![]() |
| Kutoka kulia ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila wakikagua Daraja la Jangwani. |
![]() |
| Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (kushoto) akitoa maelekezo alipokagua kazi ya kuzibua tope katika Daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam. |
![]() |
Msafara wa Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa,
Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Bw. Albert Chalamila wakikagua Daraja la Jangwani. |
![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mchengerwa katika ziara hiyo. |
WAZIRI wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa amewataka Mameneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na Mameneja wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kushirikiana kikamilifu katika kipindi hiki cha mvua za vuli ili kuhakikisha barabara zote nchini haziathiriki na mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote.
Akizungumza alipokagua Daraja la Jangwani, Barabara
ya Mwendokasi, Barabara ya Njia nane Kimara-Kibaha, Kibamba shule –Mpiji Magoe KM
9.2 na Barabara ya Kimara-Bonyokwa-Kinyerezi KM 7, jijini Dar es Salaam Mhe.
Bashungwa amewataka watendaji wote wa Wakala hizo kwenda maeneo ya kazi ili
kuhakikisha mifereji ya maji inazibuliwa na athari zinazojitokeza wakati wa
mvua zinadhibitiwa kwa wakati.
“…Sisi Mawaziri tunashirikiana katika kutafuta
ufumbuzi wa changamoto za miundombinu hivyo naagiza kuanzia sasa Watendaji
Wakuu wa TANROADS na TARURA, Mameneja na wafanyakazi kufanya kazi kwa
ushirikiano ili kuwaondolea kero wananchi na hivyo kusafiri kwa uhakika,”
amesema Waziri Bashungwa.
Amewataka wananchi kuacha kutupa taka hovyo katika mitaro ya barabara na mabonde ya maji na kuacha shughuli za uchimbaji mchanga pembezoni mwa madaraja hali inayosababisha mmomonyoko wa udongo na kusababisha uharibifu wa barabara na madaraja.
| Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa aki zungumza na baadhi ya wakazi wa wanaotumia Barabara ya Kimara-Bonyokwa-Kinyerezi KM 7, mara baada ya kuikagua jijini Dar es Salaam. |
Amewaonya wananchi na taasisi mbalimbali kuacha
kutumia hifadhi za barabara kufanya biashara kwani kufanya hivyo ni kinyume cha
sheria na usalama wa watu na mali zao na kuwataka Mameneja wote wa TANROADS nchini
kuhakikisha hifadhi za barabara
zinalindwa.
Kwa upande wake Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed
Mchengerwa amemshukuru Waziri wa Ujenzi kwa ushirikiano anaompa na
kumhakikishia ushirikiano huo utaendelezwa hususan katika ujenzi wa Daraja la Jangwani
na Bonde la Msimbazi ili kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi wa
kudumu.
“Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi hakikisheni
usafi wa mazingira unapewa kipaumbele katika maeneo yenu ili kuruhusu maji ya
mvua yaweze kupita kwa urahisi na hivyo kutoleta athari kwa miundombinu,”
amesisitiza Waziri Mchengerwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert
Chalamila amewataka wananchi kutoa taarifa kwa haraka pindi wanapobaini athari
za barabara na madaraja ili kuepuka madhara zaidi.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa yupo katika ziara ya kukagua miundombinu ya barabara na madaraja jijini Dar es salaam kuona athari za mvua na kutoa maelekezo ya hatua za haraka kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.
![]() |
| Muonekano wa eneo la Daraja la Jangwani, ambalo kazi ya uzibuaji tope inaendelea hivi sasa. |







No comments:
Post a Comment