UJUMBE WA PROF. MBARAWA, WAZIRI WA UCHUKUZI KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI (WMD) - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 24 March 2024

UJUMBE WA PROF. MBARAWA, WAZIRI WA UCHUKUZI KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI (WMD)

 

Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (MB), Waziri wa Uchukuzi.

UJUMBE WA MHESHIMIWA PROF. MAKAME MNYAA MBARAWA (MB), WAZIRI WA UCHUKUZI KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI (WORLD METEOROLOGICAL DAY - WMD)”, 23 MACHI, 2024.

Ndugu wanahabari,

Mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yameendelea kuwa ni mojawapo ya changamoto kubwa katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu kidunia, kikanda na hata katika Taifa mojamoja ikiwemo Tanzania. Kasi ya ongezeko la joto imeendelea kuwa kubwa hususan katika miaka kumi (10) iliyopita. Tayari madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yanaonekana na yatakuwa makubwa zaidi tusipochukua hatua stahiki sasa. Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ni mojawapo ya Taasisi yenye mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kupitia utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta zote za kiuchumi na kijamii. Hapa kwetu Tanzania, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepewa jukumu hilo kisheria la kutoa, kuratibu na kudhibiti huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo kuchangia katika jitihada za Taifa za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Ndugu wanahabari,

Siku ya Hali ya Hewa Duniani ni kumbukizi ya kuanza kutumika kwa Mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) mnamo tarehe 23 Machi 1950. Hivyo, Siku ya Hali ya Hewa Duniani husherehekewa kila ifikapo tarehe 23 Machi ya kila mwaka kwa kuongozwa na ujumbe wa Kaulimbiu. Kaulimbiu ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka huu wa 2024 iliyopitishwa na nchi wanachama wa WMO, ni ”At the frontline of climate action”.  Kwa tafsiri inasema “Kuwa Mstari wa Mbele Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi”.

Ndugu wanahabari,

Lengo la Kaulimbiu hii ni kuhamasisha na kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi ambapo, moja ya hatua hizi kubwa ni kuimarisha mchango muhimu wa huduma za hali ya hewa kwa usalama na ustawi wa jamii. 

Ndugu wanahabari,

Lengo la 13 la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu (Sustainable Development Goal 13-Climate Action) linasisitiza nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa "kuchukua hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi; na athari zake." Utekelezaji wa lengo hili unachagiza maendeleo na mafanikio ya Malengo mengine yote ya Maendeleo Endelevu. Vilevile, “Mpango wa  Umoja wa Mataifa wa utoaji wa tahadhari kutokana na hali mbaya ya hewa kwa jamii yote-(Early Warning for All-EW4All)” uliozinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Novemba, 2022 unatoa wito kwa Ulimwengu mzima kufikiwa na mpango huu wa tahadhari yaani EW4ALL ifikapo mwishoni wa mwaka 2027. 

Ndugu wanahabari,

Kaulimbiu ya siku ya hali ya hewa Duniani na shughuli zitakazofanyika kwa mwaka huu 2024 zinalenga kuhamasisha utekelezaji kwa vitendo wa mipango hii ya EW4ALL na Lengo la 13 la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu, pamoja na utekelezaji wa mipango na mikakati mingine.

Ndugu wanahabari,

Katika kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani, Tanzania kama Mwanachama wa Shirika la hali ya Hewa Duniani na Umoja wa Mataifa haijabaki nyuma katika kuchukua hatua Madhubuti kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kwani yameendelea kuathiri utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kilimo, ujenzi, utalii, miundombinu, usafirishaji, nishati na afya. Mifano ya hivi karibuni ni mvua kubwa zilizochagizwa na uwepo wa El Nino na kusababisha vifo na uharibifu wa miundombinu hasa barabara na nyumba za watu.

Ndugu wanahabari,

Hatua zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na janga hili la mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, ni pamoja na uboreshaji wa huduma za hali ya hewa na uimarishaji wa mfumo wa utoaji tahadhari (Early Warning Systems) nchini. Uboreshaji huu pia ni sehemu ya utekelezaji wa ILANI ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 59 J ikiweka malengo ya kuimarisha miundombinu na huduma za hali ya hewa nchini. Aidha, uboreshaji huu pia ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Utoaji wa Huduma za hali ya hewa ili kufika kwa jamii katika ngazi zote nchini- National Framework for Climate Services-NFCS” kwa lengo hilohilo la kukabiliana na kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na kuhakikisha usalama wa chakula na afya pamoja na matumizi bora ya vyanzo vya maji.

Ndugu wanahabari,

Katika kuboresha huduma za hali ya hewa na tahadhari za hali mbaya ya hewa nchini, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya hali ya hewa ikiwa ni pamoja na ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kisasa ya upimaji na uchakataji wa taarifa za hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kompyuta kubwa  ya kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data za hali ya hewa. Kompyuta hii inaiwezesha TMA kuboresha na kuongeza usahihi wa utabiri wa hali ya hewa hususan kwa maeneo madogomadogo, ambapo huduma hiyo imeshaanza kutolewa hadi ngazi ya wilaya kwa utabiri wa mvua za msimu.

