KAMPENI YA POLISI KUNUSURU WANAFUNZI SHULENI, VYUONI YAJA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 22 August 2024

KAMPENI YA POLISI KUNUSURU WANAFUNZI SHULENI, VYUONI YAJA

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Leah Mbunda (katikati) akifungua mafunzo na kutoa mada kwa askari wa Dawati la Jinsia na Watoto katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Ilala, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Glory Urassa akifuatilia.


Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Leah Mbunda (kushoto mbele) akiwasilisha mada kwa askari wa Dawati la Jinsia na Watoto mara baada ya kufungua mafunzo leo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Ilala, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Glory Urassa (kulia) akiwasilisha mada kwa askari wa Dawati la Jinsia na Watoto leo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Leah Mbunda akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mafunzo yaliotolewa kwa askari wa Dawati la Jinsia na Watoto leo jijini Dar es Salaam.

Mratibu wa Mafunzo hayo, Dk Christina Onyango akifafanua jambo kwenye mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa kwa mafunzo.

MWANDISHI WETU

JESHI la Polisi limeanza kampeni ya ‘Tuwaambie Kabla Hawajaharibiwa’ inayolenga kuwanusuru wanafunzi wapya wa kidato cha kwanza, cha tano na mwaka wa kwanza katika vyuo vya kati na vyuo vikuu nchini dhidi vitendo vya jinai wanavyoweza kutenda au kutendewa kutokana na ugeni katika mazingira mapya ya elimu.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Leah Mbunda amebainisha hayo wakati akifungua mafunzo na kutoa mada kwa askari wa Dawati la Jinsia na Watoto katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala yaliyofanyika Dar es Salaam.

Kwa nyakati tofauti ACP Leah, Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Ilala, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Glory Urassa na Mratibu wa Mafunzo hayo, Dk Christina Onyango wamesema mafunzo hayo  yanalenga kuwajengea uelewa na uwezo wa kubaini viashiria vya ukatili wa kijinsia na makosa mengine wawapo katika mazingira mapya ya kidato cha kwanza, tano au mwaka wa kwanza vyuoni.

Lengo lingine la kampeni hiyo ni kutahadharisha wanafunzi na wanachuo wapya dhidi ya tabia potofu wanazokutana nazo waingiapo shuleni na vyuoni.

ACP Leam amesema kutokana na ugeni wao katika mazingira, wengi wanajikuta wakiangukia katika jinai ama kwa wao kutenda, au kutendewa mfano kutapeliwa.

“Wengine kutokana na tamaaa, wanajikuta katika unyanyaswaji hasa wa wa kingono na hawa ni vijana wa kike na wa kiume maana mtu anataka pesa, lakini hana njia ya kupata hizo pesa, anaamua kuingia katika uhalifu au kujiweka katika hatari ya kufanyiwa ukatili na udhalilishaji wa kijinsia…” amesema.

Amesema katika utekelezaji wa kampeni hiyo, askari na maofisa hao wanapaswa kuelimisha umma kushirikiana kutoa malezi mema kwa watoo tangu wawapo nyumbani, shuleni hadi vyuo vikuu.

Kuhusu usalama na malezi ya wa watoto, ACP Leah anasema: “Inasikitisha kuona wanawake wengi Dar es Salaam hawako makini na watoto hata wakati wanavuka barabara… Yaani utaona mzazi au mlezi anamwacha nyuma mtoto huku anamshushia matusi au kumfuata na kumzaba kibao… Isitoshe, wanawaacha sana watoto kuzurura hovyo mitaani…” 

Kwa upande wake, ASP Glory amesema anawataka askari kuzingatia kuwa, katika suala la maadili, ni lazima wazingatie weledi, miongozo na sheria za nchi ili kuihumidia vyema jamii.

“Tuwe na tamaa ya kuisadia jamii kwa kukomesha ukatili wa kijinsia…,” amesema.

Naye Dk Onyango anasema mafunzo hayo yanalenga kuwafanya askari na maofisa hao wa polisi kuwa na uelewa sahihi, wa pamoja na wa kutosha katika kampeni hiyo kuhusu ukatili wa kijinsia ukiwamo wa rushwa ya ngono.

Dk Christina ametaka vijana waelimishwe kutojinyanyasa wala kujifanyia ukatili wa kingono kwa kujipiga ‘picha chafu’ na kuziweka mitandaoni kwa hali hiyo huwasababishia madhara na majuto baadaye.

“Tumebaini shuleni watoto wengine wanajichua bila kujua kuwa, wanajiathiri kimwili na kisaikolojia maana wengine wanatarajiwa kuwa baba wa familia…” alisema.

 Kuhusu madhara ya rushwa ngono, amesema ipo katika baadhi ya taasisi za elimu, dini, siasa na kazini ama kutoka kwa wanawake, au wanaume.

“Si wanaume pekee, bali hata wanawake, baadhi wanajihusisha na uchafu wa kudai rushwa ya ngono jambo ambalo ni hatari kijamii, kiafya, kimwili na kiakili,” amesema.

Amesema chanzo cha rushwa hiyo ni tamaa, matumizi mabaya ya madaraka, kutojiamini kwa baadhi ya watu, kutowajibika kazini, shuleni na vyuoni pamoja na baadhi ya wafanyakazi na wanafunzi kutokujua haki zao.

Kwa mujibu wa Dk Onyango baadhi ya viongozi katika baadhi ya taasisi za dini wakiwawamo bmitume na manabii wanajihusisha na rushwa ya ngono wakiihusisha na imani za kishirikina

Katika mafunzo hayo ya siku moja, washiriki wameonesha kukerwa na tabia ya baadhi ya wanawake mkoani Dar es Salaam kucheza ngoma maarufu ‘kigodolo’ kwa hali ya ‘nusu uchi’ hali inayokiuka maadili ya jamii na kuwafanya washiriki kujidhalilisha kijinsia.


Baadhi ya askari wa Dawati la Jinsia na Watoto katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala wakiwa kwenye mafunzo hayo leo jijini Dar es Salaam.


No comments:

Post a Comment