DKT. MSONDE APOKELEWA WIZARA YA UJENZI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 19 August 2024

DKT. MSONDE APOKELEWA WIZARA YA UJENZI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde akisaini kitabu mara baada ya kuwasili kwenye Wizara hiyo, katika Ofisi za Wizara ya Ujenzi zilizoko Mtumba tarehe 19 Agosti, 2024 Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde akizungumza na watumishi mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za Wizara ya Ujenzi tarehe 19 Agosti, 2024 Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Ujenzi mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za Wizara ya Ujenzi tarehe 19 Agosti, 2024 Jijini Dodoma.

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde leo Agosti 19, 2024 amewasili na kupokelewa katika Ofisi za Wizara ya Ujenzi zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, mkoani Dodoma na kutoa wito kwa Menejimenti na Watumishi wa Wizara kushirikiana kwa pamoja ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu na kuwahudumia Wananchi kupitia Sekta ya Ujenzi.

Akisalimiana na Menejimenti na Watumishi, Dkt. Msonde amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumleta Wizara ya Ujenzi kuungana na timu ya Wizara ili kwa pamoja kushirikiana kufungua uchumi kupitia miundombinu ya barabara na madaraja.

Aidha, Dkt. Msonde ameupongeza Uongozi, Watumishi na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kwa kazi kubwa na yenye weledi wanayoendelea kuifanya katika kuwahudumia wananchi hasa katika kipindi cha athari za mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya ambapo walirejesha mawasiliano ya miundombinu ya barabara na madaraja kwa muda mfupi.

“Binafsi niwapongeze Viongozi na Watumishi kwa utendaji mzuri, tukikumbuka katika kipindi cha mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya baadhi ya miundombinu ilikatika kabisa na hali ilikuwa ni tete lakini mlisimama usiku na mchana kufungua mawasiliano na shughuli za kiuchumi zikaendelea”, amesema Dkt. Msonde.

Awali, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Richard Mkumbo kwa niaba ya Menejimenti na Watumishi amemuahidi Dkt. Msonde kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu na adhma ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwahudumia wananchi kupitia Sekta ya Ujenzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano - IKULU, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alimuhamisha Dkt. Msonde kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI na kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi.


No comments:

Post a Comment