Ndugu wanahabari,

Aidha, Serikali iko hatua za mwisho kukamilisha mtandao wa jumla ya Rada saba (7) za hali ya hewa, ambapo katika kipidi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya sita, malengo ya ununuzi wa Rada nne (4) yamefikiwa. Kati ya hizo Rada mbili zinakamilishwa kufungwa katika mikoa ya Mbeya na Kigoma na utengenezaji wa rada nyingine mbili (2) zitakazofungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma unaendelea kiwandani nchini Marekani na zinatarajiwa kukamilika na kufungwa mwaka huu wa 2024. Rada nyingine tatu (3) zimekamilika na kufungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mtwara. Hatua hii inaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Kikanda (Afrika Mashariki) kuwa na idadi kubwa ya rada za hali ya hewa na kuimairisha huduma za uangazi na utabiri wa matukio ya hali mbaya ya hewa. 

Ndugu wanahabari,

Vilevile, Serikali imetambua changamoto kubwa iliyopo kwa baadhi ya maeneo yanayoathirika na radi za mara kwa mara na imenunua seti tano (5) za vifaa vya utambuzi wa matukio ya radi (Lighting detectors) ambavyo vimefungwa katika maeneo ya Musoma, Mwanza, Kagera (Bukoba), Tabora na Kigoma (Kibondo). 

Ndugu wanahabari,

Kwa kutambua kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa nchi yetu, Serikali imewezesha ununuzi wa vituo kumi na tano (15) vya kupima hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe (Automatic Weather Stations) ambavyo vitafungwa katika vituo vya utafiti na maendeleo ya kilimo ili kuchagiza utafiti kuhusiana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa sekta ya kilimo. 

Ndugu wanahabari,

Katika kuimarisha huduma za hali ya hewa kwa ajili ya usafiri wa anga, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuimarisha mtandao wa vituo na uwezo wa uchakataji taarifa, ikiwemo ununuzi na ufungwaji wa vifaa vya kisasa vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe (AVIMET) vinavyosaidia kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa ndege zinaporuka na kutua.

Ndugu wanahabari,

Hatua nyingine zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha hali ya hewa na ufuatiliaji wa Tsunami cha Kanda ya Mashariki, Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha ufuatiliaji wa matukio ya hali mbaya ya hewa hususan yanayoanzia baharini na ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 39. 

Ndugu wanahabari,

Uboreshaji huu wa miundombinu unaenda sambamba na kuwajengea uwezo wataalamu wa hali ya hewa na watumishi katika sekta hii na wameendelea kupatiwa mafunzo mbalimbali ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya sita jumla ya watumishi 228 (Wanaume 177 na Wanawake 51) wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi ya diploma (33), shahada ya kwanza (90), Shahada ya Uzamili (79) na Shahada ya Uzamivu (16) kupitia vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.

Ndugu wanahabari,

Katika duru za kimataifa, kwa kutambua mchango wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, tarehe 06 Septemba 2023 wakati wa Kongamano la 23 la Afrika la masuala ya hali ya hewa na tabianchi (African Climate Summit 23) lililofanyika Nairobi, Kenya Mheshimiwa Rais aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabia nchi (Advisory Board of the Global Centre on adaptation). Vilevile, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus B. Chang’a alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (Intergovernmental Panel on Climate Change - IPCC) katika uchaguzi wa viongozi wapya wa IPCC uliofanyika tarehe 26 Julai 2023, Nairobi Kenya wakati wa Mkutano wa 60 wa IPCC; Ikumbukwe kuwa pia hapo nyuma aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt.Agnes Kijazi, alishawahi kuchaguliwa kushika nafasi ya juu ya uongozi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ya kuwa Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika hilo (2019-2022). Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu katika juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi Nchini na Duniani kwa ujumla.

Ndugu wanahabari,

Haya ni baadhi tu ya mafanikio machache kati ya mengi ambayo yanatokana na Serikali kuendelea kuchukua hatua za kuboresha na kuimarisha huduma za hali ya hewa hapa nchini kwa kutenga fedha katika bajeti ya Maendeleo ya kila mwaka.

Serikali inathamini kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika kutoa huduma na taarifa za hali ya hewa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi nchini. Aidha, natoa rai kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na mashirika ya Serikali na yasiyo ya kiserikali kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za hali ya hewa. 

Ndugu wanahabari,

Mwisho, nawakumbusha na kuwasisitiza wananchi na WADAU wote wa hali ya hewa kuendelea kutumia ipasavyo taarifa za hali ya hewa kwa kuzingatia miongozo na Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019. 

“Kuwa Mstari wa Mbele Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi”

Siku ya Hali ya Hewa Duniani - 2024

Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa (MB)

Waziri wa Uchukuzi

No comments:

Post a Comment