![]() |
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akitoa salamu katika Misa Takatifu ya Kumbukizi ya Miaka Mitatu ya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi Wilayani Chato Mkoani Geita tarehe 17 Machi, 2024. Kushoto ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shingella.
Maono ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya Kitaifa kama Ujenzi wa Bwawa la Nyerere, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kama vile Daraja la Kigongo - Busisi yametekelezwa na yanaendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko katika Misa Takatifu ya kumuombea
Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, iliyofanyika katika
Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi Wilayani Chato Mkoani
Geita.
“Niwahakikishie
Watanzaniza kuwa miradi yote ambayo Hayati Dkt. Magufuli akiwa Rais wa Nchi
yetu, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaiendeleza yote kwa kasi kubwa ili
tumuenzi kwa vitendo”, amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ameeleza
kuwa Watanzania watamkumbuka Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa uwezo wake wa
kiuongozi, karama yake ya kutatua changamoto za wananchi pamoja na
kuwasikiliza, kuondoa kero mahali penye kero, kuhimiza uwajibikaji Serikalini
kwa kuondoa uzembe, ubadhirifu na rushwa.
Katika Misa hiyo,
Naibu Waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko ameongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa
kanisa jipya la Mtakatifu Yohana Maria Muzeyina na kuweza kukusanya takribani
Milioni 169 pamoja na vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake,
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kumpa nafasi ya Uwaziri katika Wizara ya Ujenzi ambayo Hayati Dkt.
John Pombe Magufuli alihudumia miaka 20.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Martine Shingella amemshukuru Rais Samia kwa kutimiza ndoto za Hayati
Magufuli za kujenga barabara kuunganisha Mkoa wa Geita na Shinyanga kwa kiwango
cha lami ambapo tayari Serikali imesaini
mtakataba wa ujenzi kilometa 73 kwa kiwango cha lami kuanzia Kahama hadi
Kakola.
Kwa niaba ya Famia ya
Hayati Magufuli, Jesca Magufuli, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kuwa karibu na familia kuwafariji, kuwajali na kuwapatia matunzo yote kadri
awezavyo.
Jesca ameongeza kuwa
kama familia wataendelea kumuenzi na kumkumbuka Hayati Dkt. Magufuli kwa namna
alivyowapenda na kuwawekea misingi mizuri ya kuchapa kazi na kumtanguliza Mungu
mbele kwenye kila jambo.
Misa ya Kumbukizi ya
Miaka Mitatu tangu alipofariki Hayati Dkt. John Pombe Magufuli imeongozwa na
Makamu Askofu, Padri Ovan Mwenge na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali, Chama
cha Mapinduzi (CCM), ndugu, jamaa na marafiki.




No comments:
Post a Comment