Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa
akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo, wakati wakikagua barabara
ya Lindi – Dar es Salam ambayo Mawasiliano yake yamekatika kutokana na mvua |
Muonekano wa sehemu ya
barabara ya Lindi - Dar es Salama, eneo la Somanga ambalo limekatika kutokana
na Mvua zinazoendelea kunyesha Mkoani Lindi.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na wananchi na wasafiri wa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na Dar es Salaam, wanaotumia barabara ya Lindi – Dar es Salam ambayo Mawasiliano yake yamekatika kutokana na mvua El-Nino zinazoendelea kunyesha Mkoani Lindi.
Waziri wa Ujenzi,
Innocent Bashungwa, ameeleza kuwa timu ya watalaamu wa Wakala ya Barabara
(TANROADS) na Makandarasi itatumia saa 72 (siku 3) kukamilisha zoezi la
kurejesha miundombinu ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam, ambayo imeharibiwa
na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zilizombatana na kimbunga Hidaya.
Amesema hayo Mkoani
Lindi Mei 05, 2024, mara baada ya kuwasili na kukagua uharibifu wa miundombinu
ya barabara ya Lindi - Dar es Salaam na kuzungumza na wananchi na wasafiri wa
Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na Dar es Salaam wanaotumia barabara hiyo na
kutoa pole na kuwataka kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea na jitihada
za kujereshwa miundombinu.
“Mitambo ipo inaletwa
hapa, kazi ya kurudisha mawasiliano ya barabara hii itaanza wakati wowote
kuanzia sasa, ni lazima tuanze na kipande kimoja ili tuweze kufika katika
maeneo mengine yaliyoathiriwa. Namna miundombinu imeharibika na tathmini
iliyofanyika tunahitaji masaa yasiyopungua 72 ili kuweza kurudisha
mawasiliano,” amefafanua Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa
mawasiliano ya barabara hiyo yamekatika katika maeneo matano ambayo ni pamoja
na eneo la barabara ya Somanga – Mtama, eneo la Mikereng’ende kutokea Somanga
na eneo la Lingaula kutokea Lindi.
Aidha, Bashungwa
amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itafanya kila jitihada ili ifikapo
Jumatano jioni mawasiliano ya barabara hiyo yarejee katika hali yake.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya
Kilwa, Mohamed Nyundo ameeleza kuwa maji yaliyokuwa yakipita juu ya barabara
yalizidi kiwango na kusababisha madaraja kushindwa kuhimili wingi na kasi ya
maji na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo matano ikiwemo
Somanga, Mikereng’ende, na Lingaula.
Nyundo amemueleza
Waziri Bashungwa kuwa kazi ya awali iliyofanyika ni kuwasiliana na taasisi
zinazohusika kwa Mkoa wa Ruvuma, Mtwara na Lindi ili kutoa taarifa kwa
wasafirishaji na watumiaji wa barabara hiyo kusimamia safari zao mpaka pale
miundombinu itakaporejeshwa katika hali yake.
No comments:
Post a Comment