Na Mwandishi Wetu, Mwanza
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)
imetaka watendaji wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura
Mkoani Mwanza na Shinyanga kuhakikisha wanatunza vifaa vya uandikishaji ili
vikaweze kutumika maeneo mengine nchini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele wakati
akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa
Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa
Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe
10 hadi 11 Agosti, 2024 Mkoani Mkoani Mwanza.
Mafunzo kama hayo pia yamefunguliwa
Mkoani Shinyanga na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa(Mstaafu) Mbarouk
Salim Mbarouk leo mkoani humo.
“Kwa kusisitiza, ni muhimu
kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa
vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama
kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji
nchini,” alisema Jaji Mwambegele.
Amesema kutokuwa makini katika
utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi
hili muhimu na amewataka kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili
muweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza.
Aidha, Jaji Mwambegele amesema
matokeo bora ya zoezi hili yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya
watendaji wote wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa
uchaguzi.
“Ninawasihi muwe na ushirikiano
mzuri na wa karibu na Tume wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na
ikiwa mnahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, msisite kuwasiliana na Tume,”
alisema Jaji Mwambegele
Mapema kabla ya kuanza mafunzo
hayo, washiriki walikua kiapo cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri
mbele ya Hakimu Mkazi wa Mwandamizi wa Wilaya Ilemela, Christian Mwalimu.
Mafunzo hayo yanahusisha namna ya
ujazaji wa fomu pamoja na kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters
Registration System - VRS) ili waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa
ya kutumia kwa ufasaha mfumo huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga
kura.
“Mafunzo haya, yanawajengea umahiri
wa kuwafundisha Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa
mafunzo hayo kwa Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi
ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” alisema Jaji
Mwambegele.
Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa
mafunzo maalum ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi
(Troubleshooting) endapo zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga
kura vituoni.
Katika hatua nyingine, Jaji
Mwambegele amewaambia watendaji hao kuwa wakati wa uboreshaji wa Daftari
mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha
wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia
mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza
kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.
Jaji Mwambegele alitoa angalizo kwa
mawakala hao kutoka vyama vya siasa kuwa hawaruhusiwi kuwaingilia
watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
Tume tayari imeanza zoezi la
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo mzunguko wa kwanza
ulianza kwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora kuanzia Julai 20 hadi 26,2024 na
mzunguko wa pili unaendelea katika mikoa ya Kagera na Geita ambao ulianza
Agosti 5 hadi 11 mwaka huu, na kauli mbiu ya uboreshaji ni “Kujiandikisha
Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi Wa Uchaguzi Bora”
za majukumu jao.
No comments:
Post a Comment