Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshulikia masuala ya Utawala na Fedha Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi, yaliyofanyika jijini Dodoma. |
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi akelezea jambo kwenye ramani ya Mji wa Serikali Mtumba walipotembelea kiwanja cha Ubalozi wa Oman, jijini Dodoma. |
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato Chumi amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman anayeshughulikia Utawala na Fedha Mhe. Khalid Hashil Al Muslahi Ofisini kwake jijini Dodoma.
Katika mazungumzo yao Mhe. Chumi amemhakikishia Mhe. Al Muslahi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na Oman katika kukuza uhusiano wa kihistoria uliopo kwa manufaa na maslahi ya pamoja kati ya nchi hizo na watu wake.
Mhe. Chumi pia ameishukuru Serikali ya Oman kwa uamuzi wa kuiunga mkono Serikali ya Tanzania kwa kuamua kujenga Ubalozi na Kituo cha Utamaduni jijini Dodoma ambapo waliongozana na Naibu Waziri Chumi na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule kutembelea viwanja hivyo, ambavyo Tanzania iliipatia serikali ya Oman kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya ubalozi na makazi vilivyopo katika mji wa Serikali Mtumba, na mradi wa kihistoria wa ujenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Oman jijini Dodoma.
Mhe. Chumi amemhakikishia Mhe. Al Muslahi kuwa Tanzania itashiriki Kongamano la Uwekezaji na Biashara la Oman litakalofanyika tarehe 26 hadi 28 Septemba 2024 Muscat, Oman ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji na Oman. Ameongeza kuwa Ujumbe wa Tanzania utaongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Sharriff Ali Shariff.
Tanzania na Oman zinashirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji na utalii ambapo Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Oman mwaka huu unatimiza miaka 54 tangu kuanzishwa kwake na kuufanya uhusiano huo wa muda mrefu wa karibu na kirafiki kuendelea kuimarika zaidi.
Aidha, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaonyesha kuwa mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda nchini Oman yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 14.6 mwaka 2022 hadi kufikia Dola milioni 16.4 mwaka 2023 na uagizaji wa bidhaa kutoka Oman umepungua kutoka Dola za Kimarekani milioni 207.9 mwaka 2022 hadi Dola milioni 100.1 mwaka 2023.
No comments:
Post a Comment