SIKU MAPALALA ALIVYOWAKWEPA MAKACHERO WA MREMA MNAZI MMOJA... - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 20 September 2024

SIKU MAPALALA ALIVYOWAKWEPA MAKACHERO WA MREMA MNAZI MMOJA...

 


Bongo Hapo Zamani:

Siku Mapalala Alivyowakwepa  Makachero Wa Mrema Mnazi Mmoja...

...Na Kisa  Cha Mrema Na Balozi Wa Kimagharibi Pale Manzese...!

Ama, Wahenga walinena;

Ndugu wakigombana, chukua jembe ukalime.  Wakipatana, chukua kapu ukavune. 

Kimsingi, na tunaojitahidi kufuatilia historia ya nchi yetu hii, tunajua, kuwa wengi wa wanasiasa wanatoka CCM kwenda upinzani kutokana na misuguano kwenye nafasi za kiuongozi.  

Na kuna wengine wanakwenda kuzitafuta nafasi za uongozi kupitia upinzani kutokana na CCM kuonekana ' kujaa'.  

Kundi hili la pili kimsingi lingeweza kutumikia chama chochote kile, ili mradi malengo yao ya Ubunge na mengineyo yatimie. Dhana ya mitazamo ya kiitikadi mara nyingi huwekwa kando. Na huo ndio ukweli.

Tunahitaji viongozi wa ukweli wa upinzani na waliojikita katika misimamo ya kiitikadi na wakaweza kujipambanua. 

Nchi hii imepata kuwa nao, ni watu wa aina ya James  Mapalala, Kassanga Tumbo , Christopher Mtikila na wengine kadhaa.

Ni watu ambao kweli tuliwaona kwa kauli na matendo, kuwa walikuwa ni wapinzani na walikuwa tayari wasote magerezani kupigania walichokiamini. James Mapalala ni moja ya mifano mizuri sana.

Nakumbuka mwaka 1990, Augustino Mrema akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alihangaika sana na James  Mapalala. 

Pale Mnazi Mmoja ilipangwa siku ya maandamano ya upinzani mwaka ule wa 1990. Ni chini ya akina Mapalala, Mabere Marando na wenzao wengine.

Nilikuwepo Mnazi Mmoja nikiwa kijana mdogo sana mwenye shauku ya habari na kujifunza. 

Nakumbuka siku ile kabla waandamanaji hawajafika Mnazi Mmoja walikutana na FFU na farasi wao waliokwishatangulia Mnazi Mmoja. 

Ikawa ni kufukuzana. Ikatangazwa baadae siku hiyo, kuwa baadhi ya waandamanaji wamekamatwa, na viongozi wao pia. 

Katika waliokamatwa hakuwamo kiongozi wao mkuu, James Mapalala. Mrema akatangaza  msako wa Mapalala mjini, akamatwe popote atakapoonekana. Lilikuwa agizo la Mrema kwa Polisi na makachero wake.

Media ya Tanzania mpaka nilipoandika jambo hili kwa mara ya kwanza miaka ya karibuni, kimsingi ilibaki gizani. Media yetu ilidhani kuwa siku hiyo Mapalala alijificha kwenye moja ya ofisi za balozi za Kimagharibi hapa nchini.

Hapana, nikaja kujua baadae, kuwa siku ile James  Mapalala aliyekuwa akisakwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema, aliweza kwa mbinu zake mwenyewe, kuwakwepa makachero wa 

Mrema na kwenda moja kwa moja Oysterbay. Alikwenda Oysterbay nyumbani kwa Balozi mmoja wa nchi ya Kimagharibi ambaye walikuwa na urafiki pia. 

Huko Mapalala alikaa akinywa kahawa na kuongea na rafiki yake Balozi huku akifuatilia yanayoendelea mjini. Hayo nilielezwa na balozi huyo mwaka 1994, balozi niliyepata bahati ya kuwa na urafiki nae. Kwa sasa ni mstaafu.

Na Mrema naye yalimkuta yepi?

Jioni moja mwaka 1996, rafiki yangu huyo, Balozi wa nchi ya Kimagharibi, kwa sababu za kidiplomasia, simtaji jina wala nchi anayotoka, alifika nyumbani nilikokuwa nikiishi, Kinondoni Biafra. 

Alikuwa yeye na dereva wake tu. Tulipokaa kuongea akanieleza kuwa ametokea ofisi za NCCR- Mageuzi, Manzese. 

Balozi huyo alikuwa ameshamaliza muda wake hapa nchini. Huko kwao kwenye Idara ya Mambo ya Nje, alikuwa Mkuu wa Idara ya Afrika. Alipita tu Dar es Salaam kikazi akitokea Rwanda.

Akiwa Dar, alipanga ahadi ya kufanya mazungumzo na Augustine Mrema katika kusudio la yeye Balozi kuwafahamu viongozi wa upinzani na kuwasikiliza. 

Akaniambia, kuwa walikubaliana na Mrema , kuwa ili kuepusha mgongano wa kidiplomasia na Serikali ya Tanzania, ziara ile ya Balozi isifanywe kuwa rasmi na kutangazwa kwenye vyombo vya habari.  Mrema kwenye mazungumzo ya Manzese alikuwa na wajumbe kadhaa wa chama chake.

Balozi yule katika kunisimulia kule nikamuuliza swali moja tu;

" Je, mazungumzo yenu yaliishaje?"

Rafiki yangu Balozi akaniambia walimaliza kwa kupiga picha ya pamoja ambayo Mrema aliitaka sana ipigwe. 

Balozi akarudia tena kuomba kuwa picha hiyo isitumike kwenye media. Mheshimiwa Balozi akaniambia, kuwa alihakikishiwa kuwa hilo lisingetokea.

Nikamwambia;

“ Nachelea kusema, kuwa makubaliano yako na Mrema yalivunjika mara tu mliposhikana mikono ya kuagana!”

Rafiki yangu Balozi yule akanishangaa sana nilipomwambia,  kuwa asishangae picha hiyo ikawa kwenye kurasa za mbele kwenye moja ya magazeti siku inayofuata.

Siku ya pili yake, gazeti la Majira likachapisha picha  ukurasa wa mbele ikimwonyesha Mheshimiwa Balozi akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa NCCR- Mageuzi. Ni kwenye ofisi za chama hicho Manzese na huku Augustino Mrema akiwa amejaa katikati ya picha kulia kwa Mheshimiwa Balozi wa Nchi Muhimu ya Kimagharibi!

Niliikata picha hiyo na kumtumia Balozi yule, naye abaki na kumbukumbu ya tukio la Manzese, Tanzania!

Maggid Mjengwa.

No comments:

Post a Comment