NAIBU KATIBU MKUU OFISI YA MAKAMU WA RAIS BI. CHRISTINA MNDEME ATETA NA NAIBU BALOZI WA INDIA NCHINI TANZANIA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday 21 June 2024

NAIBU KATIBU MKUU OFISI YA MAKAMU WA RAIS BI. CHRISTINA MNDEME ATETA NA NAIBU BALOZI WA INDIA NCHINI TANZANIA

Naibu Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Manoj Verma (katikati) akizungumza jambo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Bi. Christina Mndeme muda mfupi mara baada ya kumaliza mazungumzo baina yao yaliyofanyika katika Mji wa Serikali wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma Juni 20, 2024.

Naibu Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Manoj Verma akiagana na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Deogratius Paul mara baada ya kumaliza mazungumzo baina yake na Viongozi wa Ofisi hiyo yaliyofanyika katika Mji wa Serikali wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma Juni 20, 2024. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bi. Christina Mndeme.

Naibu Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Manoj Verma (kushoto) akiagana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Christina Mndeme muda mfupi baada ya kumaliza mazungumzo baina yao yaliyofanyika katika Mji wa Serikali wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma Juni 20, 2024.

SERIKALI ya India imeahidi kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha lengo la utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 linafikiwa, hatua itakayosaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira. 

Hayo yamebainika wakati wa kikao kati ya Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme na Naibu Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Manoj Verma kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Juni 20, 2024. 

Katika mazungumzo hayo, Bi. Mndeme ameishukuru Serikali ya India kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa huduma za maendeleo ya kijamiii na kiuchumi kwa wananchi. 

Mndeme ameeleza kuwa ajenda ya nishati safi ya kupikia ni moja ya kipaumbele cha kimkakati cha Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara katika kuhamasisha jamii na juhudi zake zinashuhudiwa na Watanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla. 

“Mhe. Rais Dkt. Samia amekuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ametumia ushawishi wake katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa kwa kutafuta fursa ili kubadilisha mfumo uliopo katika jamii yetu kwa kuacha kutumia nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia kama gesi” amesema Mndeme. 

Aidha Mndeme amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha suala la uhifadhi na usimamizi wa mazingira linaendelea kupewa kipaumbele katika mikutano na majukwaa mbalimbali ya ngazi za maamuzi. 

Mndeme pia ameishukuru Serikali ya India kwa kuendelea kutoa fursa ya mafunzo yanayolenga katika kuwajengea uwezo kwa wataalamu kada mbalimbali ikiwemo sekta ya mazingira. 

Kwa upande wake, Balozi Mhe. Verma amepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha jamii yake inahamia katika mfumo wa matumizi ya nishati safi ya kupikia hatua inayolenga kuepukana na matumizi ya nishati chafu ambayo imekuwa na madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira. 

“India imepiga hatua kubwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo takribani asilimia 80 ya wananchi wa mijini na vijijini wanatumia nishati hiyo…..Tupo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha ajenda hii inafikiwa kwa wananchi wake” amesema Mhe. Verma.

 Aidha Mhe. Verma ameeleza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni moja ya ajenda inayoendelea kupewa kipaumbele katika mikutano na majukwaa mbalimbali ya kikanda, kitaifa na kimataifa kutokana na umuhimu kugusa maslahi ya wananchi wengi hususani waliopo katika mataifa yanayoendelea. 

Mhe. Verma amefafanua kuwa umuhimu huo unatokana na ukweli kuwa Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na moja ya juhudi hizo ni kuhamasisha jamii kuachana na shughuli za ukataji wa kuni na mkaa kwa matumizi ya nishati ya kupikia. 

Ameongeza kuwa katika kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, tarehe 5 Juni mwaka huu Serikali ya India imezindua Kampeni ya Upandaji Miti ijulikanayo “A tree for Mother” inayohamasisha dunia umuhimu wa kupanda miti kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira na rasilimali za viumbe hai mbalimbali. 

Hivyo, Balozi Verma ameiomba Serikali ya Tanzania kuunga mkono kampeni hiyo, ambapo katika kipindi cha mwaka mmoja, Serikali ya India imekusudia kupanda miti bilioni 1 ikiwa ni mkakati wa kuhamasisha jamii kulinda mazingira na uhifadhi wa baianoai mbalimbali na hivyo kufikia malengo ya maendeleo endelevu. 

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Deogratius Paul na watalaamu mbalimbali


No comments:

Post a Comment