UJUMBE WA KAIMU MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA), MWAKILISHI WA KUDUMU WA TANZANIA KATIKA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO), NA MAKAMU MWENYEKITI WA JOPO LA KIMATAIFA LA SAYANSI YA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI (IPCC), DKT. LADISLAUS BENEDICT CHANG’A KATIKA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 24 March 2024

UJUMBE WA KAIMU MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA), MWAKILISHI WA KUDUMU WA TANZANIA KATIKA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO), NA MAKAMU MWENYEKITI WA JOPO LA KIMATAIFA LA SAYANSI YA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI (IPCC), DKT. LADISLAUS BENEDICT CHANG’A KATIKA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI,

Dkt. Ladislaus Benedict Chang’a.

 UJUMBE WA KAIMU MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA), MWAKILISHI WA KUDUMU WA TANZANIA KATIKA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO), NA MAKAMU MWENYEKITI WA JOPO LA KIMATAIFA LA SAYANSI YA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI (IPCC), DKT. LADISLAUS BENEDICT CHANG’A KATIKA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI, TAREHE 23 MACHI, 2024

Leo ni Siku ya Hali ya Hewa Duniani. Jumuiya ya Hali ya Hewa Duniani huadhimisha Siku ya Hali ya Hewa kila ifikapo tarehe 23 Machi tangu kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na kuanza kutumika kwa Mkataba ulioanzisha WMO mnamo tarehe 23 Machi 1950.

Maadhimisho haya huonesha mchango na umuhimu wa Taasisi za Kitaifa zinazotoa huduma za hali ya hewa kwa usalama na ustawi wa jamii. Tanzania ikiwa ni miongoni mwa Nchi 193 wanachama wa WMO inaungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani na kuonesha dhamira yake ya kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2024 ni “Kuwa Mstari wa Mbele Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi”. Kaulimbiu hii ilichaguliwa kwa kuzingatia lengo la 13 la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goal 13-Climate Action) ambalo linaitaka jamii kuchukua hatua za haraka kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Mpaka sasa, mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yameathiri kila nchi katika kila bara na pia tunatambua kuwa ripoti za Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) zinaangazia kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la joto ambalo halijawahi kushuhudiwa sambamba na kuongezeka zaidi kwa matukio ya hali mbaya ya hewa na athari zake. Athari hizi zinazidi kuongezeka na kusababisha changamoto mbalimbali katika uchumi wa taifa na kuathiri maisha ya kila siku na hata ya baadae. Aidha, kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi chafuzi kunakotokana na shughuli za viwanda kumesababisha wastani wa joto duniani kupanda zaidi ya nyuzi joto moja (1°C) ikilinganishwa na viwango vya mwaka 1850 - 1900. Kwa upande mwingine, mwaka 2023 ulivunja rekodi kwa kuwa mwaka wenye joto zaidi katika historia ya dunia ukichagizwa na ongezeko la gesijoto na uwepo wa hali ya El Niño. Wastani wa ongezeko la joto kidunia kwa mwaka 2023 ulkuwa nyuzi joto 1.4 °C ikilinganisha na kipindi cha kabla ya mapinduzi ya viwanda. Kwa upande wa Tanzania ongezeko la joto kwa mwaka 2023 lilifikia nyuzi joto 1.0 0C. Ongezeko hili kubwa likiambatana na matukio ya hali mbaya ya hewa, ikiwemo mvua kubwa, mafuriko na upepo mkali vimechangia kuleta maafa ikiwemo vifo na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu. 

Kwa muktadha huo, WMO na Wanachama wake wanaweka vipaombele vya kuimarisha huduma za hali ya hewa sanjali na kuelimisha jamii kuhusu matumizi stahiki ya huduma na taarifa za hali ya hewa. 

Huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini Tanzania zimeendelea kuwa bora zaidi katika historia ya nchi yetu kabla na baada ya uhuru. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanya uwekezaji mkubwa katika ununuzi na uboreshaji wa miundombinu ya uangazi  sambamba na wafanyakazi kujengewa uwezo. Maboresho hayo ni pamoja na ufungaji wa vifaa vya kisasa vya kuhakiki utendaji kazi wa vifaa vya hali ya hewa (Calibration Laboratory Equipments), rada za hali ya hewa, vifaa vya utambuzi wa matukio ya radi (Lightning detector) na kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data za hali ya hewa (Computer cluster). Uwekezaji huu umeongeza kwa kiasi kikubwa ubora na usahihi wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa na tahadhari za mapema hadi kufikia wastani kati ya asilimia 80 hadi 98 juu ya asilimia 70 inayokubalika kimataifa. Hii inazifanya huduma za TMA nchini kuwa za uhakika na kuchangia kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi sambamba na kuokoa maisha na mali kutokana na matukio ya hali mbaya ya hewa.

TMA inaendelea kuwa mstari wa mbele kutoa mchango katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwa kutfanya tafiti na kuhamasisha matumizi ya sayansi na uvumbuzi miongoni mwa wataalamu wake na wataalamu wengine katika vyuo vikuu na taasisi za utafiti nchini na barani Afrika. Wataalamu wa TMA wameendelea kubuni mifumo mbalimbali ya kuongeza ufanisi na kuimarisha uchakataji wa data na utoaji wa huduma za hali ya hewa. Mifumo hiyo ni pamoja na; TMA Digital Meteorological Observatory (DMO) ambao hutumika katika kuimarisha mawasiliano ya data za hali ya hewa kutoka vituoni kote nchini; mfumo wa utoaji wa taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa bahari na maziwa (Meteorological Marine MMAIS) na mfumo wa “Meteorological Aviation Information System (MAIS)” ambao hutumika katika mawasiliano na sekta ya usafiri wa anga. Mifumo hii imekuwa na manufaa na kuleta tija kubwa katika mawasiliano ya taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wa huduma za hali ya hewa ikiwemo sekta ya anga na baharini. Huduma za hali ya hewa kwa ajili ya sekta ya usafiri wa anga nchini zimethibitishwa na zinatumbuliwa kukidhi vigezo na viwango vya kimataifa kwa mujibu wa Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) kwa cheti cha ISO 9001:2015 tangu mwaka 2017 na kabla ya hapo ISO 9001:2008.

