UTAFITI WA MRADI WA EFLOWS WAONESHA MAJI YANAPUNGUA KWENYE MITO - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Tuesday, 19 September 2023

UTAFITI WA MRADI WA EFLOWS WAONESHA MAJI YANAPUNGUA KWENYE MITO

Wadau wa maji wa mto Mbarali wilayani Mbarali mkoani Mbeya wakiwa kwenye kikao cha mawasilisho ya Matokeo ya Utafiti wa miaka miwili kuangalia Mtiririko wa maji na afya ya mto huo kilichoketi juzi wilayani humo.

Na Calvin Gwabara, Mbarali

MATOKEO ya Utafiti wa miaka miwili kuangalia Mtiririko wa maji na afya ya Mto Mbarali Mkoani Mbeya yameonesha kuwa Maji yanapungua na hii ni kutokana na ongezeko la watu na mahitaji ya matumizi ya maji kuongezeka sambamba na uharibifu wa vyanzo vya maji vya mto huo.

Hayo yamebainishwa na Prof. Japhet Kashaigili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa miaka miwili wa Utafiti  wa Usimamizi Endelevu wa Madakio ya Maji Kupitia Tathmini ya Kuimarisha Mtiririko wa Maji kwa Mazingira na Utekelezaji wake katika Kulinda Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Athari za Shughuli za Kibinadamu Tanzania (EFLOWS) wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wadau wa maji wa mto Mbarali wilayani humo Mkoani Mbeya.

“Tulichokiona kwenye utafiti ni kwamba wingi wa maji kwenye mto unaendelea kupungua, wahitaji wa maji wanaongezeka lakini pia mabadiliko ya tabia nchi nayo yameathiri kwa kiasi kikubwa mtawanyiko wa maji na mvua kwenye maeneo haya na hivyo kupelekea maji kupungua mtoni na athari zake hasi zikionekana kwenye mifumo ikolojia ya mto hasa wakati wa kiangazi. Tumeona uwepo wa matumizi makubwa ya maji bila vibali kwa kutumia pampu, na uzalishaji mkubwa wa mchanga wakati wa mvua kutokana na shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo milimani na kwenye mashamba” alisema Prof. Kashaigili.

Aliongeza” Shughuli za kibinadamu zinazofanyika Mbarali kwa maana ya makazi, kilimo, ufugaji, ufyatuaji wa matofali kwenye vyanzo vya maji na mtoni, kilimo cha vinyungu, moto na shughuli zingine za kibinadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa mtawanyiko wa maji kwenye mto, lakini uchukuaji wa maji kwenye mto ndio umeonekana kuongoza kwa athari hasi”.

Prof. Kashaigili amesema changamoto hiyo ya matumizi makubwa ya maji imepelekea mto kukauka kabisa maeneo ya chini wakati maeneo ya juu ya mto na katikati ukifika unakuta maji mengi yanatiririka ambayo hayafiki mwisho yanaishia njiani kutokana na watu kuyachepusha na kuyachota kwaajili ya shughuli zao mbalimbali hususani kilimo ambacho hakizingatii matumizi sahihi ya maji hayo.

“Kwa maana hii ni kwamba Mto Mbarali hauchangii chochote kwenye Mto Ruaha Mkuu hasa wakati wa kiangazi kwenye maeneo ya uhifadhi na hii maana yake ikolojia ya mto na uendelevu wake imeathirika na hivyo kushindwa kufikia malengo makubwa ya Kidunia ya maendeleo endelevu na yale ya kitaifa ya kuifadhi na kuilinda baonuai ya mto” alifafanua Mtafiti huyo Mkuu Prof. Kashaigili.

Mtafiti huyo aliyebobea kwenye tafiti za Masuala ya maji na Mazingira Duniani amesema pamoja na Utafiti kutoa matokeo hayo kwa wadau hao.

Mtaalamu wa Sayansi za maji na Viumbe wake kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Bw. Sherald Mkama akizungumzia matokeo hayo mbee ya Waandishi wa habari nje ya mkutano huo.
Mtafiti aliyekuwa anaangalia mimea iotayo kandokando ya mito na vyanzo vya maji Dkt. Emmanuel Mwainunu kutoka Taasisi ya utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) akizungumzia eneo la utafiti wake.

 Mtafiti Mkuu wa Mradi wa EFLOWS Prof. Japhet Kashaigili kutoka SUA akiwasilisha matokeo ya mradi huo wa utafiti wa miaka miwili mbele ya wadau.

No comments:

Post a Comment