WIZARA, TAASISI ZA UMMA WEKENI PROGRAM ZA MAZOEZI YA WATUMISHI – BALOZI DKT. KUSILUKA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Saturday, 10 August 2024

WIZARA, TAASISI ZA UMMA WEKENI PROGRAM ZA MAZOEZI YA WATUMISHI – BALOZI DKT. KUSILUKA

 






Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KATIBU Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka amezitaka Wizara na Taasisi za Umma kuhakikisha wanatenga bajeti na kuweka programu ya michezo katika maeneo yao ya kazi kwani michezo ni muhimu kama shughuli zingine zozote.

Balozi Dkt. Kusiluka ametoa rai hiyo leo Agosti 10, 2024 jijini Dodoma, katika bonanza la uzinduzi wa michuanio ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania  (SHIMIWI), ,ambapo amesema siku moja haitoshi kwa michezo hivyo ni vema kila Idara iandae programu za mazoezi na michezo na ataanza kuzifuatilia kuanzia sasa.

"Mimi mwenyewe nafanya mazoezi na ofisini pale tuna eneo maalumu la kufanyia mazoezi hivyo nizitake Wizara na Idara za Serikali kuwa na Programu za mazoezi, mtambue kila mtu kulingana na umri wake anapaswa kufanya mazoezi tena unapokuwa na umri mkubwa unahitaji mazoezi zaidi, yapo mazoezi ya watu wenye afya na hata wagonjwa wanamazoezi yao, ukiangalia sasa kuna michezo ya Olimpiki inayoendelea kuna mchezo wa kutembea, hivyo hata kutembea ni mazoezi" amesema Balozi Dkt.  Kusiluka

Pia amewataka viongozi wote kuanzia Makatibu Wakuu kuhakikisha wanampatia taarifa ya namna gani  wameandaa  bajeti kwa ajili ya michezo  na michuano mbalimbali kwa kuwa kutokuwa na bajeti kisiwe kikwazo kwa watumishi kutoshiriki katika michezo mbalimbali. 

Pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa kuhakikisha wananchi na watumishi wa umma wanahamasishwa kushiriki michezo kwani sio kila michezo inahitaji bajeti kubwa nyingine ni hamasa pekee. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMIWI, Daniel Mwalusamba amesema kuwa mashindano ya SHIMIWI kwa mwaka 2024 yatafanyika mkoani Morogoro kuanzia Septemba 18 hadi Oktoba 5 hivyo kawaomba waajiri kuwaruhusu mapema watumishi wao ambao ni wanamichezo, ili kushiriki michezo hiyo ili ianze kwa kwa wakati bila kuathiri ratiba za mechi zitakazokuwa tayari zimepangwa kwenye ratiba. 


"Kumbukumbu tulizonazo baadhi ya timu zimekuwa zikichelewa sana kufika katika kituo cha mashindano hali inayopelekea kuvurugika kwa ratiba hivyo tuwaombe waajiri kuwaruhusu mapema wanamichezo kuja kushiriki mashindano ya SHIMIWI kwa wakati ili kuepukana na kupanguapangua ratiba mara kwa mara," amesisitiza Mwalusamba

Amesema lengo Kuu la  mashindano ya SHIMIWI ni kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwa na afya njema, ili waweze kutoa mchango wa ujenzi endelevu wa taifa hivyo michezo ni eneo salama la kutunza afya za Watumishi, kwa ajili ya maendeleo ya taifa endelevu. 

Naye Katibu Mkuu  Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ina kampeni ya kupinga magonjwa yasiyoambukiza kupitia michezo na kampeni hiyo itasaidia Watanzania wote waanze kufanya mazoezi. 

"Kwa sasa kila mahali kuna Jogging ni kuonesha kuwa watanzania wanaunga mkono michezo na kupinga magonjwa yasiyoambukiza kupitia michezo na kutakuwepo na afua mbalimbali za kuhakikisha kampeni hii inafanikiwa kwani tayari tumeshafanya mazungumzo na Wizara ya Mambo ya Ndani maana wenzetu wana vikosi vya   Polisi  nchi nzima na Wizara ya Ulinzi nao wana Vikosi nchi nzima hivyo wenzetu  watatusaidia kuhamasisha mazoezi sio kwa Wafanyakazi tu ila hata kwa wanachi, " amesema Msigwa

No comments:

Post a Comment