukabiliana na majanga ya hali ya hewa.
IMF na Benki ya Dunia pia zitasaidia sera za kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji, kupanua upangaji na usimamizi wa matumizi bora ya ardhi ya vijiji, kusimamia vihatarishi vya hali ya hewa katika uchumi na fedha na kutoa msaada wa kiufundi na kifedha kwa kuishirikisha pia sekta binafsi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete, akizungumza kwa njia ya mtandao kutoka Washington D.C, nchini Marekani, alisema kuwa Tanzania itanufaika na msaada wa kiufundi na kifedha kutoka taasisi hizo mbili katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu itakayokuza uzalishaji, kuhifadhi mazingira na kuwa na mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amezishukuru Taasisi hizo kubwa za Fedha Duniani (IMF na Benki ya Dunia) kwa kuiteua Tanzania kuwa nchi za mwanzo duniani, zitakazo nufaika na mpango huo kwa kuunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ni kinara wa mapambano ya kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi.
No comments:
Post a Comment