Katika hatua ya kuimarisha utoaji na matumizi ya huduma za hali ya hewa na kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, Serikali ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019.  Pamoja na utoaji wa huduma za hali ya hewa, Sheria inaiagiza TMA kusimamia na kuratibu huduma za hali ya hewa nchini. Hii inajumuisha usajili na ukaguzi wa vituo vyote vya hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusimamia data zote za uangazi wa hali ya hewa. Ni kosa kisheria kuwa na kituo cha hali ya hewa ambacho hakijasajiliwa. Lengo ni kuendelea kuimarisha upatikanaji wa takwimu za uangazi zenye ubora ili kusaidia uboreshaji wa huduma za hali ya hewa pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na pia kuongeza kiasi cha data kupitia Mfumo wa Mawasiliano wa data na taarifa za hali ya hewa Kimataifa wa WMO (Global Telecommunication System) na ule wa WMO Information System (WIS). 

Ili kuwa na idadi kubwa ya wataalam wabobevu na wenye uwezo katika taaluma ya utabiri wa hali ya hewa pamoja na uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ni muhimu pia kuendelea kuwajengea uwezo wataalam waliopo na wanaochipukia wa hali ya hewa na wale wa mazingira. Hivyo, TMA inamiliki na kuendesha Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (National Meteorological Training Centre, NMTC) kilichopo mkoani Kigoma (www.nmtc.ac.tz). NMTC inatoa mafunzo ya hali ya hewa kwa ngazi ya cheti (NTA Level 4) na astashahada (NTA Level 5 na 6). Jukumu la NMTC ni kukuza uwezo wa wataalamu katika nyanja ya sayansi ya hali ya hewa ndani na nje ya Tanzania. Miongoni mwa moduli zinazofundishwa ni uangazi na utabiri wa hali ya hewa, matumizi ya satellite na rada za hali ya hewa katika utabiri wa hali ya hewa (remote sensing, radar meteorology), mabadiliko ya tabianchi na sayansi nyingine zinazohusiana ikiwa ni pamoja na uratibu na usimamizi wa mazingira. Aidha, Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa (NMTC) kimesajiliwa kwa nambari REG/EOS/025 mnamo Machi 2014 na kuthibitishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE). Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wa kuimarisha miundombinu ya huduma za hali ya hewa na kuendelea kuijengea uwezo TMA kitaasisi na kiufundi na kuifanya Tanzania kuwa mojawapo ya nchi ya mfano katika ubora wa huduma za hali ya hewa katika Afrika na katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani.

Huduma zinazotolewa na TMA ni pamoja na utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku tano, siku 10, mwezi, msimu na tahadhari za mara kwa mara za hali mbaya ya hewa pamoja na mwelekeo wa mvua za msimu katika maeneo madogo hadi ngazi ya Wilaya. TMA pia inatoa taarifa za hali ya hewa ikiwemo taarifa ya kila mwaka ya hali ya hewa ya Tanzania (Statement on the Status of Tanzania Climate) tangu mwaka 2011. Taarifa za hali ya hewa zinapatikana kwa urahisi kwenye tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz) ilhali taarifa nyingine mahsusi hupatikana kwa mteja kutuma rasmi maombi TMA ya kupatiwa taarifa hizi. Katika kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinawafikia watumiaji wote, TMA imeendelea kuboresha mifumo ya usambazaji wa taarifa hizo kwa kutumia njia mbalimbali za usambazaji ikiwemo tovuti ya TMA, barua pepe, televisheni, redio za jamii, magazeti, mitandao ya kijamii na simu za mkononi. TMA pia ina programu za kuifikia jamii wakiwemo wanafunzi ili kuongeza uelewa juu ya sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na athari zake na mipango ya kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na upandaji miti, umuhimu na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA katika shughuli zao za kila siku. 

Katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2024, natoa rai kwa wadau wote kushiriki katika kujenga uelewa na kutumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ili kuendelea kuongeza tija na ufanisi katika kupanga na kutekeleza shughuli zetu za kijamii na kiuchumi, na kuchangia katika kuokoa maisha ya watu na mali zao kutokana na changamoto ya matukio ya hali mbaya ya hewa. Pia tunaendelea kuwakumbusha wadau wote kufuata na kuzingatia Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019 na kanuni zake ili kuhakikisha uendelevu na ufanisi wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania.

Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2024

““Kuwa Mstari wa Mbele Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi”.”

Siku ya Hali ya Hewa Duniani -2024

Dkt. Ladislaus Benedict Chang’a

KAIMU MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA); MWAKILISHI WA KUDUMU WA TANZANIA KATIKA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO); NA MAKAMU MWENYEKITI WA JOPO LA KIMATAIFA LA SAYANSI YA MABADILIKO YA HALI YA HEWA NA TABIANCHI (IPCC)

No comments:

Post a Comment