Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ameishukuru United Bank of Africa (UBA), kwa kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dkt. Nchemba, ametoa shukrani hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa United Bank of Africa (UBA), Bw. Gbenga Makinde, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa Serikali inatekeleza miradi mingi ya kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake na kuialika Benki hiyo kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo reli na umeme.
Kwa upande wake, Bw. Makinde, ameeleza kuwa Benki yake imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika kutekeleza baadhi ya miradi yake ya kimkakati ikiwemo Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere, kwa kuwawezesha kifedha wakandarasi wanaojenga mradi huo na kwamba hivi sasa Benki hiyo iko tayari kushirikiana moja kwa moja na Serikali kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi husika.
UBA ni Taasisi ya fedha ambayo iko nchini kwa miaka 15 na ina matawi zaidi ya 20 katika nchi za Afrika, na baadhi ya nchi za ulaya na Marekani.
No comments:
Post a Comment